27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

WANGEJIELEWA, WASANII WETU WASINGETUMIWA NA WAUZA UNGA

WIZIKID msanii kutoka Nigeria alizaliwa katika familia masikini na kukulia katika mitaa ya kimasikini sana. Katika harakati zake za kimaisha kakutana na mengi ya kuhuzunisha, kukatisha tamaa ila hakukata tamaa. Kwenye akili yake, mbali na kuzaliwa katika mazingira magumu aliamini atafanikiwa.

Muziki alioupenda toka utotoni, aliouhusudu kiasi cha kuwa kama chizi barabarani aliamini ndiyo ulikuwa msingi imara wa kutoka katika maisha ya ulofa na kuja kuishi maisha ya kifahari.

Baada ya mapambano ya miaka kadhaa, Wizkid leo siyo tu ni msanii maarufu Afrika na duniani ila pia ni miongoni mwa wasanii matajiri. Stori ya Wizkid haijapishana sana na Diamond Plutnumz.

Muziki na sanaa kwa ujumla ni utajiri. Iwe muziki, uchoraji ama uigizaji kama ukituliza akili vizuri na kuamua kupambana kiubunifu lazima maisha yako yashangaze wengi.

Mifano iko mingi. Wako akina Omotola, Ramsey Noah na wengine. Bila kujali ni aina gani ya sanaa unafanya, ila kama ukiamua kuwa mbunifu na kupambana bila kuchoka huna haja ya kuwa muuza dawa za kulevya.

Inashangaza mno kwa msanii kujihusisha na dawa za kulevya wakati ana uwezo wa kuwa milionea hata bila kupitia njia hii haramu. Wasanii wetu wengi wanakosa ubunifu kutoka na muda mwingi kushinda katika majumba ya starehe hivyo kutopata nafasi ya kukaa na kutafakari hatima ya sanaa yao.

Kwa kuufanya muda wote ubongo wao uwe bize na pombe, fikra za ngono, taratibu wanajikuta wakipoteza thamani yao katika sanaa wanayoifanya na kipato hushuka. Na ili kujinusuru na aibu ya kuonekana kama wamefulia, ndiyo hao wanakimbilia kujihusisha na dawa za kulevya.

Kama msanii una uwezo wa kufanya muziki wako kimataifa, ukaweza kuvutia kampuni nyingi kwa matangazo, ni kwa namna gani utakubali kufanya biashara itakayokupa msukomsuko na vyombo vya ulinzi na uslama?

Wasanii wetu wengi hawajui thamani ya sanaa yao. Sanaa inavyofanywa  vizuri na kwa ubunifu ni zaidi ya meneja ama mkurugenzi wa kampuni fulani. Sanaa inakupa pesa za kutosha heshima na umaarufu. Hivi vitu kwa pamoja ni ngumu kuvipata katika aina nyingine ya kazi.

Meneja wa kampuni fulani anaweza kuwa na pesa ila hawezi kufanana na msanii mkubwa au kama akifanana basi huenda atazidiwa heshima au umaarufu.

Shida kubwa ya wasanii wetu wengi ni kukaa club na kuiga starehe badala ya kuiga vitu vya maana. Msanii wa Tanzania anaweza kuiga kuvaa kama Rihanna ila asiige uchapakazi wake.

Huu ni uzembe. Msanii wa kiume wa Kitanzania, ataiga hereni, kuvaa suruali chini ya kiuno na mwonekano wa  Chris Brown ila hatathubutu kuandika ngoma kali na kukusanya utajiri kama Chris Brown.

Natamani kila msanii katika eneo lake angejua kama sanaa ni utajiri. Na siku ikitokea wakajua hivyo, nina hakika hatutaona tena majina ya wasanii wetu pendwa yakihusishwa na biashara hii haramu ya dawa za kulevya.

Huwa najiuliza kwa kipaji kama cha Wema akitulia na kuamua kutumia nguvu zake zote katika kuigiza atafika wapi?

Najiuliza Agness Gerald ‘Masogange’ akiamua kutulia  na kujibidisha maisha yake yatakuaje? Tatizo ni kwamba, Watanzania tuna utamaduni wa kupenda kufanikiwa bila kuumia. Tunapenda kutesa bila kwanza kuteseka. Dunia ya hivyo hakuna.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles