Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amewaagiza majaji na mahakimu wanawake kote nchini kukabiliana na vitendo vya rushwa na unyanyasaji wa kijinsia ili kusaidia wanawake kupata haki zao za msingi bila kubaguliwa.
Agizo hilo alilitoa Dar es Salaam jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nane wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA).
Pia ameonya kuhusu vitendo vya rushwa ya ngono inayofanywa na baadhi ya watendaji wenye madaraka na kusema tabia hiyo ni mbaya na lazima ikomeshwe.
Alisema vitendo hivyo vya rushwa ya ngono huzuia na kukwamisha juhudi za wanawake kufikia huduma za kijamii, ikiwamo elimu, ajira na haki kwa ustawi wa wanawake.
Katika hatua nyingine, alikishukuru Chama cha Dunia cha Majaji Wanawake (IAWJ) kwa mchango na msaada wake kwa TAWJA katika programu ya miaka mitatu ya kupambana na matumizi mabaya ya madaraka na rushwa ya ngono.
“Pia naipongeza Wizara ya Katiba na Sheria, Shirika la UN Women na wadau wengine wa TAWJA kwa kuunga mkono mapambano ya aina zote za ubaguzi na ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini,” alisema.
Samia alisema elimu ya haki za binadamu iliyotolewa na TAWJA imeleta mabadiliko kwa wengi kupitia mafunzo na machapisho, hivyo jitihada hizo lazima ziongezwe ili huduma hiyo iweze kuwafikia wananchi wengi zaidi kote nchini.
Aliitaka TAWJA iendelee kutoa msaada katika kuwasaidia wanawake na watoto wanaokandamizwa kwa kunyimwa haki zao katika jamii.