Na ASHA BANI – Dar es Salaam
WIZARA ya Maliasili na Utalii kupitia askari wa wanyamapori wa Pori la Akiba la Selous, Kanda ya Kaskazini Mashariki Kingupira, imewaokoa wafugaji 50 waliokuwa wakiwapitisha ng’ombe 18,000 ndani ya pori hilo.
Mbali na kuwaokoa, pia wamekuta mizoga saba ya ng’ombe ikiwa imekufa katika pori hilo kwa kukosa chakula na maji.
Wafugaji hao wenye asili ya Kimasai, walikuwa na ng’ombe 1,780, kondoo  200 na punda sita baada ya kutelekezwa kwa muda wa siku tano na mtu mmoja aliyetajwa kwa jina moja la Mzigua, aliyewarubuni kwamba  atawaonyesha njia za mkato bila wao kujua na baadaye kuwakimbia.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja  Jenerali Gaudence Milanzi, aliyewatembelea wafugaji hao jana, aliagiza waachiwe huku akitoa wito kwa wananchi kuacha kupita maeneo ya hifadhi kwa vile ni kosa kisheria.
Milanzi alikwenda kuwapa pole na kuwapelekea chakula na maji wafugaji hao, huku akitaka aliyewadanganya kwa kuwapitisha ndani ya hifadhi hiyo asakwe ili hatua kali dhidi yake ziweze kuchukuliwa.
Mmoja wa wafugaji aliyekuwa katika msafara huo, Lisesi Cherehani, akielezea namna walivyotelekezwa katika pori hilo, alisema kuwa walianza safari hiyo Jumatano wiki iliyopita wakitembea usiku na mchana kwa muda wa siku tano bila kujua kama wanapitishwa ndani ya hifadhi.
Alisema walipokuwa ndani ya hifadhi ndipo wakaanza kushikwa na kiu kwa vile maji waliyokuwa nayo yaliwaishia na kila walipokuwa wakijaribu kumuuliza aliyewapitisha njia hiyo, alikuwa akiwaambia baada ya muda mfupi watakutana na maji, huku wakiendelea na safari bila mafanikio.
“Tulimpa Mzigua zaidi ya Sh milioni 5 kama malipo ya kutufikisha Ilonga mkoani Morogoro tukitokea vijiji vya Ndundunyekanza, Kipungila na Chumbi wilayani Rufiji mkoani Pwani, kwa makubaliano kuwa atatupitisha njia fupi ya mkato tutakayotembea kwa muda wa siku tano tu, hatukujua anatupitisha ndani ya pori hili,” alisema Cherahani.
Alisema baada ya kukosa maji na chakula kwa muda mrefu, wakaanza kuanguka na baadhi yao walianza kunywa mikojo yao pamoja na damu za kondoo kuokoa maisha yao.
Aliongeza kuwa wasingekuwa askari wa wanyamapori ambao walikuja kuwapa msaada wa kibinadamu kwa kuwapatia maji pamoja na kuwanywesha uji wangepoteza maisha.
Awali, Mkuu wa Kanda ya Mashariki Kingupira, Paschal Mrina, alisema walipata taarifa za kupotea wafugaji hao kutoka kwa wasamaria wema pamoja na uongozi wa Wilaya ya Rufiji.