32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

BAYPORT ILIVYOIKOMBOA SEKTA YA ELIMU MOROGORO

Meneja masoko na Mawasiliano wa Bayport, Ngulu Cheyo (kushoto), akimkabidhi Kompyuta Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe.
Meneja masoko na Mawasiliano wa Bayport, Ngulu Cheyo (kushoto), akimkabidhi Kompyuta Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe.

Na Mwandishi Wetu,

UHITAJI wa vitendea kazi vya kisasa, zikiwamo kompyuta ni jambo linalohitaji kufanyiwa kazi kwa sababu kukua kwa sayansi na teknolojia kunalazimisha ofisi nyingi zikiwamo za umma kumiliki vifaa hivyo kwa lengo la kurahisisha utendaji wa kazi.

Mathalani, badala ya kupanga makaratasi ya wahitimu ndani ya kabati kwenye sekta ya elimu, sasa kompyuta moja tu inaweza kuhifadhi nyaraka za matokeo za wahitimu wa mkoa mzima, tena yakipatikana kwa urahisi.

Ni tofauti na mtumishi wa umma kushinda katika chumba cha kuhifadhia nyaraka hizo, akitafuta majina hayo, badala yake atakapohitaji tu, atayapata kwa haraka na kuendelea na kazi nyingine za ujenzi wa Taifa.

Kwa kuliangalia hilo, usambazwaji wa kompyuta 80 za Taasisi ya Kifedha ya Bayport kwa mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara kunaonyesha namna gani Taifa litakavyonufaika na utolewaji wa vifaa hivyo vya kisasa vya kiofisi vinavyoendana na wakati.

Usambazwaji huo ulianza mwishoni mwa mwaka jana, ambapo mikoa iliyonufaika hadi sasa ni pamoja na Morogoro, Arusha, Kilimanjaro na Mbeya.

Akizungumzia utoaji wa kompyuta hizo, Meneja Masoko na Mawasiliano wa Bayport, Ngula Cheyo anasema msaada wa kompyuta hizo utapunguza changamoto za uhaba wa vifaa hivyo katika ofisi za umma.

“Tunajua hatuwezi kulimaliza tatizo hili kwa haraka, lakini tutapunguza uhaba huo na kuisaidia serikali yetu kwa sababu haiwezi kufanya kila jambo.

“Mchakato huu ulianza mwishoni mwa mwaka jana ambapo jumla ya kompyuta zilizopo ni 205 zenye thamani ya Sh milioni 500, huku kompyuta 125 zikiachwa makao makuu ya Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na zilizosalia 80 ndizo tunazosambaza mikoani kwenye ofisi za serikali,” anasema Cheyo.

Mkuu wa Mkoa Morogoro, Dk. Stephen Kebwe, anaunga mkono uzalendo wa Bayport na kuwataka waendelee kubuni mambo mengine ili nchi isonge mbele.

“Tumepokea kompyuta hizi sita kwa furaha kubwa kwa sababu tunaamini zitaongeza ufanisi wa kazi, uwajibikaji na utumishi wa mfano kwa kutumia kompyuta hizi.

“Ni msaada mkubwa mno ambao mbali na kuboresha katika mambo ya takwimu kwa utawala, pia zinaweza kutumika katika harakati za kuona mkoa wetu unapiga hatua katika sekta ya elimu kwa kutunzia kumbukumbu muhimu zikiwamo za ufaulu,” anasema.

Dk. Kebwe anawataka Bayport wasaidie kujenga madarasa hususani Morogoro Vijijini ili kusaidia kukuza kiwango cha elimu, akisema eneo hilo lina hali mbaya na linahitaji ushirikiano mkubwa.

“Tunawaomba Bayport, mje kwetu Morogoro Vijijini mtusaidie kutujengea madarasa katika baadhi ya shule zenye uhitaji mkubwa, tukiamini mtaikomboa jamii inayoendelea kudidimia kutokana na changamoto za ukosefu wa elimu bora… chanzo kikiwa ni jiografia ya maeneo hayo,” anasema Kebwe na kusisitiza kuwa kompyuta hizo zilizotolewa kwa Halmashauri ya Wilaya Mvomero, Halmashauri ya Morogoro na Manispaa ya Morogoro zimekuja wakati mwafaka.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Said Mecky Sadick anawapongeza Bayport kwa ubunifu huo utakaochangia utendaji kazi kwa watumishi wa serikali si mkoani kwao tu, bali kwa maeneo yote nchini.

“Nawashukuru viongozi wote wa Bayport kwa kutusaidia kompyuta kwa sababu kwangu zimekuja wakati mwafaka, kwani ofisi za Halmashauri ya Mwanga ziliungua moto mwishoni mwa mwaka jana.

“Kompyuta hizi sita zitakwenda Mwanga, Same na Manispaa ya Moshi… naomba mtuongezee tena vifaa hivi kwa ajili ya Mwanga pekee maana uhitaji ni mkubwa,” anasema Sadick.

Anakiri kuwa uwapo wa kompyuta utachangia utoaji wa huduma bora kwa watumishi wao kama njia ya kukuza uchumi wa nchi.

Ofisa Utumishi wa Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, Emelda Kisosi, hakusita kuwapongeza Bayport kwa kuwafikishia kompyuta mbili za msaada, akiamini kuwa zitawasaidia kwa kiasi kikubwa.

“Ni jambo la kushukuru… msaada huu ni mkubwa kwetu watumishi wa Halmashauri ya Arumeru.

Naye Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Mbeya, Nyasenga Enock alipokea kompyuta nane za Bayport huku akiwahikikishia kwamba watakaporudi kwao watakuta maendeleo makubwa kwa kutumia vyema mashine hizo sambamba na kuzitunza ipasavyo.

“Tutazitunza kompyta hizi ili zilete tija kama iliyokusudiwa, hivyo katika hili wenzetu wa Bayport msitie hofu na tunaomba tuendelee kushirikiana kwa namna moja ama nyingine ili kwa pamoja nchi yetu iweze kusonga mbele,” anasema Enock.

Mratibu wa Masoko na Mawasiliano wa Bayport, Mercy Mgongolwa, anawataka Watanzania wote kuiunga mkono taasisi yao katika sekta ya mikopo kwa sababu imedhamiria kuwakwamua kwa kupitia sekta ya mikopo nafuu na ya haraka, ikipatikana katika ofisi zaidi ya 80 katika mikoa na wilaya mbalimbali za Tanzania Bara.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles