25 C
Dar es Salaam
Saturday, November 16, 2024

Contact us: [email protected]

MAZOEZI HUZUIA AROSTO INAYOSABABISHWA NA DAWA ZA KULEVYA

Dk. Fredirick L Mashili, MD, PhD.

TUNAFAHAMU kwamba mazoezi yanazo faida nyingi katika miili yetu, ikiwemo ile ya kutukinga na hata kuponya baadhi ya magonjwa.

Tafiti zinaonyesha kwamba, mazoezi yakiwa sehemu ya matibabu, yanauwezo mkubwa wa kuzuia na kudhibiti athari zitokanazo na kuzoea kutumia dawa za kulevya. Dalili za athari hizi huitwa arosto. Tafiti hizo zinaonyesha kwamba kufanya mazoezi mara kwa mara kukichanganywa na matibabu ya kawaida ya tatizo hili husaidia kuondoa dalili hizo mbaya kwa haraka. Matibabu mengine yanayotibu arosto hivyo kusaidia kuondokana na dawa ya kulevya ni pamoja na ushauriwa kisaikolojia pamoja na dawa kama vile methadone.

Fahamu kwamba mtu aliyezoea kutumia dawa za kulevya hushindwa kuacha kutokana na mabadiliko ambayo hutokea mwilini mwake pindi anapozikosa. Mabadiliko hayo humsababishia maumivu, uchovu na dalili nyingine nyingi ambazo husita pindi anapotumia dawa tena.

Zifuatazo ni faida tano za mazoezi katika kudhibiti athari za matumizi sugu ya dawa za kulevya:

Mazoezi hukupa nguvu, kujiamini na uwezo wa kufanya kazi

Mojawapo ya dalili ambazo husababishwa na arosto ni kukosa nguvu, kutokujiamini na kushindwa kufanya shughuli za kawaida. Mazoezi hukupa nguvu, kujiamini na uwezo wa kufanya kazi. Mazoezi yana uwezo wa kuongeza vichocheo kama vile testosterone ambavyo hukufanya kupata nguvu na kuwa na uwezo wa kufanya kazi.

Mazoezi hukufanya kujisikia mwenye furaha (euphoria).

Kitu kikubwa kinachowafanya watu kuanza na kuendelea kutumia dawa za kulevya ni ile hali ya kujisikia furaha au kwa lugha ya Kiingereza feeling high au kitaalamu euphoria. Kibaiolojia kujisikia furaha husababishwa na kuongezeka kwa vichocheo vinavyofahamika kitaalamu endorphinsna endocarnabinoids. Kufanya mazoezi husaidia kuongeza kiwango cha vichocheo hivi kitu ambacho hukufanya ujisikie mwenye furaha. Kwa maana hiyo baadala ya kuongeza vichocheo hivyo kwa njia yenye madhara, ni bora kufanya hivyo kwa kupitia mazoezi

Mazoezi husaidia kupunguza uzito. Kwa mtumiaji sugu wa dawa za kulevya kuacha kufanya hivyo husababisha kuongezeka uzito kwa kasi. Jambo hili huweza kumfanya kujisikia vibaya kitu ambacho huchangia kuwafanya baadhi ya watu kuendelea kuwa watumwa wa dawa za kulevya. Watumiaji sugu wa dawa za kulevya hupata matatizo ya kukosa usingizi pale wanapojaribu kuacha kutumia dawa. Kufanya mazoezi mara kwa mara, hutokomeza tatizo hili.

Mazoezi hukufanya kutumia vizuri muda wako wa ziada

Kama unajaribu kuacha kutumia ni muhimu kuwa na kitu cha kufanya ili usishawishike. Kufanya mazoezi ni njia nzuri ya kutumia muda wako wa ziada kitu ambacho hukuweka mbali na dawa hizo.

Mazoezi hukuondolea tatizo la sonona na msongo wa mawazo

Mojawapo ya dalili zinazoambatana na arosto ni pamoja na hali ya kujisikia mwenye huzuni (sonona) na wakati mwingine msongo wa mawazo. Mazoezi yanafahamika kwa uwezo wake wa kupunguza vichocheo ambavyo husababisha sonona na msongo wa mawazo. Kufanya mazoezi mara kwa mara hupunguza kiwango cha kichocheo kinachoitwa cortisol ambacho kimsingi husababisha msongo wa mawazo.

Kama hujawahi kufanya mazoezi kabisa anza kwa kufanya taratibu na ikiwezekana tafuta rafiki wa kufanya naye.

Dk. Mashili ni mtaalamu wa fisiolojia ya mazoezi na homoni. Pia ni mhadhiri katika chuo kikuu cha sayansi na tiba Muhimbili (MUHAS). Kwa maelezo zaidi unaweza wasiliana naye kwa kutumia: namba 0752255949, baruapepe, [email protected]. Unaweza pia kujifunza zaidi kwa kutembelea mojawapo ya tovuti zake: www.jamiihealthtz.com au www.jamiiactive.org

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles