Na ELIUD NGONDO, SONGWE,
MJI wa Tunduma ni kati ya miji iliyopo mipakani. Mji huu umekuwa ukipokea magari mengi yanayosafirishwa kwenda nchi jirani, kama vile Malawi na Zambia, huku mengine yakibeba bidhaa na abiria.
Tunduma ipo wilayani Momba, Mkoa mpya wa Songwe na imekuwa ni moja ya miji hapa nchini inayokua kwa kasi. Kwa kipindi kirefu, mji huu haukuwa kwenye mpangilio mzuri.
Kijiografia Mji wa Tunduma unapatikana umbali wa takribani kilomita 103 kutoka Jiji la Mbeya na ni umbali wa kilomita 31 kutoka Mji wa Vwawa, yalipo makao makuu ya Mkoa wa Songwe.
Tunduma, kwa mujibu wa Sensa ya watu na makazi ya mwaka 2012 una jumla ya wakazi 180,153 ambapo wanawake ni 95,487 na wanaume 84,666 na ukiwa na mwingiliano wa watu kutoka mataifa mengine, zikiwamo nchi za Zambia na Congo.
Mji huo ambao ni miongoni mwa miji ya kibiashara ni chanzo cha ongezeko la pato la Taifa kutokana na kuwapo kwa mpaka wa nchi mbili ya Tanzania na Zambia, maarufu kwa jina la Boda ya Tunduma, ambapo ni lango kuu la kuingia na kutoka nchi za kusini mwa Afrika.
Serikali kwa sasa ipo katika mradi mkubwa wa kuuweka katika mpangilio mzuri na kuweka barabara za mitaa, magulio, sehemu za maegesho ya magari na huduma nyingine za kibinadamu.
Mkurugenzi Mtendaji wa mji huo, Valery Kwembe, anasema kuweka mji huo katika mipango miji kutapunguza msongamano wa magari ambayo ilikuwa ikilalamikiwa kwa muda murefu bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.
Anafafanua kuwa, mji huo una ukubwa wa eneo la kilomita za mraba 42,000, ambapo wananchi wake wamekuwa wakijishughulisha zaidi na biashara, huku wakulima wa mazao ya chakula wakiwa ni wachache.
Anasema wameamua kuingia gharama za kupima viwanja maeneo mbalimbali ili kuweza kupunguza shida iliyokuwapo ambapo wameshaanza kwa baadhi ya maeneo ambayo ni Migombani, Kaloleni, Mtaa wa Nyerere na kuyapatia hati miliki kwa watakaokuwa wakinunua.
“Kutokana na mji wetu kuwa lango kuu la kuingilia katika nchi za Zambia, Kongo na mataifa mengine ya kusini, mji huu ulikuwa unakabiliwa na changamoto ya msongamano wa
magari yanayoelekea katika mataifa hayo, sasa baada ya kuanza kuupanga mji tayari msongamano huo unaonekana kupungua kwa kasi,” anasema Kwembe.
Ni dhahiri kuwa, foleni iliyodumu kwa muda wa miaka mingi katika Mji wa Tunduma imeanza kupungua kutokana na uongozi wa mji huo kutengeneza barabara za mitaa ambazo zinatumika kama mbadala wa barabara kuu na hivyo kupunguza msongamano huo.
MTANZANIA lilitembelea mji huo na kujionea kupungua kwa msongamano uliokuwa ukisumbua mji wa Tunduma kwa miaka ya kuanzia 2000 hadi 2014, ambapo wananchi pamoja na madereva walikuwa wakipata shida kupita.
Kuwapo kwa mpango mji kutasaidia kupunguza adha ya uchafu na shida ya maji ambayo ilikuwa miongoni mwa kero zilizodumu miaka mingi.
Mkurugenzi huyo anasema mkakati wa kupanga mji huo umekuwa na manufaa makubwa.
Kwembe anasema awali mpango huo ulianza kwa magari madogo (IT) ambayo yalianza kuwekwa kwenye maegesho yaliyopo katika maeneo ya Chapwa na Mpemba na hivyo kubakia magari makubwa yenye mizigo kuegeshwa kwenye maegesho ya Tunduma.
Anaeleza kuwa, baada ya kufanya zoezi hilo la kutoziruhusu hizo gari IT kuegeshwa katika mji wa Tunduma, foleni zilianza kupungua.
Kwembe anasema katika kuhakikisha suala hilo linakamilika, wameanza kupanua barabara kuu ili kuweza kuweka mpishano wa magari na kuondoa msongamano.
Anasema halmashauri hiyo ilianza kulima njia zote za mitaa katika mji wa Tunduma na kuwafanya wananchi wawe huru katika kubomoa nyumba zao kwa hiari bila malipo.
“Awali kabla ya kupasua njia za mitaa kulikuwa na vibaka wengi katika mji wetu, ambao walikuwa wakiwapora watembea kwa miguu,” anasema Kwembe.
Anasema kutokana na kuchepusha barabara hizo za mitaa, watumiaji wa baiskeli, pikipiki na bajaji wameanza kutumia barabara hizo za mitaa tofauti na walipokuwa wakitumia barabara kuu ya Tanzania na Zambia na kusababisha msongamano wa magari.
Mbunge wa Jimbo la Tunduma, Frank Mwakajoka, anasema suala la mji huo kuwekwa katika mpango miji linalenga kuwarahisishia wananchi kuweza kupata huduma za kijamii kirahisi.
Anasema mji ukipangwa kwa kitaalamu unakuwa na huduma nyingi, ikiwamo kunusuru mali za raia, hususan linapotokea janga la moto kwa kwa madai kuwa, magari kikosi cha Zimamoto na Uokoaji yanaweza kufika kwa urahisi zaidi.
Mwakajoka anasema kutokana na hali hiyo, waliunda umoja uliowahusisha viongozi wa Serikali na wanasiasa, ili kuwashawishi wananchi na kuwapatia elimu juu ya athari za mji kutokuwa katika mpangilio.
“Magari kwa sasa yanaweza kupita njia ambazo zimetengenezwa na foleni sasa imepungua, tofauti na ilivyokuwa awali ambapo magari asilimia kubwa yalikuwa yakitumia njia moja ambayo inaelekea nchi ya Zambia,” anasema Mwakajoka.
Mkuu wa Wilaya ya Momba, Juma Irando, anasema mji wa Tunduma kuwekwa kwenye mpango mji imekuwa ni fursa katika idara ya ulinzi ambapo doria imekuwa ikifanyika mtaa kwa mtaa.
“Mji wowote ukiwa katika mpangilio mzuri hata suala la ulinzi linakuwa si tatizo, kwani askari wetu wanakuwa wanafanya doria ya kuhakikisha wananchi wanakuwa katika hali ya usalama,” anasema Irando.
Mmoja wa wakazi wa mji huo, Michael Wiliam, anasema kitendo cha uongozi wa mji huo kuwahamasisha wananchi kubomoa kwa hiari nyumba zao kumepunguza uhalifu uliokua ukifanywa na vibaka.