27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

ONEKANA BAHILI LAKINI UNAJUA UNACHOFANYA

Na ATHUMANI MOHAMED

KUNA baadhi ya watu ni mabingwa wa kuiga vitu wanavyofanya wengine. Hata kama havina maana, lakini kwa sababu watu wengi wanafanya, basi wapo watu ambao kazi yao ni kufuatisha.

Wakati fulani unatakiwa kufikiri hata kidogo tu ili kung’amua kama jambo fulani ni sahihi kulifanya au kuliacha kwa ajili ya mafanikio ya maisha yako.

Mfano kuna tabia ya watu wanaoonekana kuwa makini na matumizi yao, kuitwa wabahili, wasiojua matumizi ya fedha nk.

Bahati mbaya ni kwamba baadhi ya watu huona aibu kuacha kufanya jambo fulani kwa sababu ya hofu kwamba fulani atamfikiriaje.

Kwa bahati mbaya sana, wakati ukiwaza namna gani jamaa fulani atakufikiriaje, watu wapo bize zaidi na maisha yao.

Wanaumiza vichwa wafanye nini ili waweze kujikwamua na umasikini. Wanajiuliza watumie mbinu gani ili wawe bora zaidi katika maisha yao nk.

Yapo maeneo mengi ambayo watu hukosea kwa kujikuta wakiwa watumwa wa kufanya vile watu wanavyopenda wafanye hata kama kuna athari kubwa za kiuchumi kupitia mtindo huo wa maisha.

Hapa chini nimekuandalia machache kati ya mazoea mabaya mengi ambayo yanaweza kukurudisha nyuma kimaisha kwa hofu tu ya kuogopa kuitwa mbahili.

 

MILO YA KIFAHARI

Kuna watu wanaweza kula vyakula vya kawaida majumbani mwao lakini wanapokuwa mbele za watu huamua kujitutumua!

Uwezo wake ni kula chakula cha 1500 kwa mama lishe, lakini kwa sababu marafiki zake ofisini wanakula hotelini mlo wa shilingi 4000 – 5000 na yeye ataiga ili aende nao sawa.

Hakuna maisha ya namna hiyo. Fanya kile kilichopo ndani ya uwezo wako. Unaweza kudharau shilingi 2000 yako leo, lakini ikawa na maana kubwa sana kwako kesho. Fedha inahitaji heshima ya hali ya juu. Kutumia fedha kama vile unazitengeneza siyo sahihi.

Utakuta mwingine ofisini kwao huwa wanawekewa chai ya bure, kwahiyo ni kiasi cha mtu kununua vitafunwa vyake kwa mama lishe labda vya 1000 tu ili apate kifungua kinywa, lakini atakwenda mgahawani kutumia 3000 kwa ajili ya asubuhi tu.

Siyo kosa kutumia kiwango hicho cha fedha, lakini linganisha na unachopata. Acha kuona haya na wakati maisha ni yako.

Kama uwezo wako ni kula wali maharage wa 1000, kula hicho. Ndiyo uwezo wako, acha kushindana na anayekula wali kuku kwa 5000 maana hujui mipango yake, hujui kipato chake.

Cha msingi angalia zaidi maisha yako binafsi badala ya kuishi kama anavyoishi fulani ambaye hawezi kukusaidia chochote. Zaidi utakapokwama, anaweza kuwa wa kwanza kukucheka. Kwanini uishi kwa kufuata mkumbo? Zinduka.

 

MAVAZI MAPYA

Kuna watu ni mabingwa wa kununua mavazi mapya. Akiwa na fedha mfukoni ambayo haina mpangilio akiona kitu kipya tu, tayari ananunua. Mwingine akiona fulani ofisini kwao amevaa nguo fulani mpya ni kosa. Ni kama mashindano.

Lazima na yeye akimbilie dukani kununua nguo au viatu kama vile. Hiyo siyo hekima hata kidogo. Fanya kile kilicho ndani ya uwezo wako. Acha kufanya manunuzi ya ghafla kwa sababu tu fulani naye amefanya hivyo.

Kumbuka hayo ni maisha yako, hufanyi kwa ajili ya kumfurahisha mtu fulani. Wataalamu wa mafanikio  wanasema, maisha ni yale uliyojichagulia mwenyewe.

Itaendelea wiki ijayo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles