Na Jonas Mushi, Dar es Salaam
MAMLAKA ya Hali ya Hewa nchini (TMA), imesema mvua ya mawe iliyonyesha Jumanne wiki hii wilayani Kahama na kusababisha vifo vya watu 46 na wengine 80 kujeruhiwa haikuwa ya kawaida katika ukanda huu wa kitropiki.
Mamlaka hiyo imetanabahisha kuwa iliona hali ya kuwepo kwa tonado (barafu) katika eneo la ukanda wa Ziwa Victoria nusu saa kabla ya mvua hiyo kunyesha.
Akitoa taarifa kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dk. Agnes Kijazi, alisema kabla ya mvua hiyo Mamlaka ilitoa utabiri wa saa 24 ulioonyesha kuwepo kwa wingu zito pamoja na radi katika eneo la ukanda wa Ziwa Victoria.
Alisema nusu saa kabla ya kutokea kwa tonado, mitambo ya TMA iliona hali hiyo iliyosababishwa na kushuka kwa barafu katika usawa wa dunia na kushindwa kuyeyuka, hivyo kutokana na upepo na ngurumo za radi iliyokuwepo, barafu hizo zikadondoka kabla hazijayeyuka.
“Huwa hatutarajii hali iliyotokea huko Shinyanga kwenye ukanda wa kitropiki, lakini kilichotokea ni kutokana na mabadiliko ya tabia ya nchi ambapo tunaweza kuona mabadiliko fulani ambayo hatujawahi kuyaona katika ukanda wetu siku za nyuma,” alisema Kijazi.
Alifafanua kwamba kwa kawaida mvua husababishwa na unyevu unaotoka usawa wa dunia na kupanda juu, kisha huganda kutokana na baridi iliyopo anga la juu na baadaye mgandamizo na misukumo inapotokea barafu hiyo hushuka chini ya usawa wa dunia na kadri inavyoshuka huyeyuka na kuwa mvua.
“Tonado hutokea wakati barafu iliyopo anga la juu inaposhuka na kukuta hali ya ubaridi katika usawa wa dunia, hivyo hushindwa kuyeyuka vizuri na kunapokuwa na ngurumo za radi husababisha barafu hizo kudondoka ardhini na huweza kuleta madhara kama yaliyotokea,” alifafanua Dk. Kijazi.
Kijazi aliendelea kufafanua kuwa ndani ya muda waliogundua kuwapo kwa tonado katika eneo hilo, haikuwa rahisi kutoa taarifa na kuwafikia wananchi kwa haraka ili wachukue tahadhari, ukizingatia ilikuwa ni usiku na kukiwa na changamoto ya njia ya kutoa taarifa za hali ya hewa.
Pia alielezea changamoto mbalimbali zinazoikabili mamlaka hiyo katika utoaji wa taarifa sahihi, ambapo alisema kuwa uhaba wa vifaa na fedha umekuwa ukisababisha kuwapo kwa ufinyu wa vituo pamoja na mitambo ya kukusanya na kusambaza taarifa za hali ya hewa.
“Tuna uhaba wa mitambo ya kupima hali ya hewa ya anga la juu, ambapo tunahitaji kuwa na mitambo mine, lakini kwa sasa upo mtambo mmoja tu uliopo Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
“Pia tuna rada za hali ya hewa mbili badala ya rada tano zinazohitajika, hata hivyo, rada hizo zipo kwenye mpango wetu wa mwaka huu wa fedha na tunasubiri fedha kutoka serikalini ili kuweka rada hizo,” alisema Kijazi.
Pamoja na kuwapo kwa changamoto nyingi, Kamati ya Bunge iliridhishwa na utendaji kazi wa mamlaka hiyo na kuitaka serikali kupeleka fedha mapema ili iweze kuboresha utendaji kazi wake, kwani ni moja ya mamlaka muhimu.
“Kamati ilichogundua ni kuwa mamlaka hii ni muhimu sana kwa uchumi, elimu na usalama wa Taifa letu, hivyo tunaiomba serikali kuhakikisha inapeleka fedha ili iweze kutekeleza miradi mbalimbali ambayo itaboresha huduma zinazotolewa,” alisema Aliko Kibona, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu na Mbunge wa Jimbo la Ileje.
Kibona aliishauri TMA kuharakisha mchakato wa kuanza ujenzi wa jengo la mamlaka hiyo ili kuepuka gharama kubwa wanazolipa, kama pango la nyumba ambazo ni takribani milioni 132 kwa mwezi na akaongeza kwa kuitaka serikali kuharakisha mchakato wa marekebisho ya sheria ya mamlaka ya hali ya hewa itakayotoa fursa kwa mamlaka kuuza huduma zake ili kujiongezea mapato.
Mbali na kusababisha vifo na majeruhi, pia mvua hiyo ya mawe iliua mifugo pamoja na kuharibu mazao mbalimbali na makazi ya watu.