Elias Msuya na Elizabeth Hombo
WAZIRI Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya, amekumbusha machungu ya kauli yake ya zamani ya “kila Mtanzania ataubeba msalaba wake”, huku akiwataka Watanzania kuacha kuwa walalamikaji kwa kila jambo.
Msuya aliyewahi kuwa waziri mkuu mara mbili (Novemba 7, 1980 hadi Februari 1983 na Desemba 7, 1994 hadi Novemba 28, 1995), alitoa kauli hiyo bungeni akiwa waziri wa fedha mwaka 1989.
Akizungumza jana katika uzinduzi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere lililoandaliwa na Kituo cha Rasilimali cha Mwalimu Nyerere, Msuya alisema kauli ile ililenga kukataza matumizi mabaya ya rasilimali.
“Ni kweli nilitoa hiyo kauli na wala si-‘apologize’ (siombi radhi), kwa sababu kila mtu ana tafsiri yake. Wakati ule nilikuwa waziri wa fedha, tulipeleka bajeti ya Serikali bungeni. Bajeti ile ililenga kutoza kodi kwenye bidhaa kama khanga na vitenge, ukaibuka mjadala mzito kutoka kwa wabunge ambao sitawataja,” alisema Msuya na kuongeza:
“Walilalamika kuwa wameoa wake watatu watatu, watamudu vipi gharama za kununua khanga. Nikasema kila mtu ataubeba msalaba wake mwenyewe. Mungu amesema tuoe mke mmoja, wewe umeoa watatu, utabeba msalaba wako… kuoa ni uamuzi wako, inabidi uchangie. Lengo ni kubana matumizi.”
Uzinduzi wa kavazi hilo ulifanywa na Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa na kuhudhuriwa na wasomi mbalimbali, akiwamo Mkurugenzi wa Tume ya Sayansi (Costech), Dk. Hassan Mshinda.
Msuya aliendelea kusema kuwa Watanzania wamekuwa na tabia ya kulalamika kuliko kufanya kazi.
“Ukisoma magazeti yetu na vyombo vya habari, utaona Watanzania wana ‘culture’ (utamaduni) ya kulalamika tu. Kwanini tusitumie muda huo kufanya kazi,” alihoji.
Awali mmoja wa wachangiaji katika mjadala huo, Profesa Mwesiga Baregu, alimuuliza Msuya kuhusu kauli hiyo akisema imesababisha watu kujiingiza kwenye ufisadi.
“Kuna kauli ziliwahi kutolewa na viongozi, ikiwamo ile ya Pesambili (Basil Mramba, aliyekuwa waziri wa fedha) aliyesema ndege ya rais itanunuliwa hata Watanzania wale nyasi. Nyingine ni kauli yako ya kila mtu atauchukua mzigo au msalaba wake mwenyewe, huoni kwamba imesababisha watu kukosa maadili?” alihoji Profesa Baregu.
Kuhusu vijana, Msuya alisema tofauti na enzi zao, vijana wa siku hizi hawana uvumilivu.
“Vijana wa siku hizi wana mtazamo tofauti. Zamani sisi tulikuwa tunafanya kazi kwa mshahara mdogo. Leo vijana wamekuwa wengi waliomaliza chuo kikuu, ukiwaambia hivyo hawakuelewi,” alisema Msuya.
Hata hivyo, kauli hiyo ilipingwa na mchangiaji aliyejitambulisha kwa jina la Lusekelo Mwakimage, akisema vijana wa sasa ni wavumilivu ndiyo maana hawawafanyii vurugu viongozi waliojilimbikizia mali.
Lakini Msuya huku akitoa mfano wa kazi ya ujenzi wa reli ya Tazara, aliendelea kusisitiza kuwa vijana wa sasa si wavumilivu kiasi cha kukosa nguvu kazi.
“Asilimia 65 ya Watanzania ni vijana na hawawezi kuishi maisha tuliyoishi sisi, wanataka matokeo ya hapo hapo…uwezo wetu wa kuhamasisha watu ni mdogo,” alisema Msuya.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utafiti ya Kuondoa Umaskini (REPOA), Profesa Samuel Wangwe, alisema kwa sasa taifa lina ombwe la viongozi.
“Aina ya uongozi aliokuwa akizungumzia Mwalimu Nyerere haipo na sasa tuna ombwe la uongozi. Wakati tunatupa misingi ya ujamaa, wenzetu China, Vietmam waliangalia baadhi ya mambo, lakini sisi tulitupa kila kitu. Sasa hapa ni misingi gani na si kwamba hatuna ujamaa,” alisema Profesa Wangwe.
Alisema kitendo cha taifa kutegemea misaada kutoka nje kinaondoa ubunifu wa kujitegemea.
“Unaweza ukapata misaada ili kujenga uwezo wa kujitegemea, sasa unapokubali msaada ambao si msaada unaondoa ubunifu,” alisema Profesa Wangwe.
DIRA YA TAIFA
Msuya alipinga madai ya kupotea kwa dira ya taifa kutokana na kushuka kwa maadili. Alisema bado Watanzania wanaguswa na misingi ya Azimio la Arusha.
“Jamii ya leo bado iko kwenye Azimio la Arusha na misingi yake bado inatutafuna, huo ndiyo ukweli. Sikubaliani kirahisi kwamba maadili yameshuka, mimi nimestaafu naishi huko kijijini, wananchi wakisikia ufisadi wanapiga kelele. Dira ya utaifa bado ipo, tatizo ni utekelezaji tu,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema tatizo kubwa lililopo kwa sasa ni kutokuwapo kwa utekelezaji wa dira ya taifa.
Alisema masuala yote yanayoendelea hapa nchini ikiwamo viongozi wa Serikali kuhusishwa na ufisadi, msingi wake ni kutokuwapo utekelezaji wa dira.
“Pamoja na kwamba tuna misingi muhimu ya dira yetu, dira iliyokuwa inafahamika ilikuwa ni ya ujamaa na masuala yote yanayoendelea hapa nchini ikiwamo viongozi wa Serikali kuhusishwa na ufisadi, msingi wake ni kutokuwapo utekelezaji wa dira na ndiyo maana mambo ya rushwa yanaendelea.
“Kwa sasa dola yenyewe inajimaliza. Mfano hii kashfa ya Tegeta Escrow Account ni hao hao viongozi wa Serikali ambao wamehusika, kwa maana nyingine ni kwamba Serikali yenyewe inajiibia. Hivyo ni lazima mwafaka wa kitaifa uwepo,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema mara nyingi viongozi wamekuwa wakisema mambo mbalimbali kwa maneno, lakini wamekuwa hawayafuati kwa vitendo.
Awali akizungumzia lengo la kavazi hilo, Mkurugenzi wa Kavazi la Mwalimu Nyerere, Profesa Issa Shivji, alisema ni kukusanya na kuhifadhi nyaraka na taarifa za utafiti kuhusu Mwalimu Julius Nyerere.
“Tatizo kubwa lililopo kwa sasa ni kutokuwapo miiko ya uongozi. Ni lazima tuwe na usawa na haki za binadamu na lazima tuwe na uchumi unaokua, ambao unawanufaisha wananchi wote na si kutaja tu kwa maneno kama ambavyo viongozi wengi wamekuwa wakifanya,” alisema Profesa Shivji.