32.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, November 27, 2024

Contact us: [email protected]

Zitto: Chenge afungiwe uongozi wa umma

kabweNa Aziza Masoud, Dar es Salaam
WAKATI Tume ya Maadili ya Utumishi wa Umma ikiendelea na mvutano wa sheria na Mbunge wa Bariadi Magharibi (CCM), Andrew Chenge, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Zitto Kabwe, amesema mbunge huyo alistahili kufungiwa kushiriki kwenye uongozi wa umma muda mrefu.
Zitto aliliambia Mtanzania kuwa tangu izuke kashfa ya rada ambayo pia Chenge alihusishwa, tume ya maadili ilipaswa kumuhoji na kumchukulia hatua kali za sheria.
“Chenge kwa mara ya pili sasa anaonekana kuwa ana makosa ya maadili. Kwenye rada taratibu kama hizi za sasa hazikufanyika. Ilipaswa zifanyike aeleze alipata wapi fedha alizoziita vijisenti, alizoweka huko kwenye visiwa vya Jersey.
Jambo hilo lilipita tu bila Baraza la Maadili kulifanyia kazi, wanachofanya sasa Baraza la Maadili kwenye Escrow ndiyo ilipaswa ifanyike kabla kiasi kwamba Chenge asingekuwa kwenye uongozi wa umma.
Katiba ipo wazi inasema mtu anaweza kupoteza ubunge kwa makosa ya maadili.
Zitto alisema kinachoendelea kwenye baraza hivi sasa ni funzo kubwa na kufumbua macho kwamba mfumo wa kushughulikia maadili upo isipokuwa haukuwezeshwa kufanya kazi.
Sasa tuuwezeshe uweze kushughulika na kesi za utovu wa maadili.
Swali: Ni kipi kilichofanya sasa baraza lichukue hatua?
Jibu: Baraza limeibuka kwa sababu kuna hasira za wananchi kuhusu Escrow. Hasira zilizokitisha Chama cha Mapinduzi kwa kiwango cha kuanza kuchukua hatua.
Hasira hizi hazikuweza kuelekezwa vizuri kwenye kashfa ya rada na kashfa nyingine. Sasa wananchi wanadai viongozi wanaoshutumiwa kwa ukwasi mkubwa tofauti na kipato chao wachunguzwe na waitwe mbele ya baraza kujieleza. Itasaidia kurejesha imani ya wananchi kwa uongozi wa umma.
Mbali na suala hilo, kwenye ukurasa wake wa Facebook, Zitto jana alisema Maadili ya Viongozi wa Umma ni moja ya mjadala mkubwa Uingereza hivi sasa.
“Wabunge waandamizi wawili, Jack Straw na Malcolm Rifkind, wamekutwa na kashfa kubwa ya kutumia ubunge wao kuishawishi kampuni binafsi kuhusu malipo,” alisema.
Alisema wabunge hao wameamua kung’atuka kwa aibu kubwa.
“Suala kama hili linatokea sana Tanzania ambako hakuna kanuni za maadili za wabunge – kuna Azimio la Bunge la mwaka 2004 kutunga kanuni hizi lakini hakuna lililofanyika. Niliwasilisha muswada binafsi kuweka kanuni hizi ukafanyiwa mizengwe.
“Wabunge wa Tanzania kutumia nafasi zao kushawishi kwa maslahi ya makampuni binafsi na kulipwa kwa kazi hiyo ni jambo la kawaida,” alisema.
Alisema kuna mbunge anatumia nafasi yake kutoa matangazo ya biashara kwenye gazeti lake yenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200 kwa mwaka.
“Kuna Mbunge ana gazeti linalotoka wakati wa Bunge la Bajeti tu kwa ajili ya kupata matangazo. Wengine wana zabuni za Bunge.
“Wabunge takribani wote ni wafaidika wa misamaha ya kodi ama kwa mujibu wa stahili zao au kwa kutumia ushawishi wao kupata misamaha ya biashara wanazofanya,” alisema.
Alisema Chama cha Labour cha Uingereza kimeweka katika Ilani yake ya Uchaguzi kwamba wabunge wote wa chama hicho ni marufuku kufanya kazi nyingine wakiwa wabunge na kuwa kikishika madaraka kitatunga sheria kuzuia wabunge kufanya kazi nyingine.
Wiki hii huenda ikawa ngumu kwa Mbunge wa Sengerema, William Ngeleja (CCM), pamoja na watumishi mbalimbali wa Serikali ambao wanatarajiwa kusimama mbele Baraza la Maadili kwa ajili ya kusomewa mashtaka ikiwamo kupokea mgao wa fedha za Akaunti ya Tegeta Escrow.
Februari 23 mwaka huu, alihojiwa Mbunge wa Muleba Kusini, Profesa Anna Tibaijuka (CCM) na uamuzi yunatarajiwa kutolewa Machi 13 mwaka huu.
Hata hivyo, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Andrew Chenge (CCM) aligoma kuhojiwa na baraza hilo na kuamua kukata rufaa Mahakama Kuukwa kupata tafsiri ya neno zuio.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles