26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

SERIKALI INA KAULI MBILI ZINAZOKINGANA JUU YA HALI YA CHAKULA NCHINI

SIKU nzima ya juzi nilikuwa natakiwa na waandishi wa habari kutoa maoni yangu kuhusu uteuzi wa Mtanzania mwenzetu na mke wa Rais aliyepita, Mama Salma Kikwete kuwa Mbunge wa Bunge la Jamhuri wa Muungano wa Tanzania.

Niliwaambia sina maoni yoyote. Jana baada ya magazeti kuandika maoni ya watu mbalimbali nimeulizwa tena. Jibu langu ambalo ninaliweka hapa kwa umma ni kwamba, Mama Salma Kikwete ana haki zote kama Mtanzania mwingine yeyote kuteuliwa ama kuchaguliwa kwa mujibu wa Katiba yetu. Hivyo uteuzi wake kwa maoni yangu ni kama teuzi nyengine zozote zile.

Kuolewa kwake na aliyekuwa Rais hakumwondolei yeye haki zake za kikatiba. Kama mwenyewe ataridhia ninamtakia kila la kheri katika kazi yake mpya. Sababu za kuteuliwa kwake anazijua aliyemteua na baadhi ya wasomi wabobezi kama Prof. Kitila Mkumbo, wamenukuliwa wakifanya uchambuzi mzuri kabisa kwenye gazeti la The Citizen la jana.

Kwangu mimi kwa maoni yangu, nchi yetu inakabiliwa na mambo makubwa zaidi ya kujadili na kutolea maoni ikiwemo suala la njaa. Serikali kwenye suala hili la njaa imeyumba sana na kwa kiasi flani imewayumbisha pia wananchi wanyonge wanaokabiliwa na tatizo hili na kwa maoni yangu naamini kabisa Serikali haijatekeleza wajibu inavyostahili. Kama mzalendo kwa taifa langu nachukua wajibu wangu kuonyesha mapungufu hayo ya Serikali pamoja na kutoa njia mbadala.

Jana, Serikali kupitia Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kusisitiza kuwa haitatoa chakula cha msaada kwa Watanzania watakaokabiliwa na njaa. Rais alisema: “Tumezoea kuambiwa maneno matamu matamu kwamba hakuna mtu atakeyekufa kwa njaa. Mimi nawaambia usipolima utakufa na njaa.”

Serikali kwa kauli za namna hii inawachanganya Watanzania, kwanza ni muhimu sana kujua (na naamini Serikali inajua) kuwa wananchi hawa wamelima, suala la hali ya njaa si kwa sababu ya kutokulima kwao, bali ni kwa sababu kadhaa zilizo nje ya uwezo wao, ikiwemo hali ya hewa yenye mvua chache.

Mfano mikoa ya Singida, Shinyanga na Tabora wananchi wetu walilima, lakini mvua hazikunyesha kabisa, mahindi yalikauka na majaruba ya mpunga hayakuwa na maji kabisa kati ya Desemba na Januari ambacho ndicho kipindi cha msimu wa kilimo kwa mikoa hiyo. Sasa Serikali kupitia Rais inapowaambia wananchi kuwa ‘wasipolima watakufa na njaa’ si sawa, ni kama vile tunaihusianisha njaa na wao kutolima, jambo ambalo si kweli.

Rais wetu si tu ni Amiri Jeshi Mkuu wa Taifa letu (Commander In Chief) bali pia anapaswa kuwa Mfariji Mkuu (Comforter In Chief) kwa watu wetu katika nyakati za majanga kama matetemeko ya ardhi, mafuriko na ukame ambao unasababisha njaa.

Kazi kuu ya Serikali yoyote ni ugavi wa matumaini kwa wananchi na Rais wa nchi anapaswa kuwa kiongozi wa kugawa matumaini hayo, hatusemi Serikali itoe matumaini hewa, lakini pia hatukubali Serikali ‘ivunje moyo wananchi’ kwa kuhusisha hali ya ukame na wao kutokulima. Hili si sawa.

Januari 31, mwaka huu Serikali ilitoa tamko juu ya suala la njaa, tamko husika lilitolewa na Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi, kwamba kuna halmashauri 55 zinazokabiliwa na njaa na kwamba Serikali itapeleka chakula cha bei nafuu ili kuhakikisha kuwa wananchi katika halmashauri hizo 55 hawafi njaa. Serikali hapa ilichukua jukumu lake la kutoa matumaini kwa wananchi hawa.

Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi ni mteule wa Rais, ni sehemu ya Serikali hii, sasa mkuu wa Serikali husika anaposema kuwa ‘watu walime na hakuna chakula cha msaada’ anafuta matumaini haya na si tu kufuta matumaini kwa wananchi lakini pia anawachanganya wasaidizi wake ambao wanaweza kuogopa kutekeleza msimamo wa Serikali uliotolewa bungeni na Waziri wa Kilimo, Chakula na Uvuvi wa kupeleka chakula cha msaada katika halmashauri hizo 55.

Kuogopa kupeleka chakula maeneo yenye njaa na hivyo kusababisha Watanzania kupoteza maisha. Ninarudia kauli yangu kwamba iwapo Mtanzania yeyote atakufa kwa njaa hatutakuwa na budi kumwajibisha Rais kwa kutumia Katiba.

Utafiti wa Shirika la Twaweza wa Februari 2017, unaonyesha kuwa theluthi ya Watanzania (Watanzania milioni 17) hivi sasa wanalala njaa ama kushinda na njaa. Pia nusu ya Watanzania wanakabiliwa na upungufu wa chakula. Hawa wanahitaji matumaini kutoka kwa Serikali na si taarifa mbili tofauti za Serikali zinazojikanganya.

Ni muhimu wananchi waelewe kuwa suala la njaa na ukame si jipya nchini, mwaka 2006 na 2007 nchi ilikumbwa na ukame mkubwa sana na Rais wa wakati huo alitamka kuwa ‘hakuna Mtanzania atakayekufa kwa njaa’. Tuliona Serikali nzima chini ya kiranja wao, Waziri Mkuu ikizunguka nchi nzima kuhakikisha kuwa ‘hakuna Mtanzania anakufa kwa njaa’.

Kwanini Serikali ilifanya hivyo mwaka 2006/7? Ni kwa sababu Katiba inatamka kuwa kila Mtanzania ana haki ya kuishi na ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kuwa haki hii ya kuishi inalindwa. Ndio maana Serikali ilianzisha Wakala wa Akiba ya Chakula (NFRA) kwa lengo la kuhakikisha tuna akiba ya chakula cha kutosha na kwamba ikitokea kuna majanga ya asili kama ukame basi ‘Mtanzania hafi kwa njaa’.

Naiasa Serikali itekeleze wajibu wake huu wa kikatiba, ihakikishe hakuna Mtanzania anayekufa kwa njaa. Kushindwa kufanya hilo ni kushindwa kulinda Katiba.

 

Mwandishi wa uchambuzi huu ni Mbunge wa Kigoma Mjini

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles