Na Sarah Mossi, Dar es Salaam
BALOZI wa Libya nchini,
, amejiua kwa kujipiga risasi ofisini kwake.
Sababu za kujiua kwa balozi huyo hadi sasa bado hazijafahamika.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ili kutekeleza azma yake ya kujiua, Balozi Nwairat alijifungia ofisini kwake na kujifyatulia risasi kifuani upande wa kushoto.
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Msemaji wa Wizara hiyo, Mkumbwa Ally, ikieleza kuwa maofisa wa ubalozi walisikia mlio wa bunduki na kuamua kufuatilia na walipokwenda kwenye ofisi ya Balozi Nwairat walikuta mlango umefungwa na kulazimika kuuvunja na kumkuta balozi huyo akiwa ameanguka chini.
Balozi huyo ambaye alikuwa akikaimu nafasi hiyo kwa miezi kadhaa, hadi sasa haijajulikana sababu ya kujiua kwake.
“Walimkimbiza Hospitali ya AMI Oysterbay ambako alitangazwa kuwa amekwisha kufariki na polisi wakathibitisha kifo hicho. Maiti imehamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili,” ilisema taarifa hiyo fupi ya Wizara.
Kwa mujibu wa Ally, taratibu za kuusafirisha mwili wa Kaimu Balozi huyo zinafanywa kati ya Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Ubalozi wa Libya.
MTANZANIA lilipomtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, alisema kwa sasa jeshi hilo linakusanya taarifa za ndani na baada ya muda watatoa taarifa yao.
“Kwa tukio hili tunawasiliana na wenzetu wa Wizara ya Mambo ya Nje ili tujue kwa undani na kisha kwa utaratibu wa kawaida ndipo Polisi tutatoa taarifa. Suala la kifo nami nimesikia ndiyo maana tunawasiliana na wenzetu kutokana na uzito wa tukio hili,” alisema Kamishna Kova.