27 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

PANGA KUFYEKA WENGINE TANESCO

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka

* Lengo ni kuimarisha utendaji, ufanisi wa kazi

Na ASHA BANI – Dar es Salaam


 

SIKU moja baada ya vigogo watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kushushwa vyeo, uongozi wa shirika hilo umesema utaendelea na fagio hilo kama njia ya kuongeza ufanisi kwenye utendaji.

Vigogo hao wa ngazi za juu ambao ni wakurugenzi, wamehamishiwa Chuo cha Mafunzo cha Tanesco (TSS) kwa madai kuwa shirika linaboresha ufanisi wake.

Walioshushwa vyeo ni pamoja na Declan Mhaiki aliyekuwa Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia usambazaji wa umeme.

Wengine ni Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji na Huduma kwa Mteja, Mhandisi Sophia Mgonja na Naibu Mkurugenzi Mtendaji Uzalishaji Umeme, Nazir Kachwamba.

Wakati hao wakipitiwa na panga hilo, Mkurugenzi wa Idara ya Rasilimali Watu, Watson Mwakyusa, aliamua kuandika barua kuacha kazi mwenyewe.

Akizungumza na MTANZANIA juzi, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Tito Mwinuka, alisema jana wangetoa taarifa kuhusu hamisha hamisha hiyo.

Jana mchana Idara ya Kitengo cha Mahusiano cha Shirika hilo, kilitoa taarifa na kusema kuwa wataendelea na hatua mbalimbali za mabadiliko ya uongozi kwa lengo la kuongeza ufanisi zaidi wa kiutendaji.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa mabadiliko yanayoendelea ndani ya Tanesco yatawekwa wazi wakati mwafaka kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za shirika kupitia vyombo vya habari.

Kitengo hicho kilieleza kuwa kwa sasa bado wanaendelea na panga pangua na endapo watakamilisha watatoa taarifa kwa umma.

“Tunaomba vyombo vya habari vitoe fursa kwa mamlaka husika kuendelea kukamilisha zoezi hili muhimu kwa maendeleo ya Shirika na Taifa kwa ujumla na taarifa rasmi itatolewa baada ya zoezi kukamilika,’’ ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.

Januari Mosi, mwaka huu, Rais Dk. John Magufuli alimteua Dk. Mwinuka kuwa Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, baada ya kumng’oa aliyekuwa mkurugenzi wa shirika hilo, Mhandisi Felchesmi Mramba.

Mramba alitenguliwa uteuzi wake siku mbili baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), kutangaza kuridhia ombi la Tanesco la kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 8.5 kutoka 18 waliyoomba.

Kabla ya uteuzi huo, Dk. Mwinuka alikuwa Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Akiwa mjini Bukoba kwenye ibada ya Mwaka Mpya, Rais Magufuli alisema amekerwa na kusikitishwa na vitendo vya baadhi ya watumishi wa umma kujitokeza hadharani na kutangaza au kuzungumzia mambo ya kitaifa kama uamuzi wa Serikali bila kushirikisha viongozi wao wa ngazi za juu.

Kutokana na hali hiyo, alisema watendaji hao ni miongoni mwa majipu yanayostahili kutumbuliwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles