Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM
TIMU ya soka ya Simba imeendelea kutoa dozi katika Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya jana kuichapa Ruvu Shooting bao 1-0 katika mchezo uliopigwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Matokeo ya jana yameendelea kuiimarisha Simba kileleni, ambapo sasa imefanikiwa kufikisha pointi 44 ikiwa ni tofauti ya pointi nne dhidi ya mahasimu wao, Yanga waliojikusanyia pointi 40.
Simba walikuwa wageni wa Ruvu Shooting katika mchezo wa jana, waliingia uwanjani kupambana na kuhakikisha ushindi wa pointi tatu muhimu unapatikana ili waendelee kutamba kileleni na kuzidi kuwaacha Yanga.
Bao pekee la Simba lilifungwa na Mohamed Ibrahim ndani ya dakika tatu za nyongeza kipindi cha kwanza kabla ya mapumziko baada ya kupokea pasi ya Jonas Mkude ambaye aliunganisha krosi iliyopigwa na Shiza Kichuya.
Simba walianza mchezo wa jana kwa kasi ambapo dakika ya tatu winga Pastory Athanas alikosa bao la wazi baada ya kushindwa kuunganisha vyema mpira wa krosi iliyochongwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’.
Dakika ya 30 mshambuliaji wa Ruvu, Full Maganga, alifanya shambulizi kali akiunganisha kona iliyopigwa na Shabani Kisiga, lakini shuti lake lilitoka nje ya lango.
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo dakika ya 64, Maganga aliikosesha timu yake bao baada ya kupiga shuti hafifu akiwa ndani ya eneo la hatari.
Ushindi wa jana ni wa tatu mfululizo kwa Wekundu hao wa Msimbazi tangu kuanza kwa mzunguko wa pili, ambapo awali iliizamisha Ndanda FC ugenini kwa kuwafunga mabao 2-0 kabla ya kuichapa JKT Ruvu bao 1-0.
Ruvu Shooting: Damas Makwaya, Bidii Hussein, Abdul Mpambika, Yusuph Nguya, Renatu Kasase, Baraka Mtuwi, Jabir Aziz/ Shabani Kisiga, Full Maganga, Danas Hussen, Ismail Mohamed/Chande Magonja na Abrahman Mussa.
Simba: Daniel Agyei, Jonas Mkude, Janvier Bukungu/Said Ndemla, Mohamed Hussein, Abdi Banda, Method Mwanjale, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassin, James Kotei, Pastory Athanas na Mohamed Ibrahim/Juma Luizio.