32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAGUFULI ARIDHIA KUIPA KENYA MADAKTARI 500

Na AGATHA CHARLES – Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli ameridhia ombi la kuipatia nchi ya Kenya madaktari 500 ambao tayari Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imetangaza nafasi za ajira hizo.

Ombi hilo liliridhiwa Ikulu, Dar es Salaam jana baada ya Dk. Magufuli kuzungumza na ujumbe wa viongozi wa Wizara ya Afya ya Kenya uliotumwa na Rais Uhuru Kenyatta.

Kenyatta aliomba madaktari 500 kutoka nchini watakaosaidia kukabiliana na tatizo la uhaba wa madaktari katika vituo vyake vya tiba, hasa baada ya kutokea mgomo wa madaktari ambao ulidumu kwa takriban siku 100.

Hata hivyo, mgomo huo umeripotiwa na vyombo mbalimbali vya habari vya ndani na nje ya nchi hiyo kuwa ulimalizika kwa kusaini makubaliano baina ya Chama cha Madaktari chini ya Mwenyekiti wake, Oroko Samuel na Waziri wa Afya, Dk. Cleopa Mailu, mbele ya viongozi wa kidini.

Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais-Ikulu, Gerson Msigwa na ile ya Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, ilieleza sifa za madaktari wanaopaswa kuomba nafasi hizo.

Ummy alisema ajira hizo zitawahusu madaktari ambao hawajaajiriwa serikalini (hawapo katika utumishi wa umma au taasisi za Serikali), waliomaliza mafunzo kwa vitendo na ambao wamesajiliwa na Baraza la Madaktari la Tanganyika (MCT).

“Kigezo kikubwa cha sifa za madaktari ambao watapata ajira hiyo ya mkataba Kenya ni ambao hawapo katika utumishi wa umma, asiwe ameajiriwa au anafanya kazi katika hospitali teule au hospitali za taasisi binafsi wanaolipwa mshahara na Serikali. Jambo la pili lazima awe amemaliza mafunzo ya vitendo (internship), pili awe amesajiliwa na MCT na vigezo vingine,” alisema.

Ummy aliendelea kusema kuwa Tanzania ina madaktari wa kutosha, hivyo wanaweza kupelekwa Kenya kwa ajira hiyo ya mkataba wa miaka miwili ambayo maombi yalifunguliwa kuanzia jana hadi Machi 27.

Alisema madaktari hao watatakiwa kuwa na hati za kusafiria, hivyo wajiandae kwa ajira hiyo ya haraka.

Akijibu swali la waandishi waliotaka kujua kwanini madaktari hao wanakwenda kufanya kazi nchini Kenya, Ummy alisema hilo linatokana na madaktari wa huko kudai kufanya kazi kwa muda mrefu.

Sababu nyingine alisema ilitokana na upungufu wa madaktari baada ya tangu mwaka 2013 Serikali nchini humo kuamua kushusha madaraka chini (mikoani) na mgomo ulioathiri huduma za afya.

Alisema kuwa Rais Magufuli aliomba kuhakikishiwa usalama wa madaktari watakaofanya kazi huko na kwa kuwa tuko ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), hivyo ni sifa kwa nchi.

Ummy alisema Tanzania inazalisha madaktari 1,200 kwa mwaka, lakini si wote wanaopata ajira kutokana na uwezo wa kiuchumi.

Awali, taarifa ya Ikulu ilisema kiongozi wa ujumbe huo, Dk. Mailu alimweleza Rais Magufuli kuwa Kenya ina upungufu mkubwa wa madaktari ambao hauwezi kumalizwa kwa kutegemea wanaosomeshwa nchini humo bali kupata madaktari kutoka nje ya nchi.

Katika ujumbe huo ambao pia alikuwepo Gavana wa Kisumu, Jack Ranguma, Dk. Mailu alisema Kenya ipo tayari kuwalipa stahili zote madaktari 500 watakaopatiwa kutoka nchini ikiwa ni pamoja na mishahara na nyumba za kuishi.

Katika ombi hilo, Rais Magufuli alimtaka Ummy kuharakisha mchakato wa kuwapata madaktari hao ili wawahi kwenda kutekeleza jukumu hilo.

“Matatizo ya Kenya ni matatizo ya Tanzania, tutawapatia madaktari hao 500 ili wakatoe huduma ya matibabu kwa ndugu zetu waliopo Kenya, na kwa kuwa mmenihakikishia kuwa madaktari wangu mtawalipa mishahara inavyotakiwa, mtawapa nyumba za kuishi, na mtahakikisha wanafanya kazi katika mazingira mazuri na salama, mimi sina tatizo na naamini mambo yatakwenda vizuri,” alisema Magufuli.

Naye Katibu Mkuu Utumishi, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema hakuna athari zitakazojitokeza kwa nchi kupeleka madaktari Kenya kwa kuwa wapo madaktari zaidi ya 1,000 hawajapata ajira.

Alisema uwezo wa nchi kuajiri kwa mwaka ni madaktari 450 na ajira zinatolewa kulingana na uwezo wa bajeti husika.

Itakumbukwa kuwa mgomo huo wa Kenya uliodumu kwa siku 100 ulisababisha mahakama ya masuala ya wafanyakazi nchini humo kuwahukumu jela kwa muda wa mwezi mmoja viongozi saba wa Chama cha Wahudumu wa Afya (KMPDU).

Madaktari hao 5,000 kutoka hospitali 2,000 za umma walianza mgomo wiki ya kwanza ya Desemba, mwaka jana wakiitaka Serikali kuheshimu makubaliano ya mwaka 2013 ya kuwaongezea mishahara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles