KWA matukio yanayoendelea hivi karibuni ningependa kujiuliza tu kama hii ni ile nchi yangu niliyoizoea yenye uhuru wa kuzungumza, yenye kupanga mipango shirikishi ya maendeleo, yenye demokrasia ambako kila chama kilikuwa kinaweza kunadi sera zake wakati wa uchaguzi na hata baadaye, wakilindwa na polisi, nchi ambayo hapakuwa na kamata kamata!
Niliwahi kuandika na ninakumbushia tu, kuwa ukiwa kiongozi na waliokuchagua wanakuwa tayari kukupatia ushauri, basi unakuwa na bahati sana, kwa sababu wanataka wabebe sehemu ya lawama kama mambo yakienda mrama, lakini kwa sababu vichwa vingi huleta baraka, basi wanapokuwa pamoja na wewe kiongozi hakuna kitakachoharibika. Wakati wa Nyerere hili lilikuwa likizingatiwa sana ndio maana aliomba vijiji viunde mifumo yao ya utawala na wafanye uamuzi wao kwa faida yao.
Tukaja tukaharibu sisi wenyewe kwa kudhani kuwa ubepari ungeweza kutupeleka mbele zaidi, kwa kudhani kuwa viongozi kwa kufanya uamuzi bila kushirikisha wananchi tungeweza kuleta maendeleo na kwa sasa kudhani kuwa kuwakataza watu wasifanye uamuzi kabisa na kila kitu kifanywe ikulu tunaweza kuleta maendeleo.
Maendeleo, kama alivyosema Mwalimu Nyerere, huletwa na watu, siasa safi na uongozi bora. Watu, alikuwa akimaanisha wanaoweza kujitambua, walioandaliwa vyema, waliosoma na wenye ujuzi, wazalendo, waliochana na tabia za ufisadi, wanaolinda amani ya nchi na tayari kuwatii viongozi wao kwa maelekezo na maamrisho yote yaliyo halali na ya kisheria.
Siasa safi alikuwa akimaanisha kuwa na mfumo wa itikadi unaowafanya watu waipende nchi yao, kuwahamasisha na kuwajengea mwamko, yenye kuhakikisha kuna demokrasia na uhuru wa kujieleza, uhuru wa kuchagua viongozi wao na kuwatengua, siasa ambazo hazijengi chuki wala ubaguzi na ambazo viongozi ni watumishi wa umma.
Uongozi bora ni ule unaotambua kuwa uko madarakani kwa sababu wananchi ndio waliokuweka, na ambao unatambua kuwa kama usipowashirikisha wananchi hakutakuwa na maendeleo. Uongozi bora haujali maslahi ya waliochaguliwa bali ya Taifa zima, unaojenga misingi ya haki bila kujali rangi, mifumo ya imani, kabila au jinsia ya mtu.
Lakini tunakoelekea sasa si katika misingi hii iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere! Kuna viongozi wastaafu, Jaji Joseph Warioba na wenzake, waliosema kuwa kwa sasa hivi nchi imegawanyika katika makabila mapya ya kivyama na si ile ya makabila ya kijadi.
Ukiwa wa kabila fulani wewe si mwenzetu na huwezi kushirikiana na sisi, imefikia hatua hata Rais anasema kuwa kutembeleana katika nyakati za masahibu ni kusalitiana. Imefika wakati huko Unguja watu hawasalimiani kwa kupeana mikoni na wala hawazikani, maji ya visima yanachafuliwa na ukiwa wa kabila la kisiasa lisilo letu hupewi kazi, wala cheo na unaweza ukatafutiwa sababu hata ya kubuniwa tu na ukafukuzwa kazi kabisa.
Uongozi huu hatutaki kuona watu wakishangilia chama kingine na wale wa chama kingine hawataki kusikia chochote kutoka kwa uongozi, ili mradi tu tuonekane kuwa sisi ni watu tofauti. Tulidhani ukabila huu wa kisiasa ni ule wa wakati wa uchaguzi tu na hasa katika kutafuta kura, si katika mengineyo na baada ya hapo tunarudi tena kwenye maisha kama Taifa moja. Lakini mwelekeo sasa ni kuwa baada ya uchaguzi mambo yanaendelea… wewe ulikuwa kule na ulifanya kosa basi hatukutaki.
Mwaka mmoja na miezi mitano baada ya uchaguzi tunaona viongozi wanafukuzwa uanachama, wananyang’anywa kazi zao, wanaambiwa wasaliti, hawatakiwi. Mwaka mmoja baadaye tunaendelea kutafutana kujua alikuwa wa kabila gani la kisiasa na sasa, ati mwaka mmoja baadaye, tunadhani bado ni wa kabila lile na hapaswi kuwa na sisi. Tunasahau kuwa makabila yale ya kisiasa yalikuwa ya muda tu… na hatukuwa na mpango wa kuyaendeleza baada ya kiongozi mpya kuchaguliwa.
Hii si nchi niliyozaliwa na kukulia.. si nchi ile ambayo niliahidiwa ingekuwa! Si ile nchi niliyoambiwa kuwa maendeleo hayana chama na hivyo sitakiwi kuwa na hofu hata kama aliyeshinda uchaguzi ni wa kabila la siasa asiye wa kabila langu. Naiomba ile nchi irudi na nadhani ikirudi maendeleo ya kweli yatapatikana!
[embedyt] https://www.youtube.com/watch?v=MjfYMVLABts[/embedyt]