32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

DK. KATABARO: TUSIILAUMU MTWARA KUFELISHA, TUJIULIZE MAZINGIRA YA ELIMU YAKOJE?

Dk. Joviter Katabaro

Na FARAJA MASINDE,

HIVI majuzi, Serikali ilitangaza matokeo ya kidato cha pili na yale ya darasa la nne kwa mwaka 2016/17 ambapo ufaulu umeonekana kupanda kwa kiwango kikubwa.

Akitangaza matokeo hayo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani Tanzania (NECTA), Dk. Charles Msonde hakusita pia kuweka wazi juu ya udanganyifu uliofanywa na wanafunzi kwenye mitihani hiyo ambao ulisababisha baadhi  ya wanafunzi kufutiwa matokeo.

Baraza lilitangaza wanafunzi wanaopaswa kurudia darasa licha ya awali serikali kuukataa mpango huo.

Wasomi na wadau mbalimbali wa elimu wametoa mtazamo wao juu ya matokeo hayo ikiwamo kuitaka serikali kwenda mbali zaidi katika kupima uelewa wa wanafunzi nje ya mitihani pekee.

Wasomi

Dk. Joviter Katabaro wa Shule ya Elimu katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anasema utaratibu wa mitihani ya darasa la nne na kidato cha pili ni mzuri kwa kuwa unawakumbusha wazazi na Taifa kutambua uelewa wa watoto wao.

“Changamoto iliyopo hapa ni namna gani tunaweza kutambua iwapo wanafunzi hawa wanafundishwa sawa sawa, kwa mfano maeneo kama Mkoa wa Mtawara ambako kwa kiwango kikubwa wanafunzi wake hawajafanya vizuri je, kuna viwezeshi? Kwa maana ya vitendea kazi, hali ya madarasa, walimu na miundombinu mingine.

“Haitoshi kusema tu kwamba kuna madarasa… ukiangalia katika mkoa huu karibu shule nyingi za sekondari zinauwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 20 jambo ambalo ni changamoto kubwa, hivyo ni lazima kuwapo na viwezeshi vilivyosawa kwa shule zote hapa nchini.

“Tunaweza tukalaumu mkoa kuwa haujafanya vizuri au shule kumbe madarasa hakuna au vitabu hakuna hivyo, matokeo au mitihani pekee haitoshi kuwa kipimo sahihi kwa elimu yetu bila kuangalia iwapo kuna usawa wa miundombinu na vitu vingine vya msingi,” anasema Dk. Katabaro.

Anasema haitoshi kwa mitihani hii kuwa kipimo kwa wanafunzi ambao wanatoka kwenye mazingira tofauti kuwafanya wawe kwenye kiwango sawa kwa maana ya ufaulu.

“Binafsi naona haya matokeo ya mitihani pekee bado si kielelezo bora cha kufanya vizuri, hivyo ni bora tukaangalia matokeo haya kwa kuzingatia miundiombinu ya shule zetu bila ya kuhukumu, ni vizuri kuwapo kwa kipimo hiki ili kuhakikisha elimu yetu inakuwa kwenye mlengo sahihi,” anasema Dk. Katabaro.

 Wazazi

Athumani Hashim ambaye ni mzazi na mdau wa sekta ya elimu nchini, anasema matokeo yamekuwa mazuri kwa shule za binafasi kuliko zile za serikali hivyo juhudi zaidi zinahitajika kwa shule hizi.

“Ukiangalia mikoa ya kusini ambayo ndiyo inaongoza kwa kushika mkia, imekuwa haifanyi vizuri kwa kipindi kirefu jambo ambalo serikali inapaswa kulitafakari kwa kina na kulitafutia ufumbuzi wa kudumu, kwa kuhakikisha shuleni kunakuwapo miundombinu rafiki kwa wanafunzi na walimu.

“Baada ya kuiboresha, mwaka unaofuata ufanyike tena tathimini ya hali ya ufaulu, kama utakuwa umepanda basi Serikali itakuwa imepata suluhu ya kufeli kwa wanafunzi wanaosoma shule za Serikali,” anasema Hashim.

