30.2 C
Dar es Salaam
Tuesday, November 26, 2024

Contact us: [email protected]

DK. MPANGO: HAKUNA MDORORO WA UCHUMI

philip-mpango

NA EVANS MAGEGE

MWENENDO wa hali ya uchumi wa nchi umestawi vizuri katika kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka huu kinyume na inavyoelezwa na baadhi ya watu.

Akizungumza wizarani na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, alisema uchumi unasemwa umestawi kupitia vipimo vitatu kama viashiria.

Alivitaja vipimo hivyo kuwa ni kuongezeka, kupungua au kudumaa kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi.

Dk. Mpango alisema tathmini ya vipimo hivyo katika kipindi cha miezi hiyo zinaonyesha uchumi wa nchi kwa ujumla wake umeendelea kukua.

Pia alisema uchambuzi wa tathmini ya vipimo hivyo umefanyika kwa kuangalia viashiria na malengo yaliyowekwa, kuangalia vigezo vinavyokubalika kimataifa au kulinganisha mwenendo wa viashiria vya kiuchumi katika nchi nyingine.

Alitaja kiashiria cha ukuwaji wa Pato la Taifa kwa kutanabaisha kwamba kipindi cha Julai hadi Desemba, mwaka huu takwimu za ukuwaji wa uchumi zinaonyesha kwamba uchumi umeendelea kukuwa na kuifanya Tanzania kuwa miongoni mwa nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara ambazo uchumi wake unakuwa kwa kasi kubwa ya zaidi ya asilimia 7.2.

Kuhusu kiashiria cha mfumuko wa bei  alisema ulipungua kutoka asilimia 6.5 Januari, mwaka huu hadi kufikia asilimia 5.5 Juni, mwaka huu na uliendelea kupungua zaidi hadi kufikia asilimia 4.5 Septemba, mwaka huu na baadaye Novemba, mwaka huu ulipanda na kufikia asilimia 4.8.

“Maana yake ni kuwa bei ya bidhaa na huduma ziliongezeka kwa kasi ndogo zaidi ikilinganishwa na kipindi cha nyuma. Mwenendo huu wa kushuka kwa mfumuko ulichagizwa na kasi ndogo ya ongezeko la bei za chakula nchini, kushuka kwa bei ya petroli katika soko la dunia, utekelezaji madhubuti wa sera za bajeti na fedha na utulivu wa thamani ya shilingi.

“Lakini kupanda kwa mfumuko wa bei kwa Novemba, mwaka huu kulitokana na kupungua kwa upatikanaji wa bidhaa za chakula (mbogamboga, unga wa mahindi na ngano) na mkaa,” alisema.

Alitaja kiashiria kingine ni thamani ya shilingi dhidi ya Dola ya Marekani imeendelea kuimarika na kwa sasa shilingi imekuwa ikibadilishwa kwa kati ya Sh 2,167 hadi Sh 2,199 kwa dola moja.

“Hali hii inatokana na sera thabiti za uchumi na mwenendo mzuri wa urari wa mapato ya fedha za kigeni hasa kutokana na mauzo ya bidhaa za viwandani, utalii na huduma mbalimbali,” alisema.

Pia alitaja kiashiria kingine kuwa ni mwenendo wa sekta ya benki kwa kuwa tathmini ya hali ya benki hapa nchini inaonekana ni imara na salama.

Alisema hali hiyo inatanabaishwa na mitaji na ukwasi ambapo kiwango cha mitaji kikilinganishwa na mali iliyowekezwa ni asilimia 18.60 na kiwango cha chini kinachotakiwa kisheria ni asilimia 12.0.

Hata hivyo, alisema amana za wateja katika benki kwa Desemba, mwaka jana  zilipungua kutoka Sh trilioni 20.73 na kufikia Sh trilioni 20.57 kwa Septemba, mwaka huu.

Alitaja sababu zilizochangia kupungua kwa amana katika benki kuwa ni pamoja na uamuzi wa Serikali kuhamisha sehemu ya fedha za taasisi za mashirika ya umma kutoka benki za biashara kwenda Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Hata hivyo, alisema wazi kuwa amana za Serikali katika benki za biashara ni asilimia tatu tu ya amana zote za benki.

Pia alizitaja benki zilizopata msukosuko  katika kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka huu kuwa ni CRDB na TIB ambazo zilipata hasara.

Alisema hasara hiyo ilisababishwa na tengo kwa ajili ya mikopo chefuchefu, huku Benki ya Twiga ikiwa imewekwa chini ya uangalizi wa BoT.

Alitaja sekta ya nje na akiba ya fedha za kigeni kuwa ni kiashiria kingine cha kukuwa kwa uchumi kwa kuwa hadi kufikia Novemba, mwaka huu nakisi ya urari wa biashara ya bidhaa, huduma na uhamishaji mali nchi za nje ilipungua kwa asilimia 52.5 na kufikia nakisi ya Dola milioni 1,904.2 za Marekani kutoka nakisi ya Dola milioni 4,008.3 za Marekani katika kipindi cha mwaka jana.

“Kupungua huko kulitokana na ongezeko la thamani ya madini hususani dhahabu, bidhaa asilia, mapato yatokanayo na utalii pamoja na kupungua kwa thamani ya bidhaa zilizoagizwa kutoka nje ya nchi hususani bidhaa za mitaji na bidhaa za matumizi ya kawaida.

“Katika kipindi hicho thamani ya bidhaa za huduma zilizouzwa nje ya nchi ziliongezeka kwa asilimia 6.4 na kufikia Dola milioni 8,502.8 za Marekani wakati thamani ya bidhaa za huduma kutoka nje zilipungua kwa asilimia 15.4 na kufikia Dola milioni 9,846.0 za Marekani,” alisema.

Aliongeza kusema kuwa hadi Novemba, mwaka huu, akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dola milioni 4,254.1 za Marekani zilizotosheleza kuagiza bidhaa na huduma kutoka nje ya nchi kwa takribani miezi minne.

Alisema rasilimali za fedha za kigeni za benki zilikuwa kiasi cha Dola milioni 777 za Marekani na kusababisha akiba ya fedha za kigeni kuendelea kuwa ya kuridhisha.

KILIMO CHADUMAA

Dk. Mpango alisema kilimo ni moja ya sekta zenye mchango mkubwa katika Pato la Taifa lakini inakuwa polepole.

Alitanabaisha kuwa kati ya kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka huu sekta hiyo imekuwa kwa asilimia 0.3 kutoka asilimia 2.7 ya Julai hadi Septemba, mwaka jana.

Akifafanua zaidi alisema Julai hadi Septemba, mwaka huu kilichangia kwa asilimia 24.7 huku ujenzi ukichangia kwa asilimia 14.6, biashara kwa asilimia 10.3, viwanda kwa asilimia 7.3 na madini kwa asilimia 5.2.

SEKTA ZINAZOKUWA HARAKA 

Alizitaja sekta zilizokuwa haraka katika uchangiaji wa Pato la Taifa ndani ya kipindi cha Julai hadi Septemba, mwaka huu kuwa ni madini kwa asilimia 19.9, mawasiliano kwa asilimia 14.3, usafirishaji kwa asilimia 12.2, nishati kwa asilimia 11.8 na huduma za fedha kwa asilimia 8.7.

MISAADA NA MIKOPO

Kuhusu misaada na mikopo yenye masharti nafuu, Dk. Mpango, alisema kwa mwaka 2016/2017 washirika wa maendeleo waliahidi kuchangia bajeti ya Serikali kwa kiasi cha Sh trilioni 3.6 na kati ya hizo, misaada ya bajeti ikiwa ni Sh bilioni 483.3.

Alisema mifuko ya kisekta ni Sh bilioni 372.1 na miradi ya maendeleo ni Sh trilioni 2.7.

Pia alisema jumla ya misaada na mikopo nafuu iliyotolewa kwa kipindi cha Julai hadi Novemba, mwaka huu ni Sh bilioni 603.9 sawa na asilimia 21.5 ya lengo la Sh trilioni 2.8.

MWENENDO WA MATUMIZI

Katika hatua nyingine, alitaja mwenendo wa matumizi katika kipindi cha Julai hadi Novemba, mwaka huu na alisema jumla ya Sh trilioni 9.4 zilitolewa na Hazina kwa wizara, idara zinazojitegemea, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa.

DENI LA TAIFA

Kuhusu Deni la Taifa alisema limeendelea kuongezeka na kufikia Dola milioni 21,087.9 za Marekani kwa kipindi cha mwishoni mwa Oktoba, mwaka huu kutoka Dola milioni 19,861.1 za Marekani kwa Desemba, mwaka jana.

Alisema deni la nje liliongezeka kwa asilimia 3.4 na kufika Dola milioni 16, 407.6 za Marekani kwa Oktoba, mwaka huu (sawa na asilimia 77.8 ya deni la Taifa), kutoka Dola milioni 15,863.9 za Marekani kwa Desemba, mwaka jana.

Alisema hali hiyo inatokana na kuongezeka kwa mikopo mipya pamoja na malimbikizo ya malipo ya madeni.

BIASHARA KUFUNGWA

Pia alienda mbali zaidi kwa kuelezea kasi ya wafanyabiashara kufunga biashara zao.

Alisema hali hiyo imeongezeka kati ya Agosti na Oktoba, mwaka huu. Alitolea mfano kwa Jiji la Dar es Salaam katika Wilaya ya Ilala ambako wafanyabiashara 1,076 walifunga biashara zao.

Alitaja wilaya nyingine ni Kinondoni, wafanyabiashara 443 walifunga biashara zao, Temeke wafanyabiashara 222 walifunga biashara zao huku mkoani Arusha wafanyabiashara 131 nao walifunga biashara zao.

Akifafanua zaidi alisema aina ya biashara zilizofungwa kwa wingi ni katika sekta ya ujenzi na biashara ya jumla na rejareja huku chache katika huduma za usafiri.

“Hata hivyo, sababu hasa zilizosababisha biashara hizo kufungwa hazijafahamika kutokana na ugumu wa kupata taarifa kutoka kwa wenye biashara zilizofungwa. Sababu za mtu kufunga biashara yake zinaweza kuwa nyingi, ikiwamo kushindwa kuingiza bidhaa nchini bila kulipa kodi stahiki, kushindwa kulipa au kulipwa madeni, kubadilisha aina ya biashara na kushindwa kusimamia biashara,” alisema.

WATALII

Kuhusu takwimu za wageni walioingia nchini mwaka huu, alisema kwa ujumla idadi ya watalii imeongezeka  ikilinganishwa na mwaka jana.

“Madai kuwa watalii wameikimbia Tanzania kwa sababu ya VAT katika baadhi ya huduma za utalii hayana msingi. Na kama nia ni kutolipa kodi na wakati huo huo Serikali inadai fedha kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya utalii na huduma nyingine kwa wananchi, hilo halikubaliki. Nawaalika wadau wa sekta ya utalii waje wajenge hoja zenye mashiko wakati wa mapitio ya marekebisho ya kodi kwa ajili ya bajeti ya 2017/18,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles