Na Dennis Luambano – Same
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba, amesema anakusudia kulitangaza eneo la Ndolwa lililopo Kata ya Mamba Myamba, Wilaya ya Same mkoani Kilimanjaro, kuwa ni hatarishi na kuwataka wananchi wanaoishi kuhama na kuacha shughuli za kibinadamu.
Kusudio hilo alilitangaza mjini hapa jana baada ya kuombwa na Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule, kutokana na kuwapo kwa dalili za awali na hatarishi za kutokea maporomoko ya ardhi katika eneo hilo.
January aliyetembelea wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya kukagua shughuli za uhifadhi wa mazingira, alisema watalitangaza kama eneo linalolindwa kwa mujibu wa sheria ya mazingira kifungu cha 51 na 52.
“Tumeamua tutalitangaza rasmi kama ni eneo hatarishi. Watu wa NEMC (Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira) watafanya tathmini ya kitaalamu ya athari ya mazingira kisha nitalitangaza katika Gazeti la Serikali.
“Hatutaki kuona maafa yanatokea kwa mara ya pili katika eneo hilo,” alisema January.
Licha ya kusudio la kulitangaza, pia alisema watazingatia utashi wa wananchi wanaoishi katika eneo hilo ili kuepusha migogoro.