25.6 C
Dar es Salaam
Sunday, January 5, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

OBAMA ACHOCHEA MATOKEO MSHINDI WA PILI KITAIFA

Na NORA DAMIAN,

MWANAFUNZI Cynthia Mchechu, ambaye ameshika nafasi ya pili kitaifa kwenye matokeo ya mtihani wa kidato cha nne uliofanyika Novemba mwaka jana, amesema Rais Mstaafu wa Marekani, Barack Obama, amechangia mafanikio yake.

Cynthia aliyekuwa akisoma Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Francis Mbeya, alisema ndoto yake ya baadaye ni kuja kuwa mwanasheria.

“Wakati Rais Obama anaapishwa mwaka 2009 (yeye alikuwa darasa la nne) nilifuatilia historia yake nikajikuta nimevutiwa nayo na kuamua kuongeza juhudi katika masomo. 

“Kumwamini Mungu pia ni siri kubwa ya mafanikio yangu, uhusiano mzuri kati ya wazazi na walimu wangu na kusoma kwa bidii,” alisema.

Akielezea ratiba yake ya kila siku mwanafunzi huyo alisema huamka saa 12:00 asubuhi kisha hufanya usafi wa mwili na wa shule. Ikifika saa 12:45 huenda kunywa chai hadi saa 1:15 wanapokwenda mstarini.

Alisema kuanzia saa 1:30 huingia darasani hadi saa 10:20 jioni ambapo hutoka na kwenda kuoga kisha kwenda kupata chakula kuanzia saa 11:30 hadi saa 12:15 jioni ambapo huingia tena darasani kwa ajili ya kusali rozali.

Alisema husali rozali hadi saa 1:00 usiku kisha kuingia kujisomea hadi saa 5:30 usiku na kwenda kulala.

“Kidato cha kwanza hadi cha pili walikuwa wanalala saa 3:30 usiku lakini kidato cha tatu na cha nne tukawa tunalala sasa 4, lakini baadaye sisi wa kidato cha nne tulibadilishiwa ratiba tukawa tunalala saa 5:30 usiku,” alisema.

ATAMANI KUWA MWANASHERIA

Mwanafunzi huyo alisema matarajio yake ni kuja kuwa mwanasheria kwa sababu anapenda kutetea watu na anapenda kuona haki ikitendeka kila mahali.

“Kuna gazeti lilimuandika Rais Obama kuwa ni mwanasheria, baada ya kulisoma ndoto yangu ikaanzia hapo…na nitaendelea kusoma kwa bidii nataka nije kusoma Chuo Kikuu cha Havard Marekani…nataka niwe mwanasheria tena jaji na ikiwezekana zaidi niwe jaji mkuu,” alisema.

Aliwashauri wanafunzi kuwa na imani katika kile wanachokifanya na kuzingatia muda na kwenda mbele zaidi ya yale wanayofundishwa na walimu wao.

Alisema pia anajivunia wakati alipokuwa kiongozi shuleni kwani aliweza kujifunza mambo mengi.

“Nilikuwa dada mkuu msaidizi, kuna mambo mengi mazuri na ya kujifunza unakuwa mtu wa kati ya mwalimu na mwanafunzi kwahiyo unapata uchungu na utamu wa pande zote, kwakweli nilijifunza mambo mengi sana,” alisema.

Mwanafunzi huyo alisema anapenda sana kusoma vitabu, kuandika mashairi na kusafiri.

WAZAZI

Cynthia ni mtoto wa pili kuzaliwa kati ya watoto wanne na msichana pekee katika familia ya Nehemia Mchechu na Mercy Mchechu.

Mama mzazi wa Cynthia, Mercy alisema alikuwa akitegemea matokeo ya mwanawe kuwa mazuri kutokana historia yake katika madarasa ya nyuma.

“Kwa kweli ni jambo la kumshukuru Mungu na ni ndoto ya kila mzazi kuona mwanawe anafanya vizuri katika mitihani. Cynthia alikuwa akipenda sana mambo ya shule na amekuwa akisoma zaidi ya vitu ambavyo hupewa darasani.

“Tuliposikia habari hizi kwamba ameongoza kitaifa tumefurahi sana tunaendelea kumwombea kwa sababu safari yake bado inaendelea,” alisema Mchechu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles