25.5 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

USIJINYIME FURAHA KWA KUJILINGANISHA NA WENGINE

Na Christian Bwaya,

TUNAISHI katika zama ambazo kujilinganisha na wengine kumekuwa kawaida ya maisha. Tunafanya karibu kila kitu kwa kuiga. Thamani ya kile tulichonacho inategemea kile walichonacho wanaotuzunguka.

Kwa mfano, unaweza kuwa na kitu kizuri kinachokidhi mahitaji yako. Lakini uzuri wa hicho ulichonacho unaweza kupotea pale unapohisi jirani yako anacho kilichobora zaidi. Hata hivyo, unaweza kushangaa inakuwaje kitu hicho hicho kikaonekana kuwa cha thamani pale unapojua kuwa wanaokuzunguka hawana. Tunashindwa kutambua thamani bila kwanza kuilinganisha na thamani inayotuzunguka.

Kwa sababu hiyo, tunatumia muda wetu mwingi kujilinganisha na watu. Mitandao ya kijamii nayo kwa kiasi kikubwa inarahisisha shughuli hii. Kwa kule kutazama ufahari bandia unaotangazwa na watu mitandaoni, tunajihukumu kuwa bado hatujafanikiwa. Tunakosa amani kwa kutathmini thamani yetu kwa vigezo vya yale tunayoyaona kwa wengine. Tunasahau kuwa hata hao wanaojinasibu kwa ufahari huo wanao upungufu wao ambao hawauaniki hadharani.

Katika makala haya, tunasaili tabia tatu muhimu unazohitaji ili kujenga furaha isiyoathiriwa na maisha ya watu wanaokuzunguka.

Furahia hatua uliyonayo

Kutokufurahia ulichonacho tayari kunaweza kuwa sababu kubwa ya kukosa furaha. Unapokuwa mtu wa kutamani kile usichokuwa nacho huwezi kufika mahali ukajisikia utoshelevu. Kila hatua utakayopiga mbele, itaendelea kuzamisha kwenye shauku ya kupata zaidi. Shauku hii haitakuhakikishia furaha kwa sababu hutafika mahali ukakubali kuwa unavyo vya kukutosha.

Ikiwa unatamani kuwa mtu mwenye furaha, unahitaji kujenga utaratibu mpya wa maisha. Furahia na kuona thamani ya kile ulichonacho tayari bila kungoja upate unachokitarajia. Ona thamani ya kile kilichopo tayari kwa sababu ndicho ulicho na uhakika nacho. Usipoweza kufurahia kile ulichonacho tayari, hutaweza kufika mahali ukafurahia kikubwa utakachokuwa nacho.

Hata kama unafanya kazi unayoiona kuwa ndogo, ifurahie. Ifanye kwa bidii na kwa moyo. Hiyo haimaanishi usiwe na ndoto za kufanya kazi nzuri zaidi. Kuwa na ndoto kubwa isiwe sababu ya kukosa furaha ya kile ulichonacho tayari.

Usitishiwe na mafanikio ya wengine

Kwa kawaida, mwanadamu ana tabia ya kushindana na wengine. Anatamani kuwa bora ikiwezekana kuliko wengine wote. Hulka hii hutufanya tuwe watu wa kupenda kujilinganisha na wengine. Bahati mbaya, kujilinganisha hakuwezi kutupa furaha.

Unapojilinganisha na wa chini yako, unazalisha kiburi cha kujiona bora. Kiburi kitakukosanisha na watu kama tutakavyoona hivi punde. Kwa upande mwingine, unapojilinganisha na wanaokuzidi, unajenga hisia za wivu. Wivu, kadhalika, hauwezi kukupa furaha.

Ni vizuri kutambua kuwa kila mmoja wetu ana mazingira yake ya pekee. Hatufanani. Ni vigumu kujua mazingira yanayompendelea mwenzako na hivyo huna sababu ya kutishika kuzidiwa.

Wainue unaowazidi

Kinyume na kutishwa na mafanikio ya wengine, wakati mwingine tunajisikia kiburi tunapoona tunawazidi wengine. Kwa fikra, maneno na vitendo, tunafurahia kuwa zaidi yao. Hali hii inaweza kujenga hisia za uadui na wivu kwao na kuathiri namna tunavyohusiana nao.

Badala ya kujisikia kuridhika kwa kuwazidi watu wengine, unahitaji kujenga tabia mpya ya kuwainua wale unaowazidi. Badala ya kutumia muda mwingi kuwathibitishia namna unavyowazidi, wasaidie kuinuka. Sema maneno yanayowajenga kihisia badala ya kuwaumiza. Tenda yanayolenga kuwainua badala ya kushindana nao. Kwa kufanya hivyo, utakuwa ukijenga daraja la watu kukuongezea sababu ya kuwa mtu mwenye furaha.

Mwandishi ni mhadhiri wa Saikolojia Chuo Kikuu cha Kikatoliki Mwenge, Moshi. Blogu: http://bwaya.blogspot.com, 0754870815

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles