25.2 C
Dar es Salaam
Friday, November 8, 2024

Contact us: [email protected]

BARCA YAVUNJA REKODI YA MIAKA 10 ESTADIO ANOETA

CATALUNYA, Hispania


BarcelonaMIAMBA ya soka nchini Hispania, Barcelona, wamefanikiwa kuvunja mwiko katika dimba la Estadio Anoeta mara baada ya kuibuka na ushindi wa bao 1-0 mbele ya wenyeji Real Sociedad katika mchezo uliotawaliwa na ufundi wa hali ya juu kwa pande zote mbili.

Ilikuwa ni siku ya aina yake kwa wapenzi na mashabiki wa miamba hiyo ya Catalunya ambayo licha ya ubabe wao kwa klabu nyingine zinazoshiriki La Liga, lakini wamekuwa wakipata wakati mgumu zaidi kila wanapoenda kukipiga katika dimba hilo lenye uwezo wa kubeba mashabiki 32,076.

Uwanja huo unaopatikana Manispaa ya San Sebastian, ulizinduliwa rasmi Agosti, 13, 1993 ni moja kati ya viwanja vigumu zaidi katika Ligi Kuu ya Hispania kwa wageni kuondoka na pointi tatu, klabu nyingi zimekuwa zikikumbana na kichapo.

Shukrani pekee zimwendee mshambuliaji wa Brazil, Neymar aliyefunga bao pekee kwa njia ya mkwaju wa penalti na kufikisha idadi ya mabao nane katika Ligi Kuu ya Hispania ‘La Liga’, mchezaji huyo ambaye mara ya mwisho kufunga katika mchezo dhidi ya Deportivo La Coruna Aprili 20, 2016.

Neymar alipata penalti hiyo katika dakika ya 21, alidhihirisha ubora wake mara baada ya kuwa katika ukame wa mabao kwa zaidi ya miezi mitatu na kurudi rasmi mbali na kufunga mshambuliaji huyo alipiga mashuti mawili yaliyokwenda nje ya uwanja.

Barcelona wamepata ushindi katika  mchezo huo uliopigwa katika dimba la Estadio Anoeta, ambapo imefanikiwa kujiweka mguu sawa kuelekea mchezo wa pili wa marudiano utakaopigwa wiki ijayo katika dimba la Camp Nou.

Wakali hao wa Camp Nou wamerudi mara baada ya kupata matokeo yasiyoridhisha katika michezo iliyopita kiasi cha kuachwa pointi sita na mahasimu wao Real Madrid ambao wamepoteza michezo miwili mfululizo ya ligi na Kombe la Mfalme.

Licha ya kuibuka na ushindi huo miamba hiyo ilikumbana na changamoto kubwa kutoka kwa mshambuliaji, Willian Jose ambaye alikuwa mwiba kwa safu ya ulinzi ya Wakatalunya hao waliokuwa kwenye kiwango cha hali ya juu katika mchezo huo.

Neymar ambaye alikuwa nje kwa muda kutokana na kushuka kwa uwezo wake alianza katika kikosi cha kwanza cha Barca mara baada ya kocha wake, Luis Enrique, kufanya mabadiliko saba katika kikosi chake cha kwanza kilichocheza mchezo uliopita wa La Liga.

Katika mchezo huo mbali na Neymar, pia mlinzi wa kati raia wa Ufaransa, Samuel Umtiti, alionyesha ukomavu wa hali ya juu kwa kuonyesha soka la kuvutia na kuwa kikwazo kwa Real Sociedad ambao walikuwa wakihaha kuhakikisha wanaondoka na ushindi na kuendeleza rekodi yao kwa wababe hao.

Mfaransa huyo alionyesha kuwa ameanza kuzoea katika kikosi cha Enrique ambaye ameonyesha kumwamini zaidi mlinzi huyo wa kati huku mlinda mlango, Jasper Cillessen, pia aking’aa zaidi katika mchezo huo na kuwastaajabisha mashabiki wa klabu hiyo waliojitokeza katika dimba hilo kushuhudia mtanange huo.

Enrique ambaye ameanza kumwamini Jasper Cillessen ambaye alimsajili kuziba pengo la Claudio Bravo ambaye alijiunga na Manchester City, ameanza kupata nafasi hiyo kutokana na kocha wake kuanza kumpumzisha Andre ter Stegen ambaye amekuwa akifanya makosa ya kizembe ambayo yamekuwa yakiigharimu timu.

Mholanzi huyo amezidi kuimarika kadiri siku zinavyozidi kwenda huenda akamnyang’anya namba mtangulizi wake aliyemkuta klabuni hapo ambaye amekuwa akibweteka siku za karibuni.

Katika mchezo huo moja kati ya maeneo yaliyokuwa na ushindani mkubwa, ilikuwa sehemu ya kati ambapo vita ilikuwa kati ya kiungo wa ulinzi wa miamba hiyo, Sergio Busquet na Asier Illarramend ambao walikuwa wakitumia nguvu kubwa na kuonyeshana umwamba ambapo mwisho wa siku Busquet aliibuka kinara katika vita hiyo.

Ni ushindi wa kihistoria kwa miamba hiyo ambayo mara ya mwisho kushinda katika dimba la Anoeta ilikuwa mwaka 2007, Barca  imekuwa ikipata matokeo yasiyoridhisha katika dimba hilo ambalo limekuwa kama mkosi kwao,                                                                                                                      wakali hao wametoka kupoteza mchezo uliopita dhidi ya Athletic Bilbao na kutoa morali ya kikosi chao.

Real Sociedad ambao wamekuwa wakiwapa ushindani mkubwa makocha waliopita katika kikosi cha Barca ambao wengi wamekuwa wakipoteza michezo mbele ya wabishi hao wa Anoeta wakianzia na Pep Guardiola, Tito Vilanova, Tata Martino na hivi sasa Luis Enrique ambaye alipoteza mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya wakali hao katika mzunguko wa kwanza.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles