27.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, February 7, 2023

Contact us: [email protected]

YALIYOJIRI MICHUANO YA AFCON 2017

BADI MCHOMOLO NA MITANDAO

MICHUANO ya 31 ya Kombe la Mataifa ya Afrika (Afcon) kwa mwaka 2017, imefikia tamati jana nchini Gabon baada ya mataifa 16 kuoneshana uwezo kisoka.

Kati ya timu 16, mbili tu ambazo ni  Misri na Cameroon ndizo zilizoweza kufika hatua ya fainali, lakini hadi gazeti hili linakwenda mitamboni fainali hiyo ilikuwa bado haijapigwa.

Hata hivyo, SPORTIKIKI tumekuwa tukifuatilia michuano hiyo kwa karibu sana tangu siku ya kwanza hadi inafikia mwisho, kutokana na hali hiyo leo hii tumeyafanyia uchambuzi baadhi ya mambo yaliyojitokeza kwenye mikiki mikiki hiyo.

Ufunguzi

Maandalizi ya michuano hii kwa mwaka huu yalionekana kuwa na msisimko wa aina yake pale nchini Gabon, ambapo siku chache kabla ya michuano hiyo kuanza mashabiki walionekana wakitumia vitu vingi vyenye rangi ya njano.

Jezi mitaani zilitawala zile za njano ambazo zilikuwa zinawakilisha Taifa hilo kama wenyeji wa michuano hiyo.

Lakini siku zote hakuna kitu kizuri kitafanyika bila ya baadhi ya watu kupinga, hali hiyo imetokea kwa wananchi wa nchini Gabon ambao walionekana kupinga michuano hiyo siku ya ufunguzi.

Baadhi ya wananchi hao walionekana na mabango wakiilalamikia Serikali kwamba imetumia fedha nyingi kuandaa michuano hiyo wakati huo wananchi wao wengi ni masikini na kuna baadhi ya huduma bora za kijamii wanazikosa kama vile hospitali, shule, maji na mambo mengine.

Lakini hoja za wachache hao hazikuweza kusitisha michuano hiyo kuendelea, mambo yalikwenda kama yalivyopangwa.

Sherehe za ufunguzi zilianza mapema kabla ya saa 1:00 jioni ambapo mtanange wenyewe wa soka ulianza kutimua vumbi, kulikuwa na burudani ya muziki, sarakasi, ngoma na mambo mengi.

Kwa upande wa muziki, kulikuwa na wasanii wakali kutoka barani Afrika kama vile Nasibu Abdul ‘Diamond’ kutoka nchini Tanzania, Akon kutoka nchini Marekani, lakini ni raia wa nchini Senegal, Davido kutoka nchini Nigeria.

Wasanii hao walikuwa kivutio kikubwa kwenye ufunguzi huku wakipokelewa na rais wa nchi hiyo, Ali Bongo Ondimba.

Msisimko

Siku ya kwanza ya michuano hiyo kulionekana kuwa na msisimko wa hali ya juu kwa kuwa wenyeji Gabon walishuka dimbani hivyo mashabiki walijitokeza kwa wingi, lakini siku zilivyokuwa zinazidi kusonga mbele hali ilionekana kubadilika.

Wenyeji Gabon walitakiwa kuonekana kuwa wengi kwa kuwa wapo nyumbani, lakini kutokana na matokeo ya sare za michezo yao miwili ya awali katika hatua ya makundi ziliwakatisha tamaa.

Idadi ya watu uwanjani ilipungua siku hadi siku, hali ilikuwa mbaya zaidi baada ya wenyeji hao kutolewa mapema katika hatua ya makundi, hivyo viwanja vilizidi kupungua idadi ya mashabiki na msisimko kupotea kabisa.

Ubovu wa viwanja

Inadaiwa kwamba kuna baadhi ya wachezaji walishindwa kuonesha uwezo wao kutokana na kuchangia kwa ubovu wa viwanja.

Kumekuwa na malalamiko makubwa kwamba kuna viwanja havikuwa na viwango vizuri kwa ajili ya kucheza michuano hiyo kama vile kiwanja cha Stade de Port-Gentil.

