NA MWANDISHI WETU,
RAIS Dk. John Magufuli anauma na kupuliza. Ndivyo unavyoweza kutafsiri mwenendo wa uamuzi wake wa kutengua uteuzi watendaji mbalimbali serikalini na baadaye kuwapa baadhi yao nafasi nyingine za uongozi.
Tangu alipoapishwa Novemba 5, mwaka jana, tayari Serikali yake ya awamu ya tano imewatumbua watendaji zaidi ya 300, wakiwamo watumishi wa taasisi mbalimbali za Serikali na wajumbe wa bodi ambazo zimevunjwa.
Baadhi ya watumishi waliwajibishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, huku wengine wakichukuliwa hatua na mawaziri.
Rais Magufuli hakuishia serikalini tu, akiwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pia ameanza kukisafisha chama hicho kwa lengo la kufanya mabadiliko makubwa.
NDANI YA SERIKALI
Kwa upande wa watendaji serikalini, wapo baadhi aliotengua uteuzi wao na kuwaahidi kuwapangia kazi nyingine na wengine pasipo kuwaahidi chochote, wakiwamo wale aliowatumbua kwa makosa mbalimbali ya uzembe na ubadhirifu.
Pamoja na kuwatumbua watendaji hao kwa nyakati tofauti, Rais Magufuli ameamua kuwarudisha mmoja baada ya mwingine kwa muda wake ili kutumikia nafasi nyingine za utumishi wa umma.
Mmoja wa watendaji wa Serikali waliokumbwa na machungu ya kutenguliwa kabla ya kupozwa ni Profesa Yunus Mgaya aliyekuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU).
Profesa Mgaya alirejeshwa kundini wiki iliyopita kwa kuteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Tiba na Magonjwa ya Binadamu (NIMR) akichukua nafasi ya Dk. Mwele Malecela ambaye Rais Magufuli alitengua uteuzi wake.
Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa akitoa taarifa za kutumbuliwa watendaji mbalimbali serikalini, naye alionja machungu baada ya mapema mwaka huu Rais Magufuli kutengua uteuzi wake katika nafasi yake ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Lakini baada ya miezi kadhaa kupita, Rais Magufuli aliamua kumpoza kwa kumteua kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Diplomasia.
Rais Magufuli alifanya uamuzi kama huo kwa aliyekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Dk. Ramadhan Dau.
Dk. Dau aliyetumikia nafasi hiyo kwa takriban miaka 19, aliondolewa katika nafasi hiyo mapema mwaka huu kabla
miezi michache baadaye kuteuliwa kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malaysia.
Mwingine ni Diwani Athuman aliyekuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), ambaye alitenguliwa uteuzi wake na Rais Magufuli.
Lakini maumivu hayo yalipozwa ndani ya wiki chache tu baada ya kuteuliwa kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.
Sylvester Ambokile ambaye Rais Magufuli alitengua wadhifa wake wa Kamishna Mkuu wa Uhamiaji, naye amepozwa kwa kuteuliwa kuwa balozi.
Pia Balozi Peter Kallaghe aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, naye nafasi yake ilitenguliwa na Rais Magufuli mwanzoni mwa mwaka huu, lakini hivi karibuni alimpoza kwa kumteua tena kuwa Ofisa Mwandamizi Mwelekezi–Mambo ya Nje katika Chuo cha Taifa cha Ulinzi (NDC).
Ado Mapunda ni miongoni mwa watendaji wa Serikali walioumwa na Rais Magufuli na kisha kupulizwa.
Awali Mapunda alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, lakini akajikuta akiwa mmoja kati ya makatibu tawala 10 walioachwa katika uteuzi mpya wa Rais Magufuli alioufanya Aprili mwaka huu, akiahidiwa kupangiwa kazi nyingine.
Septemba mwaka huu, Mapunda alijikuta akiteuliwa tena kushika nafasi hiyo, lakini safari hii akipelekwa Mkoa wa Mara kuchukua nafasi iliyoachwa wazi na Benedict ole Kuyan ambaye amestaafu.
NDANI YA CHAMA
Duru za siasa zinasema, uamuzi wa Rais Magufuli kumwondoa Rajabu Luhwavi katika nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara na kumteua kuwa balozi, ni kiashiria kimojawapo kinachojenga taswira ya uamuzi wake wa kuuma na kupuliza.
