NA DK. CHRIS MAUKI,
NINAANDIKA makala haya baada ya kukutana na wazazi wengi wakilalamika juu ya watoto wao, wengine wakiwaleta ofisini kwangu kupata msaada wa kisaikolojia na wengine wakisema wameshauriwa watafute msaada wa kisaikolojia na walimu wa watoto hao mashuleni baada ya kuona wana ugumu sana kwenye usikivu, utulivu “concentration” na hata kwenye uwezo wa kujifunza “low learning ability”.
Utakubaliana na mimi kwamba ukiwasikia walimu wengi leo, hulalamika kwamba watoto wao siku hizi wamekuwa wagumu kuelewa, wagumu kufundishika na wana tabia mbaya.
Wazazi nao kwa upande mwingine wamezidi sana kulalamika kwamba malezi ya siku hizi ni tofauti na zamani. Imekuwa ngumu kulea mtoto mdogo siku hizi na kila mzazi anapata changamoto kubwa.
Najua wengi tuna maswali, tatizo liko wapi? Nini kinasababisha hali hii? Yamkini ulikuwa hujui au hufahamu kwamba chanzo kinaweza kuwa ni wewe mzazi, leo ninakuja na jibu kwako mzazi. Suluhisho liko mkononi mwako, jawabu linaanza na wewe mzazi.
Ni jambo la ukweli kabisa na limehakikiwa kitafiti kwamba leo watoto wanakwenda shule wakiwa wamechoka akili zao, watoto wanasinzia darasani na wengine wanalala kabisa, watoto wanakinai shule badala ya kuhamasika na shule.
Wako watoto ambao inamchukua mzazi au mlezi saa kadhaa kumshawishi mtoto avae nguo za shule tofauti na awali ambapo mtoto anadamka hata kabla ya muda wa shule anatamani kwenda shule.
Watoto hawana hisia na shule, hawana hisia na mambo ya kijamii yanayoendela shuleni “they are emotionally disconnected”. Ni vema kufahamu kwamba ubongo ni kitu kilaini sana kinachoweza kubadilishwa na mazingira, mazingira tuishiyo yanaweza kuufanya ubongo uwe imara au uwe dhaifu sana. Ubongo huu pia unahitaji kufunzwa, na kwa jinsi ubongo unavyofunzwa ndivyo unavyokuwa na kuendesha tabia ya mtu. Watoto wetu kwa kiasi kikubwa wapo vile walivyo na wanafanya yale wanayoyafanya kwa kadiri tulivyotengeneza ubongo wao.
Bahati mbaya, kwa kiasi kikubwa wazazi wengi tumetengeneza ubongo wa watoto wetu vibaya, na hicho ndicho chanzo cha matatizo yote. Utaniuliza kivipi? Jibu hili hapa!!!
1. Matumizi makubwa ya teknolojia
Siku hizi kuna kila aina ya mashine au vitu vilivyotengenezwa kwa teknolojia ya kisasa katika kumfanya mtoto atulie, asisumbue au asilie. Zamani kulikuwa na sehemu za kumweka mtoto mchanga akae peke yake, siku hizi sehemu ile imefungwa vikorokoro vingi kumfanya mtoto aweke mawazo yote kwenye hivyo vitu wakati mzazi akiwa anafanya mambo mengine.
Watoto wanataka kuwa kwenye simu muda wote wakicheza michezo ya kompyuta “video games”. Teknololojia za michezo ya kompyuta iko katika uwezo wa juu sana katika hali ambayo mtoto huyu mwenye umri mdogo anapofika darasani ambapo mwalimu anatakiwa kumfundisha kwa kuzungumza akiwa mbele ya darasa na akitumia michoro iliyochorwa na mikono kwa ajili ya kiwango cha uelewa cha mtoto huyu, mtoto anapoteza hamasa.
Pia mara nyingi yale wanayoyaona na kujifunza kwenye michezo ya kompyuta hayahusiani sana na yale wanayojifunza darasani. Michezo hii inawafanya wengi wachoke akili au wachelewe kulala na hivyo kufika darasani wamechoka sana akili na wakiwa wagumu sana kujifunza.
Teknolojia kwa kiasi kikubwa imewatenganisha kihisia watoto na wazazi wao, watoto wakiwa kwenye gari na wazazi, kila mmoja ana simu au mashine ya kuchezea, hakuna anayemwongelesha mwenzake au kuongelea vitu vinavyowahusu wao.
Uwepo wa mzazi kihisia kwenye maisha ya mtoto ni kirutubisho cha muhimu sana kwenye makuzi ya ubongo wa mtoto, kwa bahati mbaya sana watoto wetu wananyimwa kirutubisho hiki cha muhimu kwasababu tu ya kitu kiitwacho teknolojia.
Hii inaweza kuonekana kama inawagusa watoto wachache wa familia zinazojiweza lakini ukweli ni kwamba jamii hii inaongezeka kwa kasi siku hizi maana kila mzazi anafikiri kumnunulia mwanae michezo hii ndio ukisasa na hapo tatizo linakuwa kubwa zaidi.
Itaendelea wiki ijayo