Huu ni uwanja ambao ulifunguliwa mwaka 2015 na nyota wa klabu ya Barcelona na timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, uliwekwa jiwe la msingi na nyota huyo kwa ajili ya michuano hiyo ya Afcon huku ukichukua idadi ya watazamaji 20,000.

Stade de Port-Gentil ni uwanja ambao umetupiwa lawama kwa kiasi kikubwa na makocha pamoja na wachezaji mbalimbali huku wakidai kuwa umechangia baadhi ya wachezaji kupata majeraha tofauti na viwanja vingine.

Beki wa timu ya Taifa ya Morocco, Mehdi Benatia, alikuwa miongoni mwa wachezaji ambao walikuwa wanaulalamikia uwanja huo, malalamiko hayo aliyasema mara baada ya kutolewa katika michuano hiyo dhidi ya Misri hatua ya robo fainali.

Kocha wa timu ya Taifa ya Ghana, Avram Grant, aliweka wazi kuwa kiwanja hicho kilichangia mshambuliaji wake hatari, Asamoah Gyan ambaye ni nahodha kuumia akiwa peke yake na mpira, hata hivyo mchezaji wake mwingine beki Baba Rahman, ambaye aliumia hatua ya makundi na kushindwa kuendelea hadi mwisho wa michuano hiyo na baadhi ya wachezaji wengine watatu kuumia.

Kocha wa timu ya Taifa ya Misri, Hector Cuper, naye alilalamika juu ya uwanja huo na kudai wachezaji wake wameshindwa kuonesha kiwango kizuri kutokana na ubovu wa uwanja huo kila walipoutumia.

Caf wakanusha ubovu wa viwanja

Baada ya wachezaji na makocha kulalamika kuwa kuna baadhi ya viwanja vimekuwa vibovu na vimechangia wachezaji wao kuumia na kushindwa kuonesha uwezo wao, Shirikisho la Soka Afrika ‘CAF’ walikanusha habari hizo.

Msemaji wa Shirikisho hilo, Junior Binyam, alidai kuwa hakuna usahihi wa habari za ubovu wa viwanja hadi pale wanasayansi watakapoweka wazi kama kweli kuna viwanja vilichangia wachezaji kuumia.

“Hakuna ukweli huo wa ubovu wa wachezaji, tunaamini vilikuwa sawa kama vilivyo vingine labda wanasayansi wathibitishe.

“Hata katika viwanja bora vya Ligi Kuu nchini England, kuna wachezaji wengi wanatoka huko wakiwa wameumia sasa tunashangaa kuona vikitajwa viwanja vya Afcon,” alisema Binyam.

Kadi nyekundu/njano

Tangu kuanza kwa michuano hiyo Januari 14, kwa upande wa kadi nyekundu kabla ya mchezo wa jana timu nyingi zilionekana kuwa na nidhamu ya hali ya juu, ambapo timu ya DR Congo pekee ambayo mchezaji wao, Joyce Mutambala, alioneshwa kadi nyekundu.

Lakini mbali na kadi nyekundu kwa mchezaji huyo, kadi nyingi zilikuwa za njano msimu huu, timu ya Burkina Faso imeongoza kwa kuwa na kadi nyingi za njano hadi inamaliza michuano hiyo jumla ya kadi 10 zilitolewa kwa upande wao, wakati huo wakifuatiwa na Cameroon kadi 10, huku Algeria, Senegal na Misri wakiwa na kadi saba kila timu.

Katika michuano hiyo timu ambayo imeweka historia ya kuwa na makosa mengi ni pamoja na Cameroon kabla ya mchezo wa jana ambapo ilifanya makosa mara 124, ikifuatiwa na Morocco yenye makosa 103, wakati huo DR Congo ikifanya makosa mara 97.

Uchache wa mabao

Baadhi ya washambuliaji wameshindwa kuonesha makeke yao ya kupachika mabao kama ilivyo kwenye klabu zao, nyota wa timu ya Taifa ya Gabon, Pierre Aubameyang, ambaye anaongoza kwa kufunga mabao mengi katika Ligi Kuu ya Ujerumani katika klabu yake ya Borussia Dortmund, katika michuano hiyo ya Afcon alionekana kuwa kawaida na vile ambavyo wengi walitarajia, hadi timu yake inatolewa katika makundi alikuwa na jumla ya mabao mawili.

