25.8 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KWA HILI SIMBA WANASTAHILI PONGEZI

Na ADAM MKWEPU-DAR ES SALAAM

WAUNGWANA siku zote hupongezana, pindi jambo jema linapofanyika licha ya wakati mwingine kutofautiana kimawazo na kimtazamo lengo likiwa kujenga nyumba moja.

Kutofautiana ni afya ya maendeleo kwa kuwa jambo jema huja baada ya kuchuja mawazo tofauti bila kujali itikadi au mambo mengine yanayowatofautisha katika jambo husika.

Lakini leo nisingependa kutofautiana na maamuzi yaliyochukuliwa na uongozi wa klabu ya soka ya Simba.

Wiki iliyopita Simba ilifikia mwafaka na makubaliano na Baraza la wadhamini wa klabu hiyo, lengo likiwa ni kuboresha mchakato wa mabadiliko, baada ya kutofautiana kwa muda mrefu.

Kwa muda mrefu baraza hilo lilikuwa likipinga utaratibu uliokuwa ukitumika katika mchakato wa mabadiliko ya klabu hiyo ya kutoka matumizi ya mfumo wa kadi, hadi hisa kwa wanachama likidai kuwa ulikiuka katiba ya klabu hiyo.

Katika makubaliano hayo, baraza hilo limewataka viongozi wa klabu hiyo kuwapelekea mapendekezo yaliyomo ndani ya mchakato wa mabadiliko hayo, ili kuyafanyia maboresho zaidi kwa kubaini faida na hasara zitakazopatikana.

Simba ipo katika mchakato wa maboresho ya katiba yao ili kumpa nafasi mfanyabiashara na mwanachama na mpenzi mkubwa wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, kuwa na uhuru wa kununua hisa za asilimia 51 na wanachama kubaki na asilimia 49 hatua iliyopingwa na Baraza hilo kuwa halikushirikishwa.

Naunga mkono juhudi zilizofanywa hadi mwafaka wa viongozi na baraza hilo ukapatikana, hivyo kilichobaki ni kumaliza palipobakia.

Uamuzi huo ni hatua kubwa kwa klabu hiyo ambayo kwa sasa ipo katika mbio za ubingwa ikiwa na tofauti ya pointi chache na vinara wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga.

Umoja na mshikamano ni miongoni mwa mambo ambayo yanaweza kuisaidia timu hiyo kuwa imara na kuendelea kufanya vizuri zaidi, kama ambavyo tumeshuhudia mwanzoni mwa msimu.

Muda mrefu umepita tangu Simba kutwaa taji la Ligi Kuu, hivyo kuunganisha nguvu ni jambo la busara kwa masilahi ya klabu hiyo.

Kwani uongozi na baraza hilo kama wangeendelea kutofautiana kungeathiri vitu vingi, likiwamo suala la kutwaa ubingwa msimu huu.

Hivyo uamuzi wa kuunganisha nguvu pamoja kwa sasa kutawaongezea kasi kuelekea katika ubingwa msimu huu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles