29.9 C
Dar es Salaam
Sunday, November 17, 2024

Contact us: [email protected]

MWAKA 2017 UFUFUE MATARAJIO YA WANANCHI

Na ELIZABETH HOMBO


 

maguTANGU Rais Dk. John Magufuli aingie madarakani kipaumbele chake kikubwa kimekuwa ‘kutumbua’ watumishi ambao ni wazembe kazini na baadaye kuteua wengine kujaza nafasi, lengo likiwa ni kujaribu kurudisha nidhamu ya uwajibikaji na dhana kongwe iliyofifia kwamba cheo ni dhamana.

Lakini tayari tumeshuhudia namna hatua hizo zilivyoathiri maisha ya Mtanzania wa kawaida, kutokana na kutokuwa na maandalizi ya kutosha hususani tahadhari ya matokeo ya hatua hizo za ghafla, zilizosababisha kuibuka kwa mdodoro wa uchumi tunaoshuhudia sasa uliokumba si tu sekta mbalimbali lakini pia sehemu kubwa ya wananchi ambao hawana tena uhakika na ustawi wa maisha yao.

Hivi sasa hakuna anayetimiza malengo ya ustawi wake kimaisha ikiwamo kujenga na kuwekeza katika rasilimali binafsi, kwani kinachoonekana kutokea ni kwa waliojilimbikizia fedha siku za nyuma wamezishikilia kwa sababu hawajui mustakabali wao utakavyokuwa, hivyo kuathiri mzunguko kutowafikia wasiokuwa nazo na kuzalisha pengo la matabaka baina ya makundi hayo.

Athari nyingine ni kwamba Serikali imeacha kutumia mabenki ya biashara kitendo kinachoathiri mzunguko wa fedha.

Hatua hiyo si tu inapunguza mgawanyo wa mzunguko wa fedha ambao kwa kawaida hudhibitiwa kwa kupanda na kushuka kwa bei (inflation & diflation), lakini pia inaua uwezo wa kujimudu wa wananchi wa daraja la kati na kusababisha wananchi wa daraja la chini kuteseka zaidi, kwa kuwa tija hutiririka kutoka daraja la juu kupitia la kati hatimaye kuwafikia.

Mtindo huu wa utumbuaji unadhoofisha hata utendaji  kwa wanaohamishwa nafasi zao kabla hawajatimiza mikakati waliyopanga katika nafasi waliyokuwapo awali.

Wanashindwa kutimiza mikakati yao kutokana na uteuzi na utenguzi kila kukicha ikionekana kama kipaumbele cha pili baada ya utumbuaji na hivyo kuzua maswali kwamba ni lini ‘panga pangua’ itakamilika na kujikita katika kuwaletea maendeleo wananchi walioichagua Serikali?

Ni lazima kuwapo ustahamilivu mkubwa na busara katika kutoa hukumu kwa makosa yanayorekebishika, kwani kama awamu zilizopita nazo zingefanya hivyo hata maendeleo tunayoshuhudia yaliyopatikana katika awamu hizo yasingekuwapo. Taswira halisi inajiakisi kwa kutathimini baadhi ya maeneo yafuatayo;

Serikali kupoteza kodi

Kitendo cha wamachinga kuruhusiwa kufanya biashara kokote kunaifanya Serikali ipoteze mapato kwa sababu, sasa wanashirikiana na wenye maduka kwa kuwauzia bidhaa zao kwa biashara ya mabadilishano ya kuaminiana.

Nasema hivyo kwa sababu wafanyabiashara hao wanafahamu kuwa wamachinga wanakopesheka bidhaa kwani hawataporwa kutokana na utetezi wa Serikali kuwa wasiguswe.

Uamuzi kama huo unaashiria uendeshaji wa siasa za hisia, badala ya kutathimini athari.

Kudorora kwa elimu

Sekta nyingine inayoyumba kila mara ni elimu ambayo kwa sasa wasimamizi wake nao wanatekeleza kipaumbele cha kutumbua kwa nguvu kubwa, ikiwamo kutudhihirishia kuwa wasiolipa mikopo ya elimu ndiyo wanaosababisha wengine wasipate mikopo.

Lakini ukweli halisi ni kuwa hata kama wameelimika kwa kiwango kikubwa lakini kama hawatengenezi tija kwa kukosa ajira kutokana na kuwa na uwezo mdogo wa kuajiri sehemu kubwa ya wahitimu, ni dhahiri kuwa anguko la elimu litaendelea si tu kwa kutorejeshwa mikopo bali pia kutokana na kunakili sera za wengine wakati wa kutafuta dhamana ya kuongoza, bila kufanya kazi ya ziada kupanga mikakati ya utekelezaji.

Eneo lingine linalozua maswali ni matokeo ya hatua zinazochukuliwa ili kuleta mabadiliko ‘chanya’ badala ya kufanya mambo kwa mazoea ya kusifia bila kuangalia athari ‘hasi.

Licha ya hotuba kwenye mikutano ya kisiasa majukwaani kujaribu kutuaminisha kuwa uchumi unakua lakini takwimu halisi hazidhihirishi hicho kinachonadiwa, kwani ikiwa pato letu la jumla (GNP) pamoja na pato letu la ndani (GDP) hayakui kwa kukidhi mahitaji kwa kubainisha kiwango cha ukuaji.

Inamaanisha kwamba bado tunaendesha uchumi wetu unaoathiriwa na sera za kisiasa kutokana na ilani ya chama kilichoko madarakani, kwa kubahatisha badala ya kuzingatia weledi kwa kutelekeza vipaumbele thabiti badala ya kukazania vipaumbele vya ‘panga pangua’ ‘tumbua’ na ‘teua na tengua’.

Kwa muktadha huo kutokana na mfumo wa uendeshaji sekta mbalimbali kutegemeana, hivyo kupwaya kwa sekta muhimu lazima kutayumbisha sekta nyingine mtambuka zikiwamo ambazo hazikuwekewa mikakati na kusababisha maamuzi ya kukurupuka, kwa kuwa tu Watanzania kwa sasa wameshazoea kusikiliza wimbo wa kutumbua kila kukicha hivyo kila kiongozi mwenye dhamana asipotumbua anahisi kama hatimizi wajibu.

Mfano mdogo unahusu sekta ya elimu ambapo hivi karibuni tulishuhudia uhamasishaji mkubwa wa kukabiliana na tatizo la ukosefu wa madawati, wito ulioitikiwa na kulipunguza tatizo hilo kama si kulimaliza kabisa lakini hakuna muunganiko wa mafanikio hayo na ajira za kutosha za walimu, watakaowafundisha wanafunzi wanaotarajiwa kufaidika na elimu ya bure lakini inayokosa nyenzo muhimu za kutosha vikiwamo vitabu kutokana na uhaulishaji mtaala kila mara.

Hali hiyo pamoja na uwezo duni wa kiuchumi wa wazazi wengi wenye kipato duni ambao ndiyo daraja la chini lisilopokea tija kutoka daraja la kati linaloyumba, ambao wameshatahadharishwa kuwa wasiowapeleka shule watoto wanaostahili kuandikishwa watachukuliwa hatua stahiki katika kinachoonekana kuwa ni kuwatisha ili watimize hulka ya bora liende.

Lakini licha ya elimu kuwa bure bado kuna mahitaji ya kimsingi wanayopaswa kuyatimiza ili watoto wasome vyema lakini hawana uwezo wa kumudu kutokana na kudorora kwa uchumi binafsi.

Licha ya kipaumbele cha kutumbua lakini bado kuna wasimamizi wasiotimiza ipasavyo majukumu waliyokasimiwa na hivyo kusababisha walio juu yao kimamlaka kusimamia mambo madogo yaliyopaswa kusimamiwa na waliowatuma.

Mifano michache midogo ni suala la Faru John kuvaliwa njuga na Waziri Mkuu, wakati kuna Waziri mwenye dhamana ya utalii na watendaji wengine ambao hawakupaswa kusubiri kuulizwa na mkubwa wao!

Kwanini suala la Dangote hadi limfikie Rais wakati kuna wasimamizi wa sekta inayohusika na uwekezaji, ambao hawakutimiza wajibu waliopaswa ili wakuu wao wajielekeze katika kusimamia mambo mengine makubwa zaidi?

Hiyo ni mifano miwili tu midogo ya namna mnyororo wa uwajibikaji ulivyojaa kutu au umekatika katika baadhi ya maeneo hivyo ukichanganya na hatua mkurupuko unaweza kuanza kuhisi kuwa, kwanini ghafla maisha yamegeuka magumu zaidi tofauti na matumaini yaliyotarajiwa kwa ujio wa awamu ya tano!

Tutarajie nini?

Kwa tathimini hii ni ukweli ulio wazi kuwa yanahitajika mabadiliko ya mwenendo, kwa kuwa muda bado unaruhusu ukizingatia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano ndiyo kwanza imeanza mwaka wa pili wa muhula wa kwanza wa uongozi wa miaka mitano.

Lakini pia tukiwa tumeshavuka nusu ya mwaka wa kifedha wa Serikali ambao huanza Julai hadi Juni ya mwaka mwingine, huku tukijenga matumaini kuwa mwaka mpya wa 2017 ulioanza siku chache zilizopita utafufua matarajio kwa kujipanga vyema kutimiza kilichosubiriwa kwa hamu na wananchi tofauti na hali ilivyo sasa Mwisho.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles