Na JANETH MUSHI- BABATI
SERIKALI imeombwa kujenga zahanati katika kituo cha kulelea wazee wasiojiweza katika Kata ya Magugu, wilayani Babati, Mkoa wa Manyara.
Ombi hilo lilitolewa hivi karibuni na wazee hao ambao walisema kutokana na eneo hilo kutokuwa na zahanati wamekuwa wakilazimika kutembea umbali mrefu kufuata huduma za afya.
Mmoja wa wazee hao, Joseph Apolinary, alisema licha ya ukosefu wa zahanati katika kituo hicho, pia kituo chao hakina gari la kubeba wagonjwa, jambo linalowalazimu kutumia gharama kubwa kukodisha usafiri ikiwamo kupanda pikipiki pindi wanapohitaji huduma za afya.
“Tunaiomba Serikali ijenge zahanati kituoni hapa au karibu na eneo hili ili tunapohitaji huduma ya afya tuipate kwa wakati.
“Pia tunaomba gari la wagonjwa kwani kutokuwapo kwa gari hilo, kunatulazimu wakati mwingine kupanda pikipiki ingawa umri wetu hauruhusu kabisa kupanda pikipiki,” alisema Aporinary.
Naye mkuu wa kituo hicho kiitwacho Makao, Samson Munuo, alisema wamekuwa wakitembelewa kituoni hapo mara moja kwa wiki na madaktari ila wakati mwingine inapotokea dharura wakati wa usiku, wanapata shida kutokana na kukosekana kwa usafiri.
“Tunatembelewa na madaktari mara moja kwa wiki ila umbali wa kituo cha afya umekuwa changamoto hasa nyakati za usiku kunapotokea mgonjwa.