25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MUUGUZI AFUKUZWA KAZI KWA KUSABABISHA KIFO

TIMOTH ITEMBE Na BENJAMIN MASESE-TARIME

BARAZA la Madiwani Halmashauri ya Wilaya ya Tarime mkoani Mara, limemfukuza kazi muuguzi wa kitengo cha dawa za usingizi katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime, Jackson Nega, baada ya kudaiwa kuomba na kupokea rushwa na kusababisha vifo vya wajawazito watatu kwa nyakati tofauti.

Wakati Nega akifukuzwa kazi, naye Ofisa Utumishi wa halmashauri hiyo, Gevarson Kaguma, ameshushwa cheo kwa kosa la uzembe kazini  ambao umesababisha watumishi wa halmashauri hiyo kufanya kazi kwa mazoea na kushindwa kuandaa taarifa za watumishi kupandishwa madaraja.

Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao cha dharura cha Baraza la  Madiwani ambapo kilihudhuriwa na Mbunge wa Jimbo la Tarime Mjini, Esther Matiko (Chadema), Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Elias Ntiruhungwa, Katibu Tawala wa Wilaya, John Marwa, mganga wa hospitali hiyo pamoja na viongozi mbalimbali.

Kabla ya kufikiwa kwa uamuzi huo, baraza hilo lilijigeuza kuwa kamati kwa ajili ya kujadili taarifa za uchunguzi wa watumishi hao ambao walisimamishwa tangu Januari 6, mwaka huu baada ya kutuhumiwa na wagonjwa kwa kupokea rushwa na kutoa lugha chafu wakati wa utoaji huduma katika hospitali hiyo.

Akitoa maazimio yaliyofikiwa na kamati hiyo mbele ya waandishi wa habari, Mwenyekiti wa halmashauri hiyo, Khamis Nyanswi, alisema kamati imepitia kwa kina taarifa ya tume ya uchunguzi wa tuhuma hizo na kuwahoji watuhumiwa na kujiridhisha kwamba muuguzi Nega alipokea rushwa kutoka kwa wagonjwa kwa nyakati tofauti na kutoa lugha chafu.

Pia alisema ilibainika mtumishi huyo amekuwa na tabia hiyo kwa muda mrefu na ameonywa kwa barua mara kadhaa na mkuu wake wa kazi, lakini hakuweza kubadilika hadi aliposimamishwa Januari 6, mwaka huu kwa ajili ya tuhuma za kuchelewesha dawa kwa mjamzito aliyetakiwa kujifungua kwa upasuaji na kusababisha kifo chake na mtoto.

“Tumepokea taarifa za uchunguzi, tumezipitia na kujiridhisha muuguzi Nega alipokea rushwa na kutoa lugha chafu kwa wagonjwa, pia alisababisha kifo cha mjamzito wakati wakiwa chumba cha upasuaji baada ya kuchelewesha dawa za usingizi.

“Wapo baadhi ya watumishi waliopewa onyo katika sakata hilo la rushwa kwa sababu ya kuomba rushwa, kama tunakumbuka hivi karibuni kuna vifo vitatu vilitokea hapa eti sababu inaelezwa kwamba ni rushwa, vitendo hivi vikijirudia tutachukua hatua nyingine.

“Kwa leo tunamchukulia hatua za kumfukuza kazi muuguzi Nega na kumvua cheo ofisa utumishi wa halmashauri ili iwe fundisho kwa watumishi wengine wenye tabia hizi,” alisema Nyanswi.

Naye Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Ntiruhungwa, alisema anaunga mkono uamuzi uliochukuliwa dhidi ya watumishi hao kwani vitendo hivyo vimekuwa vikirudisha nyumba juhudi za kuboresha huduma kwa wagonjwa na kuchafua sifa ya hospitali ya wilaya.

Kwa upande wa Mbunge wa jimbo hilo, Esther, alisema hatua zilizochukuliwa kwa watumishi hao ni sahihi na wanaendelea na mkakati wa kuhakiukisha watumishi wengine wenye tabia hiyo wanasitisha kama si kuacha mwenendo wao wa kuomba rushwa wakati wa utoaji huduma.

“Ninavyojua huyu muguuzi Nega yeye alisababisha kifo cha mjamzito mmoja na mtoto wake wakiwa chumba cha upasuaji, lakini wale wanawake wengine wawili wao vifo vyao vilisababishwa na wauguzi wengine, tumeanza kuchunguza mazingira yalivyokuwa ili hatua zichukuliwe,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles