26.1 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MAJALIWA AZINDUA MRADI WA MAJI WA BILIONI 1.09/-

majaliwakassim

Na Mwandishi Wetu- Ruvuma

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, amezindua mradi wa maji safi na tenki lenye uwezo wa kuhifadhi lita 200,000 utakaohudumia vijiji viwili vya Mkongotema na Magingo katika Kata ya Mkongotema, Wilaya ya Songea mkoani Ruvuma.

Akisoma taarifa ya mradi huo kwa Majaliwa juzi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Madaba, Shafi Mpenda, alisema mradi huo ulianza kujengwa mwaka 2013 na umegharimu Sh bilioni 1.09.

“Hadi kukamilika kwake, mradi huu umegharimu shilingi 1,092,439,812 na kati ya hizo, shilingi 1,069,647,312 zimetolewa na Serikali kuu na shilingi 22,792,500 zimechangwa na wananchi,” alisema.

Mpenda alisema hadi sasa kaya 915 zenye watu 5,300 zinahudumiwa na mradi huo wenye vituo 57 vya kutolea huduma za maji kwa jamii. Alisema lengo lao ni kufikisha vituo 71 ifikapo mwishoni mwa mwaka huu.

Pia alisema kukamilika kwa mradi huo kumesaidia kuwapunguzia wananchi gharama za kununua maji ambapo pipa moja liligharimu Sh 3,000. “Pia kutasaidia kupunguza adha ya kufuata maji umbali mrefu, kupunguza magonjwa yanayotokana na mlipuko na kuwapa wananchi muda wa kutosha kufanya shughuli nyingine za maendeleo,” alisema.

Akizungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi wa mradi huo, Majaliwa, aliwapongeza wakazi hao kwa kukubali kuchangia ujenzi wa mradi huo kwa sababu katika baadhi ya maeneo miradi kama hiyo imekwama kukamilika kwa sababu wananchi waligomea kuchangia.

Aliwataka wakazi wa vijiji hivyo wasiharibu mazingira na watunze vyanzo vya maji ili mradi huo uweze kuwa endelevu. “Mradi huu ni lazima tuutunze kwa sababu hali ya hewa imebadilika hivi sasa, sababu ni sisi wenyewe wananchi ambao tumekata miti ili kupanua maeneo ya kilimo,” alisema na kuongeza:

“Changamoto inayotupata hivi sasa ni kwamba tumebakia kuwa na eneo kubwa la kilimo lakini mazao yanayopatikana ni kidogo. Mtazamo wetu katika Serikali hivi sasa ni kulima kwenye eneo dogo lakini mavuno yawe mengi.

“Mtu asilime chochote karibu na chanzo hiki ili tuweze kukitunza chanzo chetu. Na wenyeviti wa Serikali za vijiji vyote viwili, wekeni utaratibu wa wananchi kwenda kupanda miti ili eneo hili libaki kuwa na unyevunyevu kwa muda mrefu.

“Sera ya Serikali ni kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata maji katika umbali usiozidi mita 400 na hili tutaweza kulitimiza kama tu mtatunza vyanzo vya maji vilivyopo.”

Pia alikagua utoaji huduma katika Kituo cha Afya cha Madaba na ujenzi wa Kituo cha Kupozea Umeme cha Madaba.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles