NA VIVIAN SHANGO
JESHI la Polisi mkoani Tabora limewakamata watu wanne wakiwa na bunduki ya SMG ikiwa na risasi mbili, baada ya kuvamia Kijiji cha Tura wilayani Uyui.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tabora, Suzan Kaganda, alisema watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kupigwa na wananchi ambao walimuua mtuhumiwa mmoja.
“Watu hawa wakiwa watano walivamia kijijini hapo, wakavunja na kupora Sh milioni 2.3.
“Lakini wakati wanataka kukimbia wakiwa na pikipiki walizungukwa na wananchi waliowashambulia na mmoja alipoteza maisha,” alisema Kamanda.
Kaganda alisema pia kuwa polisi waliwakamata Malimatamu Ndawayake (38), Shija Mihayo(40) na Mwinyimzee Kiloge (36) wakazi wa Wilaya ya Nzega, kwa kupatikana na magunia mawili na nusu ya bangi.
Katika operesheni hiyo watuhumiwa wengine sita walikamatwa wakiwa na lita 160 za gongo.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Achimwene Peter (45), Hamisi Songambele (45), Sofia Stepheno (42)Thadeo Paulo (37), Devotha Paulo (26) na Aziza Juma (35).