Paul Kayanda na Kadama Malunde, Kahama
WATU 42 wamefariki dunia na wengine zaidi ya 91 wamejeruhiwa vibaya baada ya mvua kubwa ya mawe iliyoambatana na upepo mkali kunyesha katika Kijiji cha Mwakata, Kata ya Isaka, Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga.
Pamoja na vifo hivyo, nyumba za makazi na majengo ya taasisi mbalimbali, yamebomolewa na mafuriko yaliyosababishwa mawe kusambaa kijiji kizima.
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Benson Mpesya, aliiambia MTANZANIA kwa simu jana kwamba zaidi ya kaya 100 zimeathiriwa na mvua hiyo, nyumba 160 zimebomolewa na zaidi ya watu 600 hawana makazi.
“Ndugu mwandishi naomba mtuombee Mungu kwa sababu hali zetu ni mbaya sana tena sana, kwani tangu saa 11 alfajiri hadi jioni hii tunavyozungumza sijapumzika.
“Kwa takwimu tulizonazo ni kwamba watu 42 wamepoteza maisha, mejeruhi ni kama 91, kaya 100 zimeathiriwa, watu zaidi ya 600 hawana makazi na nyumba zaidi ya 160 zimebomolewa.
“Kwa wale wenzetu waliosalimika tunatarajia kuwahifadhi katika Shule ya Msingi Mwakata na wengine watachukuliwa na ndugu, jamaa na marafiki zao wenye nafasi za kuwahifadhi.
“Majeruhi tumewapeleka katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama ila wanne tumewapeleka katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga kwa matibabu zaidi.
“Hadi sasa nawashukuru watu mbalimbali wametoa misaada mingi na tumefanikiwa kupata vyakula mbalimbali kama maji, sukari, chumvi, viberiti, mishumaa, mikate, mafuta ya kula, juisi na vitu vingine.
“Tunatarajia kuwagawia waathirika wote vitu hivyo kwa sababu bila kufanya hivyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa vile hawana hata pa kuanzia,” alisema mkuu huyo wa wilaya.
Kuhusu vifo vilivyotokea, Mpesya alisema kuna baadhi ya familia zimepoteza watu wote na nyingine zimepoteza baadhi ya wanafamilia.
“Kuna familia moja ilikuwa na watu saba wote wamefariki dunia, familia nyingine ilikuwa na watu watano, wote wamepoteza maisha na familia nyingine zilipoteza watu kadhaa tu,” alisema Mpesya.
Katika maelezo yake, Mpesya alisema mvua ya mwisho kubwa kunyesha mkoani Shinyanga ilikuwa Septemba 4 mwaka jana ambako mabwawa ya maji katika Mgodi wa Dhahabu wa Bulyankulu yalifurika maji na kutiririsha maji ya kemikali katika maeneo ya makazi ya wananchi.
Wakati mkuu huyo wa wilaya akisema hayo, mtoa taarifa mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Bakari Karandi, mkazi wa Kijiji cha Mwendakulima ambaye alikwenda kijijini hapo baada ya mvua hiyo kunyesha, aliiambia MTANZANIA kwa simu jana kwamba mifugo mbalimbali ikiwamo ng’ombe, mbuzi, kondoo, punda, kuku, nguruwe na mingine, imekufa maisha kutokana na kukumbwa na mafuriko.
Alisema mvua iliyosababisha madhara hayo ilinyesha juzi saa 4.00 usiku kwa saa tatu ingawa mvua kubwa zaidi ilidumu kwa dakika zipatazo 21.
“Hapa nilipo niko Kijiji cha Mwakata ambacho kimekumbwa na mafuriko ya ajabu. Hali kijijini hapa ni mbaya, yaani kijiji chote kimesambaratishwa na mafuriko, nyumba karibia zote zimebomolewa na bado kuna mawe ya barafu yamekusanyika katika maeneo mbalimbali.
“Kuna mahali nimepita nimekuta kwenye mji mmoja kuna majeneza makubwa matano, maana yake ni kwamba katika mji huo kuna watu wazima watano, wamefariki dunia.
“Kuna mji mwingine nimeona kuna majeneza manne makubwa na madogo, kwingine nimeona majeneza mawili yaani ndugu yangu hali ni mbaya, katika uhai wangu sijawahi kuona kitu kama hiki.
