NA CHRISTOPHER MSEKENA
TEKNOLOJIA imechukua nafasi yake kwenye biashara ya muziki kwa njia ya mtandao, kila uchwao yanabuniwa masoko mapya yenye lengo la kuzipa thamani kazi za sanaa hasa audio na video za muziki.
Kwa Tanzania tumeshuhudia masoko mapya yakitengenezwa kwa mfumo wa tovuti ambapo shabiki anaweza kupata audio au video ya wimbo wa msanii anayempenda kwa kuchangia gharama ndogo ya fedha.
Ni mfumo uliowanufaisha wasanii kwa kuwaongezea chochote kitu kwenye vibubu vyao japo kumekuwa na changamoto nyingi mfano wasanii kutokupata malipo wanayostahili kutokana na ukweli kuwa tovuti nyingi haziweki wazi taarifa za mauzo.
Kwa muda mrefu duka la kimtandao la mkito.com limekuwa likitegemewa na wasanii wakubwa kwa wadogo katika biashara ya kuuza nyimbo na tovuti hiyo ndiyo imeasisi biashara hii inayochukua sura mpya kila kukicha.
Si audio tu hivi sasa mpaka masoko ya kuuza video yamebuniwa na tayari wasanii wanapiga fedha ndefu kwa kuuza kazi zao. Jana Ijumaa staa wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, naye ameingia kwa miguu miwili kwenye biashara hiyo.
Amezindua tovuti yake ya wasafi.com ambayo lengo lake ni lile lile la kuuza nyimbo za wasanii wa Tanzania na wale wa nje ya nchi. Kilichomsukuma kuanzisha duka hilo la kimtandao ni changamoto ambazo zimekuwepo kwa muda mrefu katika muziki wa Bongo Fleva.
Ujio wa tovuti hii unaleta sura mpya ya mafanikio katika vita ya kupigania haki za wasanii kunufaika na jasho lao ili watimize wajibu wao wa kulingana na mapato wanayoingiza.
Wasafi.com inafungua ukurasa mpya wa mapambano ya kibiashara kati ya tovuti moja na nyingine kwa vipimo vya kutazama ubora wa huduma hasa uwazi baina ya mmiliki wa tovuti na msanii anayepeleka bidhaa yake sokoni.
Muziki wetu bado unakuwa, unahitaji kuwa na soko huria la nyimbo za wasanii ili mwanamuziki awe na uhuru wa kupeleka kazi yake kwenye tovuti yoyote anayoona itamwingizia kipato.
Mkito na Wasafi hazitoshi, japokuwa ujio wa tovuti hii ya Diamond unaweza kuamsha hamasa ya wadau wengine kuwekeza kwenye teknolojia ili kutuletea masoko mengine zaidi yenye lengo la kuipa thamani kazi ya msanii.