27.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, February 8, 2023

Contact us: [email protected]

WiLDAF: WANAWAKE NI MHIMILI WA UCHUMI

Wanawake wajasiriamali wakiwa kwenye mkutano

Na ASHA BANI,

TAKWIMU za sensa za mwaka 2012 zinaonesha kwamba wanawake ni asilimia 51.7 ya Watanzania wote ambao idadi yao ni 44,928,923.

 Wanawake wengi wanajishughulisha na kilimo cha mazao ya chakula, kazi za ufundi kama vile ushonaji, udarizi wa nguo, ususi wa nywele, mikeka na biashara ndogo ndogo ili kuweza kupata mahitaji ya familia.

Wanawake pia wanashiriki kwenye kilimo cha mazao ya biashara katika kuongeza nguvu kazi, lakini hawana uwezo wa kumiliki ama kutumia mapato yatokanayo na mazao hayo, ambapo mara nyingi huchukuliwa na kumilikiwa na wanaume.

Kaimu Mkurugenzi wa Shirika la Wanawake katika Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WiLDAF), Anna Kuyara, anasema kwa wanawake ambao wamekuwa wakijishughulisha na biashara ndogo ndogo, wamekuwa wakikabiliwa na changamoto za kukosa mitaji.

Anasema licha ya kuwa wanawake ni wengi zaidi ya wanaume, wanawake wanakumbana na changamoto zinazowafanya kushindwa kufurahia matunda ya kazi zao na kuzidi kuongeza umaskini na utegemezi, mambo ambayo yanasababisha ukatili wa kijinsia.

Kutokana na changamoto hizo zinazosababisha ukosefu wa kipato, baadhi ya wanawake na wasichana hujiingiza katika biashara zisizokuwa halali, ikiwa ni pamoja na biashara ya ngono na wengi wakijikuta wanaishia katika vitendo vya udhalilishwaji, ikiwa ni pamoja na kubakwa, kulawitiwa, kupigwa na hata kukashifiwa.

MIKATABA YA KIMATAIFA

Mikataba ya kimataifa ya haki za wanawake kiuchumi Tanzania ni miongoni mwa nchi iliyosaini mikataba hiyo, ambayo ni mkataba wa kimataifa wa haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni wa mwaka 1966.

Mkataba wa kimataifa wa kuondoa aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake (CEDAW) wa mwaka 1979 na mkataba wa nyongeza wa Afrika wa haki za binadamu za wanawake.

Kuyara anasema mikataba hiyo inatoa wajibu kwa nchi wanachama, Tanzania ikiwamo, kuweka fursa na mazingira ya usawa baina ya wanawake na wanaume katika nyanja ya kiuchumi ili kuwa na maendeleo endelevu.

WAJIBU WA SERIKALI

Anasema Serikali inawajibika kuhakikisha kwamba watu wote, wanawake kwa wanaume, bila kujali rangi, jinsi, lugha, dini, siasa, kabila, hali ya mtu, wanapata fursa sawa za kiuchumi na wanatumia fursa hizo bila ubaguzi.

Pia serikali haipaswi kutengeneza sheria itakayowanyima watu fursa ya kutengeneza umoja wao wa kiuchumi na kibiashara.

SHERIA NA HAKI KWA MWANAMKE

Anasema Serikali inatambua uwepo wa tatizo la ukatili wa kijinsia kiuchumi, hususan kwa wanawake.

Hivyo basi, Serikali imetunga sheria mbalimbali kuweza kuhakikisha uwepo  wa fursa na haki sawa za kiuchumi baina ya wanawake na wanaume kwa ajili ya maendeleo endelevu.

Machi 8 wakati wa uzinduzi wa Siku ya Mwanamke Duniani, WilDAF iliiomba Serikali kufanyia marekebisho Sheria ya Mali za mirathi ya mwaka 1963, ili iweze kwenda na mahitaji ya sasa.

Kuyara alisema sheria hiyo imekuwa kandamizi na kusababisha usumbufu, vilio, hususani kwa wajane, jambo ambalo linaweza kumalizika iwapo Serikali itakubali kuyafanyia kazi maombi yao.

Kuyara alisema, sheria hiyo imekuwa haimtambui mjane, licha ya kuwa miongoni mwa waliosaidiana na mume wake kuchuma mali.

Aidha, alisema kwa zaidi ya miaka 20 sasa, kumekuwapo na jitihada za wadau kuiomba Serikali kuifanyia marekebisho sheria hiyo, lakini mpaka sasa imekwama bila kujua sababu.

Anasema iwapo sheria hiyo itabadilishwa, itaweza kumnyanyua mwanamke, hasa katika suala zima la kujikwamua kiuchumi.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Shirika hilo, Naomi Kaihura, alisema: “Tusimame kidete sisi wanawake kwa umoja wetu, tatizo tunashindwa kutekeleza yale tunayoyapanga, umefika wakati sasa tukasimama na kuitaka Serikali itekeleze mapendekezo yetu.

 “Tuidai Serikali mabilioni kama si matrilioni  ya wanawake waliodhulumiwa mirathi…wanawake wengi wanadhulumiwa haki zao na hao hao wa mahakamani.”

Anasema miongoni mwa watu wanaorudisha nyuma jitihada za wajane ni wafanyakazi wa serikalini ambao nao ni wajane.

Awali, akifungua mkutano huo kwa niaba ya aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Dk. Harrison Mwakyembe, Mkurugenzi wa Huduma za Kisheria kwa Umma wa Wizara hiyo, Justus Njara, alisema suala hilo wanalifahamu na walilipokea rasmi mwaka 2010.

Alisema walishindwa kuendelea nalo, hasa baada ya kuanza kwa mchakato wa mabadiliko ya Katiba mpya, wakidhani mambo mengi yataingizwa, hasa kutokana na kushirikisha watu wengi zaidi.

“Toeni tu azimio la upole upole, wala msitumie nguvu kubwa kwa sababu suala hili ni gumu, kwani linagusa mila na desturi za makabila mbalimbali na dini tofauti tofauti,” alisema Njara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,871FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles