NAIROBI, KENYA
RAIS wa Kenya, Uhuru Kenyatta na Rais Jakaya Kikwete wamekubaliana magari ya Tanzania yaruhusiwe kuingia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyata na safari za ndege za Shrika la Ndege la Kenya (Kenya Airways) ziruhusiwe ziendelee na safari zake kama kawaida nchini Tanzania.
Katibu Mkuu wa Mambo ya Nje wa Kenya, Amina Mohammed, alisema uamuzi huo ulifikiwa jana katika mkutano kati ya Rais Jakaya Kikwete na Uhuru Kenyatta mjini Windhoek Namibia, katika sherehe za maadhimisho ya 25 ya Rais wa tatu wa Jamhuri ya Namibia, Hage Geingob.
Wakuu hao wawili walikutana na kujadiliana masuala ambayo yalijadiliwa na mawaziri wao wa utalii kuhusu kuruhusiwa kwa magari hayo ya Tanzania kuingia uwanja wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta bila ya kutozwa ushuru kama ilivyofanyika katika wiki mbili zilizopita kitendo kilicholalamikiwa.
Katika makubalino hayo, Tanzania imekubali kuziruhusu ndege za Kenya kutua katika viwanja vya ndege nchini kama ilivyokuwa awali
Tanzania ilichukua uamuzi wa kupunguza safari za ndege za Kenya katika viwanja vyake baada ya Kenya kuzuia magari ya utalii nchini kuingia uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta kama ilivyokuwa mwanzo.
Yamekuwapo malalamiko ya muda mrefu kwa wakenya wanaofanya shughuli za utalii wakisema kuwa wamekuwa wakipata vikwazo katika mbuga za Tanzania lakini kwa upande wa Kenya watanzania wamekuwa hawapati vikwazo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania, Benard Membe ametangaza kurejea kwa uhusiano kati ya nchi hizo.
Majibu ya Tanzania kuhusu mgogoro huo yalionekana kuwa na athari kubwa kwa Kenya kutokana na kuathiri uendeshaji wa shirika la ndege la Kenya.