Mshambuliaji wa timu ya Taifa ya DR Congo, Junior Kabananga, amekuwa kinara wa mabao katika michuano hiyo baada ya kufunga matatu, huku nyota wengine kama vile, Andre Ayew akiwa na mabao mawili, Aristide Bance, mabao mawili na Islam Sliman akiwa na mabao mawili.

Lakini hii ni hali ya kawaida kwa miaka ya hivi karibuni ambapo mabao yamekuwa chini ya tano kwa mchezaji, msimu uliopita wa 2015 wachezaji watano walikuwa vinara wa mabao ambapo wote walikuwa sawa huku wakiwa na mabao matatu sawa na 2012, lakini 2010 nyota wa timu ya taifa ya Misri, Mohamed Nagui ‘Geddo’,  alikuwa kinara wa mabao ambapo alifunga jumla ya mabao matano.

Wenyeji kuyaaga mashindano mapema

Wenyeji Gabon hawakupewa nafasi kubwa kutokana na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja ndani ya kikosi hicho, ila baadhi ya watu waliwapa nafasi kutokana na kuwa wenyeji wa mashindano. Hali ilikuwa tofauti kwani timu hiyo ilikuwa ya pili kuyaaga mashindano hayo huku wa kwanza wakiwa Uganda.

Lakini nahodha wa timu hiyo, Aubameyang, aliweka wazi sababu ya timu yao kuondolewa mapema, alidai kuwa chama cha soka nchini humo kilishindwa kufanya maandalizi ya kutosha kuelekea michuano hiyo.

Aubameyang alisema, kosa kubwa ambalo walilifanya chama cha soka nchini humo ni kumfukuza kocha wao, Jorge Costa, ambaye walimzoea kwa muda mrefu na nafasi yake ikachukuliwa na Jose Antonio.

Inasemekana kuwa kocha huyo alifukuzwa kazi ikiwa ni siku 70 kuelekea michuano hiyo, hivyo kocha mpya alishindwa kuwatumia wachezaji hao, hivyo chama cha soka kilishindwa kufanya maandalizi mapema.

Walipewa nafasi

Kuna baadhi za timu ambazo zilipewa nafasi lakini zilishindwa kuonesha ubora wao kutokana na ushindani uliojitokeza kwa timu zote 16.

Mabingwa watetezi, Ivory Coast ambao walisheheni idadi kubwa ya wachezaji wanaocheza soka la kulipwa barani Ulaya, walishindwa kutetea ubingwa wao na kulikuwa na nyota kama vile, Wilfried Zaha ambaye anakipiga katika klabu ya Crystal Palace, Wilfried Bony wa Stoke City, Eric Billy wa Man United, Serge Aurier wa PSG, Salomon Kalou na wengine wengi.

Senegal nayo ni miongoni mwa timu iliyopewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri katika michuano hiyo lakini ilishindwa kuwatumia wachezaji wao hatari kama vile Sadio Mane ambaye anakipiga katika klabu ya Liverpool.

Mchezaji huyo alipewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri lakini alishindwa kuibeba timu yake na alionekana kikwazo kwa timu yake kusonga mbele baada ya kukosa penalti yake ya mwisho kuelekea hatua ya nusu fainali.

Ghana ambayo msimu uliopita ilifika fainali dhidi ya Ivory Coast walipewa nafasi ya kufika fainali na ikiwezekana kutwaa ubingwa kutokana na maandalizi ambayo waliyafanya, lakini walijikuta wakichezea kichapo cha mabao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Cameroon, hivyo safari yao iliishia nusu fainali.

Burkina Faso vibonde kwa Misri

Burkina Faso waliweza kupambana hadi kufika hatua ya nusu fainali, lakini walishindwa kufika fainali baada ya kuchezea kichapo cha mabao 4-3 ya mikwaju ya penalti huku wakitoka sare ya 1-1 ndani ya dakika 120.

Misri wamekuwa wakijipigia Burkina Faso mara kwa mara katika michuano hii na sasa ni mara ya nne wanakutaka katika hatua ya nusu fainali na mara zote Misri wamekuwa wababe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,885FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles