Na ELIYA MBONEA-ARUSHA
SIKU moja baada ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (Chadema), kuachiwa kwa dhamana, mke wake, Neema Lema, amesema kuna baadhi ya watu wana roho za shetani na sasa wanahangaika baada ya kushindwa.
Kauli hiyo aliitoa jana alipozungumza na MTANZANIA Jumapili kwa simu alipoulizwa alipokeaje dhamana ya mumewe aliyekaa mahabusu miezi minne katika Gereza Kuu la Kisongo.
Alisema kitendo cha mumewe kupewa dhamana kimeibua furaha ya ushindi kwa ndugu na wanafamilia, ambao kwa kipindi chote alichokaa mahabusu walikuwa wakimwombea.
“Najua wapo watu hawajafurahia kuona Lema amepata dhamana, unajua hata shetani akishindwa huwa anahangaika,” alisema Neema na kuongeza:
“Sisi familia yote na hasa mimi kama mke, tumepokea ushindi huu kwa unyenyekevu mkubwa na kumshukuru Mungu.”
Akielezea mazingira ya nyumbani kwake baada ya Lema kufika na kuonana na watoto wake, alisema: “Kwa ujumla alifurahi na siwezi hata kukuelezea, familia yote tumekuwa na furaha. Baada ya marafiki na viongozi wa chama kuondoka, alitumia muda mrefu kumwomba na kumshukuru Mungu kwa jinsi alivyoonekana kwake. Hivi sasa (jana) tunavyozungumza saa 4:40 asubuhi bado amelala.”
Neema pia alisema kuwa Lema aliwaombea watuhumiwa wengine aliowaacha mahabusu.
“Anajua amewaacha katika mazingira gani ndiyo maana ameahidi kuendelea kuwaombea mbele za Mungu,” alisema Neema aliyekuwa akienda Gereza la Kisongo kwa kipindi chote mumewe alichokaa mahabusu kumpelekea chakula.
Lema alipewa dhamana juzi na Mahakama Kuu Kanda ya Arusha.
Kutolewa kwa dhamana hiyo kuliibua shangwe na vifijo katika viwanja vya mahakamao na licha ya wafuasi wa Chadema, pia viongozi wakuu wa chama hicho walikuwapo mahakamani.