“Nilipita sehemu nyingine nimekuta mifugo mingi ajabu imekufa, aisee, hali ni mbaya ndugu yangu, hawa wenzetu wanahitaji msaada wa haraka vinginevyo hali inaweza kuwa mbaya zaidi kwa sababu mazao yote yameharibiwa.
“Hata zile nyumba moja moja zilizobaki zimezingirwa na maji na naamini kama mvua itanyesha tena, nazo zinaweza kuharibiwa ila tuombe Mungu isinyeshe tena,” alisema Karandi na kuvitaja vijiji vilivyoathiriwa na mvua hizo kuwa Mwakata, Nhumbi na Magung’humwa.
RPC Shinyanga
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Justus Kamugisha, alisema jitihada za kuopoa miili zinaendelea ikiwa ni pamoja na kuokoa mali mbalimbali zilizofunikwa na udongo. Alisema tukio la aina hiyo halijawahi kutokea mkoani Shinyanga.
Mganga mkuu wa wilaya
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Dk. Joseph Ngowi, aliwaambia waandishi wa habari kuwa majeruhi watatu kati ya waliokuwa wamefikishwa hospitalini hapo walikufa.
“Hatuna idadi kamili ya watu waliojeruhiwa au waliokufa, hivi sasa tumewatuma madaktari wetu kwenda kijijini hapo kwa ajili ya kutoa huduma ya kwanza na kufanya uchunguzi kubaini idadi kamili ya waliofariki dunia. Tutakapopata taarifa kamili tutawaeleza,” alisema Dk. Ngowi.
Zimamoto watoa msaada
Kamanda wa Kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga, Elisa Mugisha, alisema baada ya kupata taarifa za tukio hilo, askari wa kikosi hicho walikwenda kutoa msaada.
“Tulipata wakati mgumu kutokana na ubovu wa miundombinu lakini tulijitahidi kadiri tulivyoweza na kufanikiwa kuokoa maisha ya baadhi ya wananchi.
Majeruhi wazungumza
Mmoja wa majeruhi waliolazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama, Paulina Malongo, aliiambia MTANZANIA kwamba mvua ilianza kunyesha saa 4.00 usiku ikiambatana na upepo mkali.
“Ilikuwa kama saa 4.00 hivi tulikuwa tumelala, ghafla nikasikia upepo mkali ukiambatana na mvua kubwa ya mawe. Mvua ilipozidi maji yakaanza kuingia ndani, ghafla nyumba iliezuliwa na kuanguka.
“Wakati tunajiokoa wajukuu zangu wanne walishindwa na walipoteza maisha kwa sababu waliangukiwa na nyumba,” alisema Paulina.
Rais Kikwete atuma rambirambi
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete amemtumia salamu za rambirambi Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Ali Rufunga, kuomboleza vifo vilivyotokea na kuwatakia kheri majeruhi.
“Nimepokea kwa huzuni na masikitiko makubwa taarifa za vifo vya watu 42 waliopoteza maisha na wengine 91 waliojeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kahama kwa matibabu baada ya nyumba zao kusombwa na maji.
“Msiba huo siyo wa wana Shinyanga pekee bali ni wa Taifa zima ambalo limepoteza nguvukazi muhimu kwa maendeleo yake na ustawi wa jamii ya Watanzania kwa ujumla.
“Naomba upokee salamu zangu za rambirambi za dhati za moyo wangu kwa kupotelewa ghafla na wananchi 42 kwa mara moja katika mkoa wako. Kupitia kwako, naomba rambirambi zangu ziwafikie wafiwa wote kwa kuondokewa na wapendwa, ndugu na jamaa zao.
“Namuomba Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema azipokee na kuzilaza roho za marehemu wote mahala pema peponi, amina”, alisema Rais Kikwete katika salamu zake zilizotumwa na Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu.
Pia aliwaomba wafiwa wote wawe na moyo wa uvumilivu, utulivu na subira wakati huu wa majonzi makubwa kwao wanapoomboleza vifo vya ndugu na jamaa zao, lakini amewataka wasisahau ukweli kwamba kazi ya Mungu haina makosa.
Aliwahakikishia wafiwa wote kuwa yuko pamoja nao katika kipindi chote cha kuomboleza msiba huu mkubwa kwao na kwa Taifa.