32.2 C
Dar es Salaam
Monday, November 25, 2024

Contact us: [email protected]

MSUMBIJI WAMEMSAHAU MWL. NYERERE, SAMORA?

Mwalimu Nyerere (kulia) akiwa na Samora Machel

Na Baligagwe Mwambungu,

ILIKUWA ni sera ya Tanzania ya kuunga mkono juhudi za Ukombozi wa Bara la Afrika, hasa Kusini mwa Afrika. Na hii haikuwa kwa bahati mbaya, ulikuwa ni msimamo thabiti wa mwasisi wa Taifa la Tanganyika, Mwalimu Julius Nyerere, ambayo baada ya kuungana na  Zanzibar mwaka 1964, ikazaliwa Tanzania.

Nyerere aliamini katika umoja, ndiyo maana alikuwa tayari kuahirisha uhuru wa Tanganyika, ili nchi za Afrika Mashariki—Tanganyika, Kenya na Uganda, zipate uhuru kwa pamoja. Alijua kuwa nchi hizo zikiungana na kuwa taifa moja, lingekuwa taifa lenye nguvu.

Nyerere katika baadhi ya hotuba zake, anasema vinchi vidogo vidogo vya Kiafrika, bila kuungana, vilikuwa haviwezi kuwa na sauti mbele ya mataifa makubwa. Ikumbukwe kwamba wakati huo kulikuwa na vita baridi kati ya nchi za Magharibi zikiongozwa na Marekani, na nchi za Mashariki (kikomunisti) zikiongozwa na iliyokuwa Jamhuri ya Kisoviet ya Urusi.

Mwalimu Nyerere pamoja na viongozi wa nchi huru za Kiafrika, wakaunda Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Mei 23, 1963, baada ya vuta nikuvute nyingi. Ilipotokea nafasi ya kuungana na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar baada ya Mapinduzi ya 1964, Nyerere hakusita kukubali kuziunganisha Tanganyika na Zanzibar.

Bahati mbaya hakuna nchi nyingine iliyojiunga na Muungano huo, ambao tunaweza kusema ulitoa fursa ya kipekee kwa nchi za Afrika Mashariki—Kenya na Uganda ambazo zilikuwa tayari zimepata uhuru.

Hii ilitokana na mzozo wa ndani nchini Uganda, na kutokuwa na utashi wa kisiasa kwa upande wa Kenya. Lakini pia ni ukweli kwamba nchi hizo zilishindwa kujiunga kwenye Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kwa sababu ya utamu wa madaraka. Mwasisi wa Taifa la Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, alikubali kujishusha alipomwambia Mwalimu Nyerere katika mazungumzo ya kuunda Muungano: “Wewe Rais, Mimi Makamu.”

Nyerere aliamini kwamba ingelikuwa rahisi kwa  Kenya, Uganda kuungana na Tanganyika, kwa sababu zilikuwa na mambo yanayofanana. Zote  zilitawaliwa na Uingereza na zote zilikuwa nchi changa.

Pili, Serikali ya Malkia wa Uingereza ilianzisha Kamisheni ya Afrika Mashariki (The East African High Commission), kabla ya nchi hizo kupata uhuru, lakini jina hilo lilibadilishwa na Uingereza kabla ya Tanganyika kupata uhuru wake, Desemba 9, 1961 na kuitwa The East African Common Services Organisation (EASCO). Viongozi wapya wa nchi za Afrika Mashariki walirith EASCO na wakaiona kuwa ilikuwa fursa ya kuziunganisha nchi hizo katika kutafuta umoja wa kisiasa na maendeleo ya pamoja.

EASCO ambacho kilikuwa ni chombo cha utoaji wa huduma za pamoja, kilihusika na mambo ya  usafiri na usafirishaji, reli, bandari, barabara, mawasiliano na posta, biashara na viwanda, ushuru na forodha, utafiti na huduma za jamii, utawala na fedha.

Baada ya Uganda na Kenya kupata uhuru, uwezekano wa kuunda Shirikisho la Afrika Mashariki, viongozi wake hawakuonyesha utashi wa kisiasa. Itoshe tu kusema kuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Uganda, Milton Obote, aliingia katika mzozo na Rais Edward Mutesa,  ambaye alikuwa ni Kabaka (Mfalme) Mutesa II wa Buganda. Mutesa akakimbilia uhamishoni Uingereza na Obote akajitangaza kuwa Rais mwaka 1966.

Uganda ilipata uhuru mwaka 1962, ikifuatiwa na Kenya mwaka 1963, lakini hazikuchukua fursa ya kutafuta umoja wa kisiasa wa Afrika Mashariki kama ilivyotarajiwa. Kimsingi viongozi wa Kenya, Uganda na Tanganyika,  walikuwa wamekubaliana kuwa wangeunda Shirikisho la Afrika Mashariki baada ya kuibadilisha EASCO na kuwa Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC). Jumuia ilianzishwa rasmi Februari 3, 1967, na kurithi mambo yote yaliyokuwa yakisimamiwa na EASCO. Bahati mbaya EAC ilivunjika mwaka 1977, kutokana na tofauti za kisiasa na msigano wa sera za kiuchumi na kijamii.

Tofauti hizo zilianza kujitokeza baada ya Tanzania kutangaza Azimio la Arusha Februari 3, 1967 na  Rais Obote wa Uganda, ambaye pia alikuwa Rais wa Uganda People’s Congress, akatangaza The Common Man’s Charter, Oktoba 24, 1968 ambayo dhima yake pia ilikuwa sawa na siasa ya Ujamaa iliyokuwa imetangazwa na Mwalimu Nyerere.