Anabainisha kuwa pamoja na serikali kuendelea na utekelezaji wa kutoa elimu bure, isiishie tu hapo bali ihakikishe pia inatoa elimu bora.

“Ifike mahali wanafunzi wanaofeli wawe wachache kuliko ilivyo sasa. Utaratibu huu wa kukariri darasa utamfanya mwanafunzi aongeze bidii kama kweli ana nia ya kusoma.

“Pia itapunguza wimbi la wanafunzi wanaofeli kidato cha nne, ambako huko wanakuwa hawana nafasi ya kurudia darasa hivyo ni bora wakajiimarisha mapema wakiwa katika ngazi za chini,” anasema na kuongeza kuwa:

“Maslahi ya walimu pia yanapaswa kuboreshwa hasa wale waliopo vijijini ambako mazingira wanayofanyia kazi ni magumu.”

Ikumbukwe kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, imezitaka shule zote zilizowataka wazazi/walezi kuwahamisha watoto wao kwa kigezo cha kutofikia wastani wa ufaulu, kufuta agizo hilo na kuendelea na wanafunzi hao bila masharti yoyote.
Hivyo, Kaimu Kamishna wa Elimu, Nicolas Buretta aliagiza wazazi wenye wanafunzi waliorudishwa nyumbani kwa sababu hiyo wahakikishe wanawarudisha kwenye shule walizokuwa wakisoma ili waendelee na masomo yao kama kawaida.
“Serikali imefikia hatua hiyo baada ya kubainika kuwa bado kuna shule nyingi za msingi na sekondari hususani zisizo za Serikali hasa za kidini zinaendelea kukaririsha, kuhamisha au kuwafukuza wanafunzi kwa kigezo cha kutofikia alama za ufaulu zilizowekwa na shule hizo jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

“Shule ni lazima ziwe na utaratibu wa kuinua viwango vya taaluma kwa wanafunzi wenye ufaulu mdogo na si kuwakaririsha darasa. Iwapo ikitokea ni lazima kufanya hivyo, taratibu zilizopo zifuatwe,”anasema.

 Tamongsco

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania, (Tamongsco), Benjamin Nkonya anasema wanachama wake hawafukuzi wanafunzi baada ya kushindwa vigezo bali inaangalia uwezo wake wa kujifunza mambo mawili; ung’amuzi wa kujifunza kwa nadharia na ufundi au mchindo.
“Tukiona mwanafunzi amefeli katika ung’amuzi, mfumo ambao Serikali inauzungumzia, tunampeleka katika mchindo ambao ni ufundi stadi na si kuwarudisha nyumbani,” anasema.

Anafafanua kuwa mchindo ni kama chuo cha Veta ambacho dereva asiyejua kusoma na kuandika anakwenda kujifunza mwishowe anakuwa dereva bora.
Anasema mfumo huo unasaidia kukuza wabunifu hasa katika mapinduzi ya Serikali kuwa nchi ya viwanda.
Hata hivyo, Waziri Kivuli wa Elimu, Suzan Lyimo amenukuliwa akisema kinachofanyika kwa mujibu wa agizo hilo ni Serikali kutaka shule za Serikali na binafsi ziwe na mfumo wa utoaji elimu unaofanana jambo ambalo ni gumu.

Anasema kuwa utaratibu huo ni wazi kuwa unapingana moja kwa moja na huu uliotolewa na Necta ambapo.

Kwa mujibu wa Dk. Msonde wanafunzi 36,737 sawa na asilimia 8.98 watakariri kidato cha pili mwaka huu kutokana na kushindwa mtihani huo.
Wanafunzi waliofanya mtihani huo ni 410,519 kati yao waliopata wastani wa kuanzia alama 30 na kuendelea ni 372,228 sawa na asilimia 91.02 ambao wataendelea na kidato cha tatu.
Kwa darasa la nne, wanafunzi 67,547 (asilimia 6.64) waliopata alama ‘E’ kwenye Mtihani wa Upimaji wa Taifa (SFNA) nao watakariri darasa hilo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles