26.9 C
Dar es Salaam
Friday, January 3, 2025

Contact us: info@mtanzania.co.tz

WAKONGWE 7 WANAOMALIZA 2016 KWA HESHIMA

chaz-hillary

Na JOSEPH SHALUWA

MWAKA 2016 umekuwa wenye changamoto nyingi kwenye burudani Bongo. Tumeshuhudia mengi, wengine wakipanda, wengine wakishuka na wapo waliong’ang’ania.

Ilikuwa ngumu kwa wakongwe wa fani mbalimbali kutunisiana misuli na kizazi kipya cha burudani ambacho damu zao bado mbichi.

Baadhi ya wakongwe wameshindwa kutetea heshima zao kutokana na challenge kubwa kutoka kwa mastaa wapya ambao wameingia na ubunifu mpya.

Hapa Swaggaz linakupa msimamo wake juu ya mastaa wa fani mbalimbali Bongo ambao ama walipotea na mwaka huu wamefanikiwa kurejea kwenye game au wameendelea kujenga heshima ndani ya fani wanazotumikia.

 TIDO MHANDO (Mtangazaji)

Huyu ni mkongwe mwingine kwenye utangazaji. Alianzia Radio Tanzania Dar es Salaam (RTD – sasa TBC Taifa), baadaye akaenda kufanya kazi nchini Kenya kwa miaka mingi kabla ya kwenda Ughaibuni na kufanya kazi katika mashiriki makubwa ya habari ya kimataifa.

Tido amewahi kufanya kazi katika Idhaa ya Kiswahili ya Sauti ya Amerika (VoA) na Radio Deutche Welle (DW) ya Ujerumani kisha Idhaa ya Kiswahili – BBC London ambapo mwaka 1999 alipewa cheo cha Mhariri wa Idhaa ya Kiswahili hadi mwaka 2006 aliporejea nchini na kuanza kazi katika Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) kama Mkurugenzi Mtendaji wa shirika hilo, lakini mwaka 2010 alisimamishwa kazi.

Tido alipumzika kwa miaka miwili kabla ya Machi, 2012 kujiunga na Kampuni ya Mwananchi Communication kama Mkurugenzi Mtendaji kabla ya mwishoni mwa mwaka 2014 kutua Azam TV kama Naibu Mkurugenzi Mtendaji, wadhifa anaoutumikia hadi sasa.

Pamoja na kuwa bosi katika kituo hicho, Tido ameendelea kufanya kazi ya utangazaji kwa weledi mkubwa na kujizolea mashabiki lukuki.

Itakumbukwa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, Tido alikuwa akifanya mahojiano na wanasiasa mashuhuri nchini katika Kipindi cha Funguka kilichojizolea umaarufu mkubwa.

Anamaliza mwaka huu akiendelea kuwa kileleni, licha ya ukongwe wake na kuwaacha mbali watangazaji vijana.

CHARLES HILLARY (Mtangazaji)

Historia yake ni ndefu, akiwa mwenye sauti tamu na ya kipekee akisikika nyuma ya kipaza sauti. Hillary alikuwa miongoni mwa watangazaji waasisi wa Radio One Sterio ya jijini Dar es Salaam mwaka 1998.

Amewahi kutangaza vituo vya kimataifa vya Radio Deutsch Welle (Ujerumani) na BBC London (Uingereza) kwa nyakati tofauti akitambaza zaidi kwenye taarifa za habari na hasa za michezo na matangazo ya moja kwa moja ya mpira wa miguu kutoka katika viwanja mbalimbali.

Baada ya kukaa nje ya nchi kwa miaka kadhaa, mwaka jana alirejea nchini na kujiunga na Azam TV ambapo mpaka sasa anafanya vizuri.

 MAULID KITENGE (Mtangazaji)

Mtangazaji huyu si kariba ya akina Tido na Hillary, lakini ana zaidi ya muongo mmoja kwenye fani. Kitenge alidumu Radio One kwa miaka mingi akiwika bila kuchuja katika vipindi mbalimbali vya michezo kwenye redio hiyo na Runinga ya ITV.

Utundu wake wa kucheza na sauti ndiyo unaomfanya aendelee kubaki kileleni miongoni mwa watangazaji wa michezo nchini. Mwaka juzi alijiunga na Radio E FM ya jijini Dar es Salaam baada ya kuamua kuacha kazi Radio One.

Kwa sasa ni gumzo mjini, akiwika katika Kipindi cha Sports Headquarters, kikiwa ni kipindi pekee na cha kwanza cha michezo nchini kuruka asubuhi kuanzia saa 3 – 6 mchana.

Kitenge anamaliza mwaka akiwa kifua mbele na hakuna ubishi kuwa ndiye mtangazaji aliye juu zaidi kwenye vipindi vya michezo Bongo.

MWANA FA (Bongo Fleva)

Hamisi Mwinjuma ni miongoni mwa wakongwe kwenye Bongo Fleva. Alianza miaka ya 2000 akiwika na tungo zake zenye mashairi yenye utata.

Kwa muda mrefu, staa huyu aliyejenga heshima na vibao vyake maarufu kama Mwanafalsafani, Show Time, Bado Niponipo, Asanteni kwa Kuja, Yalaiti, Alikufa kwa Ngoma alikuwa kimya lakini wakati tukielekea ukingoni mwa mwaka huu alifyatua Dume Suruali, kibao kilichomuweka pazuri kwenye ramani ya muziki.

Dume Suruali amemshirikisha  Vanessa Mdee ‘V – Money’ ambaye amefanya kazi siyo ya kitoto ndani ya wimbo huo.

GK (Bongo Fleva)

Anaitwa Gwamaka Kaihula, Rais wa East Coast Team ya Upanga jijini Dar es Salaam. Crew hii ina memba wengine kama Mwana FA, AY, O Ten, Snare, Buff G na wengine kibao kutoka maskani yao Upanga Mashariki.

Baada ya kimya cha muda mrefu, aliibuka na kibao Mzuri Pesa, huku akieleza kuwa ni mwanzo wa ujio wake, wakati huohuo wakijiandaa kufanya kazi mpya kama kundi.

JB (Bongo Muvi)

Jacob Stephen ‘JB’ anatesa kwenye sinema za Kibongo. Huyu ni msanii wa kitambo tangu akiwa kwenye Kundi la Mambo Hayo miaka ya mwishoni mwa 90. JB bado anatesa na amemaliza mwaka kwa heshima kutokana na sinema yake Kalambati Lobo inayofanya vizuri sokoni.

GARDNER (Mtangazaji)

Ni miongoni mwa watangazaji wenye uwezo mkubwa katika vipindi vya jioni. Kwa sasa yupo katika Kipindi cha Jahazi, Radio Clouds FM alipochukuliwa kutoka E FM kwa mkwanja mrefu.

Kabla ya E FM alikuwa Times FM akitokea Clouds FM alipokuwa awali ambapo ndicho kituo chake cha kwanza kuanza utangazaji mwishoni mwa miaka ya 90. Habash amemaliza mwaka kwa heshima, akielezwa kuwa miongoni mwa watangazaji wachache Bongo wanaovuta mkwanja mrefu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
593,000SubscribersSubscribe

Latest Articles