Na RAMADHAN HASSAN-DODOMA,
WATU wenye uwezo na uchumi mzuri nchini wanatakiwa kutumia mali zao katika kuwasaida watu wenye mahitaji maalumu ikiwemo watoto yatima ili nao waweze kuishi kama walivyo wengine na kupata elimu nzuri.
Wito huo ulitolewa juzi na Meneja wa Benki ya Diamond Trust Tanzania (DTB) Tawi la Dodoma Athuman Msangi, alipokuwa akikabidhi vyakula na vifaa vya shule kwa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu katika shule ya Zamzam English Medium iliyopo Mtaa wa Miyuji mjini hapa.
“Tulicholeta hapa ni sehemu ya faida ambayo benki huipata kutoka kwa wateja wake na ndiyo maana tunarudisha kwao kupitia njia hii, lakini niwaombe na wengine watambue kuwa, wakati wanakula vizuri na watoto wao, wako wenye mahitaji makubwa hata chakula hawana,” alisema Msangi.
Kwa upande wake Meneja wa shule hiyo, Alhaji Rashid Bura alisema shule hiyo ina mahitaji makubwa hivyo akaomba Watanzania wengine kujitokeza na kuwasaidia ikiwemo chakula na vifaa vingine kama walivyofanya DTB.
“Shule hii ilianza kama kituo cha kuwasaidia watoto yatima na wenye mahitaji maalumu lakini baadaye tulibaini kuna mahitaji makubwa katika kundi la vijana ambao waliachwa mitaani bila elimu.
“Kwa sasa shule hii imesajiliwa na Serikali na tuna wanafunzi 123 ambao wanasomeshwa na taasisi ya Dalai Islamic Center. Wanafunzi hawa huwa tunawapata kupitia viongozi wa mitaa na waumini pale wanapobaini uwepo wa mtoto yatima au anayeishi na wazazi wasiokuwa na uwezo,”alisema Bura.