Na Kulwa Mzee, Dar es Salaam
UPELELEZI wa kesi inayowakabili wahitimu sita wa mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) umekamilika .
Hayo yalielezwa jana na Wakili wa Serikali, Gines Tesha mbele ya Hakimu Mkazi, Frank Moshi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Washtakiwa katika kesi hiyo ni Mwenyekiti wa Umoja wa wahitimu hao, George Mgoba, Makamu Mwenyekiti, Parali Kiwango, Katibu Linus Steven na wahitimu wengine, Emmanuel Mwasyembe, Ridhiwani Ngowi na Jacob Mang’wita.
Tesha alidai kwamba kesi ilikuwa inatajwa na kwamba upelelezi umeshakamilika hivyo aliomba tarehe nyingine ya kuwasomea maelezo ya awali washtakiwa hao.
Hakimu alikubaliana na ombi hilo na kupanga Aprili 8 mwaka huu kwa ajili ya kuwasomea washtakiwa maelezo ya awali.
Katika hatua nyingine wakili wa washtakiwa hao, Joseph Manzi aliiomba mahakama itoe amri ya kupatiwa matibabu kwa mshitakiwa wa kwanza, Mgoba.
Manzi alidai kwamba mshtakiwa huyo tangu akamatwe hajapatiwa matibabu ya uhakika na hivyo kufanya afya yake kuwa mbaya na kusababisha ashindwe kutembea vizuri.
Alidai kama gerezani inashindikana kupatiwa matibabu basi ndugu wa mshtakiwa wagharamie kwa uangalizi wa Serikali aweze kupata nafuu.
Hakimu alisema mshtakiwa ana haki ya kupatiwa matibabu katika gereza husika na kama kuna sababu za msingi basi atibiwe hata katika hospitali za nje kwa uangalizi wa Serikali.
Washtakiwa hao kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kula njama, kufanya mkusanyiko usio halali na kushawishi wenzao kwenda Ikulu kushinikiza ajira.