Na MWANDISHI WETU,
NANCY Sumari si jina geni nchini Tanzania. Tangu mwaka 2005 aliposhinda tuzo ya kuwa mrembo wa Tanzania na kuwa mshindi wa Miss World Africa amekuwa ni simulizi ya kuvutia.
Akiwa na uzoefu wa kuwa mjasiriamali wa ukweli – Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Bongo5 Media na hali kadhalika Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Neghesti Sumari na Jenga Hub.
Hamasa iliyotokana na Jenga Hub ni kutaka kutatua changamoto zilizopo ndani ya jamii.
Wiki iliyopita Tigo Tanzania kwa kushirikiana na asasi isiyo ya kiserikali ya Reach for Change, ilimpatia tuzo ya Dola za Marekani 20,000 baada ya kuwa mshindi mwenza wa shindano linaloitwa Waleta Mabadiliko Kidijitali wa Tigo akitoka miongoni mwa washiriki 350. Mshindi mwingine ni Sophia Mbega ambaye aliwavutia majaji kwa ubunifu mkubwa wa kidijitali ambao ulijielekeza katika kusaidia makundi ya wanawake kujisaidia wenyewe katika mpango unaoitwa Benki za Jumuia Vijijini (VICOBA).
Jenga kama lilivyo neno lenyewe ambalo Nancy amelitumia kuunda ubunifu wake wa Jenga Hub, unalenga kuwapatia watoto na vijana fursa za kuwa wataalamu wa kidijitali. Wanapatiwa nafasi ya kuandaa, kuunda na kuchanua kupitia teknolojia za kidijitali. Ubunifu huo unaangalia uwiano uliopo kati ya muundo na uhuru katika kujifunza kupitia mchakato wa teknolojia.
“Ninafurahi kushinda tuzo hii; nitahakikisha natumia fedha hizi vizuri kuendeleza maudhui yangu ili kuweza kuwasaidia watoto kuzifikia ndoto zao za baadaye,” anasema Nancy na kuongeza;
“Naishukuru mno Tigo na Reach for Change kwa kuanzisha wazo hili zuri ambalo hadi sasa limezaa matokeo chanya kwa jamii.”
Akielezea jinsi ubunifu wake wa Jenga Hub unavyofanya kazi, Nancy anasema inawapatia watoto fursa sahihi ya kujifunza program za kompyuta, stadi za kiroboti na kuweka alama. Ubunifu huo pia unawawekea wazi watoto misingi ya kujifunza Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) kama vile stadi za program ambazo zinaweza kugeuzwa na kutumika katika malengo mapana ya kielimu na burudani.
Watakaojiunga watawezeshwa kutumia zana zinazokuwapo katika kompyuta kuanzisha kazi za sanaa, kuchora picha, kuigiza, kuanzisha mtandao wa wavuti, kufanya sanaa za kiroboti, kutunga muziki, uwasilishaji kupitia zana kadhaa habari na mengineyo.
“Jenga Hub inatoa miundo ya kozi, stadi za kompyuta na matumizi mengine ya msingi,” anasema.
Shindano la Waleta Mabadiliko
Shindano hilo linalenga kutambua na kusaidia wajasirimali jamii ambao wanatumia zana na teknolojia za kidijitali kuboresha na kuleta mabadiliko ndani ya jamii pamoja na kizazi kijacho.
Mbali na msaada huo wa kifedha, washindi wamepewa nafasi ya kuitumia Reach for Change ambayo hutoa ushauri, utaalamu na namna ya kufikia mitandao mingine duniani ambayo inawawezesha kujenga ujasirimali endelevu wa kifedha ambao unaleta mabadiliko makubwa na ya kudumu.
Kwa mujibu wa Meneja Mkuu wa Tigo, Diego Gutierrez Waleta Mabadiliko ambao tayari wako ndani ya program hiyo wameyagusa maisha ya watoto zaidi 250,000 nchini Tanzania.
“Tunaamini kwamba kwa nyongeza hii ya waleta mabadiliko tutaleta mabadiliko katika maisha ya watoto wengi zaidi na kusaidia kuifanya Tanzania kuwa sehemu nzuri kwa vizazi vijavyo,” anasema Gutierrez wakati wa hafla ya kutoa tuzo hizo jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa mwezi huu.
Gutierrez aliendelea kufafanua kwamba kama nembo ya maisha ya kidijitali Tigo inatoa msukumo kwa mawazo na miradi inayoendeshwa na teknolojia ambayo yanaleta mabadiliko endelevu.
“Teknolojia ya kidijitali si tu inabadilisha namna ambavyo tunafanya biashara ndani ya Afrika, bali pia inaleta mapinduzi kwa njia tofauti na kutatua masuala ya maendeleo ya jamii.
“Hivyo, kutokana na heshima hii kubwa ni kwamba kwa mara nyingine tunaunda fursa kwa mawazo hayo kutambuliwa, kuungwa mkono na kubadilisha hadi kiwango cha juu cha matokeo ya kijamii na kiuchumi,”anasema.
Huu ni mwaka wa tano ambapo Tigo na Reach for Change wanatangaza washindi wa shindano hilo. Washindi wanaoingia fainali ambao huchaguliwa kutoka kundi la mamia ya wajasirimali jamii ambao wametumia zana za na teknolojia kupata suluhisho kwa matatizo yanayoikabilia jamii ya Watanzania.
Gutierrez aliwapongeza washindi waliotangulia na papo hapo akitoa msukumo kwa wengine kushirikiana mawazo yao.
“Mkusanyiko wetu katika ujasiriamali jamii unavutia mno. Hadi sasa tumeshasaidia Waleta Mabadiliko ya Kidijitali nchini Tanzania na tunatarajia kuwasaidia wajasiriamali jamii wengi zaidi kila mwaka ili kusukuma mkakati wetu mbele,” anafafanua Meneja huyo.
Anasema; “tumekuwa msaada mkubwa kwa kazi zote za Waleta Mabadiliko wetu na mwaka huu tunatarajia kuangalia namna ya kusaidia mashujaa wawili zaidi na wajasiriamali jamii walio wabunifu.”