Pia duru hizo zinasema uamuzi wake wa kuwateua wajumbe wa Kamati Kuu ya CCM kama Dk. Pindi Chana na Dk. Emmanuel Nchimbi kuwa mabalozi, kunajenga tafsiri nyingine ya mtazamo huo wa kuuma na kupuliza.
Ni wazi kuwa kupitia uteuzi huo, kwa namna moja au nyingine kunaleta ugumu kwa makada hao kuhudhuria vikao vya uamuzi ndani ya CCM.
Pia uamuzi wa Rais Magufuli kumteua aliyekuwa Msemaji wa CCM, Christopher ole Sendeka kuwa Mkuu wa Mkoa wa Njombe, unachukuliwa kama sehemu ya tafsiri ya uamuzi huo huo wa kung’ata na kupuliza.
MAONI YA WASOMI
Mtazamo wa maamuzi ya Rais Magufuli ya kuuma na kupuliza kwa maana ya kutengua na kuwarudisha baadhi ya watendaji wa taasisi za umma, umewavuta wasomi na wataalamu wa sayansi ya siasa, ambao kwa nyakati tofauti wametoa maoni yao.
Akizungumza na MTANZANIA Jumapili jana, Mwalimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashiru Ally, alisema katiba na historia ya nchi zinaipa mamlaka makubwa taasisi ya urais.
“Huyu ni rais wa tano tangu tumepata uhuru kwa upande wa Jamhuri ya Muungano… nguvu hizo hizo na mamlaka hayo hayo yametumiwa na marais wote waliopita, hakuna rais ambaye hakufukuza na kurudisha, hakuna rais ambaye hakuhamisha, hakuna ambaye hakutumbua na hakuna jambo lolote jipya ambalo analifanya Magufuli ambalo halikufanywa na Nyerere.
“Zinaweza kuwapo tofauti za kimtazamo na mwelekeo au kwa mtindo na itikadi na falsafa, lakini linapokuja suala la kufukuza, kuteua, kupandisha vyeo au kushusha vyeo, marais wote watano wamefanya hivyo.
“Kwahiyo mtu anayetaka kutumia historia ya nchi, taasisi za kikatiba, sheria na mamlaka yaliyopo kwenye hiyo taasisi ya urais, hakuna jambo lolote ambalo amelifanya Magufuli halikufanywa na Nyerere, Mwinyi, Mkapa au Kikwete,” alisema Bashiru.
Naye Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Mwesiga Baregu, alisema hatua zinazochukuliwa ni nzito, lakini hazina maandalizi au umakini katika kufanya uamuzi mkubwa wa kutengua na kuteua.
Alisema hali hiyo inazalisha tatizo kubwa katika utumishi wa umma na katika uchumi wa nchi, kwa sababu hali hiyo ni sawa na kujenga mazingira ya sintofahamu ambayo kwa vyovyote yanaathiri utendaji na tija ya utekelezaji, ufuatiliaji na uwajibikaji wa shughuli za umma.
“Kwa mtazamo wangu, hilo ni tatizo kubwa kwa sababu uamuzi huo unatetemesha hali ya utendaji katika Serikali. Pia nadhani hata hii tumbua tumbua ambayo msingi wake haueleweki, mara nyingi Watanzania wamekuwa wanatangaziwa tu fulani katumbuliwa, fulani katumbuliwa, lakini haionekani wazi wazi ni sababu gani, kama ni mtu mzembe au katumbuliwa kwa sababu ya ufisadi.
“Mara nyingi hii haiwekwi wazi kama mtu katumbuliwa kwa sababu gani na amepewa nafasi ya kujitetea akashindwa kujitetea au kaonekana anakwenda kinyume na matakwa ya rais.
“Hii inatakiwa iwekwe wazi ili watu kwenye utumishi wa umma waweze kujifunza na kuepuka madhambi waliyoyafanya wenzao. Lakini bila kuwa na uwazi ni vigumu kwa wengine kujua kwamba jambo fulani ni kosa ambalo linafanya utumbuliwe,” alisema.
Aliongeza kuwa uamuzi wa rais wenye tafsiri ya kuuma na kupuliza, unatoa mtazamo kuwa anauma bila kutenda haki, hivyo inambidi arudi nyuma apulize jeraha.