Kwa mtazamo huu, msimamo wa Nyerere na Obote ukachukuliwa kama ulilenga kuidhoofisha Kenya, ambayo bado ilikuwa inaendelea na sera ya uchumi wa kibepari.

Sera ya mambo ya ndani na nje ya Tanzania, ilijikita katika Azimio la Arusha—sera ambayo ilitamka wazi na chama tawala cha Tanganyika African National Union (TANU)—kwamba  Afrika ni moja na Waafrika ni ndugu.

Kwa hiyo, Tanganyika ikawa imeonyesha toka mwanzo, kwamba ilikuwa tayari kushiriki katika ukombozi wa Bara la Afrika. Na ni katika misingi hiyo, ikawa tayari kushirikiana na nchi nyingine za Kiafrika kuunda Umoja wa Afrika.

Ni katika muktadha huo, Tanzania ikawa kitovu cha Kamati ya Ukombozi wa Afrika na kimbilio la wakimbizi kutoka sehemu mbalimbali za Afrika—ikiwamo Afrika Kusini, Namibia, Zimbabwe, Angola, Mozambique na kwingineko.

Vyama vya wapigania uhuru kama FRELIMO—the  Mozambique Liberation Front,  Zimbabwe African National Union (ZANU), Movement for the Liberation of Angola (MPLA) na South West Africa People’s Organisation (SWAPO) of Namibia, vilikuwa na ofisi zao Tanzania na Zambia.

Wananchi wa Tanzania walitoa mchango mkubwa—wa hali na mali, kuwasaidia ndugu zao wa Kiafrika katika nchi ambazo zilikuwa zikikandamizwa na wakoloni na masetla wa Kireno, Kizungu na Makaburu wa Afrika Kusini. Siyo siri tena kwamba, askari wa Kitanzania walipigana vita ya msituni kuwasaidia ndugu zao wa Mozambique (Msumbiji) na wengine kupoteza maisha. Tanzania ikawa adui mkubwa wa utawala wa makaburu, Wareno na walowezi wa Rhodesia.

Kulikuwa na idadi kubwa ya watu wa Msumbiji hapa Tanzania, lakini tofauti na wakimbizi wa sasa kutoka Congo (DRC) na Burundi, ambao hukaa katika kambi, wakimbizi kutoka Msumbiji walikubaliwa na kuishi ndani ya jamii ya Kitanzania. Hawakubaguliwa au kutengwa. Walianza kurudi kwao na mali waliyochuma Tanzania baada ya nchi yao kujinyakulia uhuru Juni 25, 1975.

Leo hii tunapoona na kusikia kwamba Msumbiji inawapiga vita na kuwanyanyasa Watanzania ambao wamekuwa wakiishi nchini humo na kujitafutia riziki, ni jambo la kushangaza. Isitoshe, kuna uhusiano mkubwa wa kindugu kati ya Frelimo—chama kinachotawala Msumbiji na Chama Cha Mapinduzi –CCM, kinachotawala Tanzania.

Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere na aliyekuwa kiongozi wa Frelimo na Rais wa Kwanza wa Msumbiji, Samora Moises Machel, waliamua kujenga Daraja la Umoja kwenye Mto Ruvuma, ili iwe ishara ya kudumu ya umoja wa Tanzania na Msumbiji na kurahisisha uhusiano wa kijamii na kibiashara baina ya wananchi wa nchi hizi mbili.

Sasa inaonekana wazi kwamba viongozi wa sasa wa nchi ambazo zilisaidiwa na Tanzania kujivua kongwa la utumwa wa kikoloni, wamesahau walikotoka—nani alikuwa nyuma yao wakati wa dhiki na mateso.

Viongozi hao, labda si Msumbiji pekee, wamesahau kabisa kwamba bila Tanzania, huenda hadi sasa wangekuwa chini ya ukoloni. Ni viongozi wachache ambao baada ya kujitawala walitambua na kukiri mchango wa Tanzania—Nelson Mandela alikuwa wa kwanza kufanya hivyo. Tanzania ni nchi ya kwanza aliyoitembelea Mandela mara baada ya kuachiwa huru mwaka 1990, baada ya kukaa miaka 27 kwenye Gereza la Robben Island, Afrika Kusini.

Rais mstaafu wa Namibia, ambaye pia alikuwa kiongozi wa SWAPO, Sam Nujoma, aliwaalika Watanzania wenye ujuzi kwenda kumsaidia kuijenga upya nchi yake. Inaaminika kwamba kuna Watanzania ambao wameamua kuishi Namibia.

Rais Robert Gabriel Mugabe wa Zimbabwe, kwa kutambua mchango wa Tanzania katika vita ya ukombozi dhidi ya utawala wa masetla wa Kizungu, inaelezwa kwamba alitoa msaada wa fedha kwa Tanzania ilipokuwa katika mkwamo wa kiuchumi, Rais Ali Hassan Mwinyi alipoingia madarakani. Itoshe tu kusema kwamba, Zimbabwe na Tanzania hazijawahi kutofautiana au kukwaruzana kisiasa na kidiplomasia. Kuna Watanzania wengi tu wanaoishi Zimbabwe na wanaofanya biashara baina ya nchi hizi.

Pamoja na mambo mengine, utawala wa sasa wa Rais Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda, unajua na unatambua mchango wa Tanzania wa kumng’oa Jenerali Idd Amin mwaka 1978. Museveni pia alitoa dola za Marekani 200,000 (Sh milioni 437) kwa ajili ya maafa ya tetemeko lililoukumba Mkoa wa Kagera.

Inawezekana hata uamuzi wa kupitisha bomba la mafuta Tanzania, badala ya Kenya, uliongozwa na dhana hiyo ya: Nikune mgongo nami nitakukuna.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles