BARA la Afrika linaelezwa kuwa moja ya maeneo yanayoongoza kuwa na ajali nyingi zaidi duniani kutokana na sababu mbalimbali hasa uzembe pamoja na ubovu wa miundombinu yake ya barabara.
Karibu watu milioni 1.3 hufa kila mwaka kutokana na ajali za barabarani na kutokana na sababu kama hizo.
Kwa sababu hizo, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilitangaza kuwa kipindi cha miaka 10 kuanzia 2011 hadi 2021, kuwa mwongo wa vitendo kwa ajili ya usalama barabarani.
Katika kukabili ajali hizo, pamoja na mambo mengine, inahimizwa uendeshaji mzuri na kuhakikisha hakuna kilevi kilichotumika kabla ya kukaa nyuma ya usukani na kadhalika.
Ni kwa vile nyingi ya ajali hizo huweza kuzuilika kwa uendeshaji mzuri na kufuata sheria nyingine za usalama barabarani.
Hata hivyo, kuna baadhi ya barabara ambazo hata uwe dereva mzuri kiasi gani, ufuate sheria kiasi gani, unaweza bado ukasababisha ajali kama kawa!.
Kwamba katika mazingira ya barabara kama hizi, ajali mara nyingi haziepukiki kwa madereva watumiao vyombo moto.
Kwa sababu hiyo, hufanya maeneo hayo kuwa kipimo kwa madereva kuhusu utaalamu wao na kadhalika kuhusu ujasiri wao wa kupita katika maeneo kama hayo.
Kama utadhani maeneo haya hatari ni sawa na Kitonga, kule mkoani Iringa, yaani hapa kwetu Tanzania, utakuwa umechemsha kwa vile barabara hiyo hatarishi iliyopo eneo katika mlima Kitongo haifui dafu kwa hizi lengwa katika makala haya.
Hizi ni barabara, ambazo dereva akifanya kosa japo dogo tu, tayari ameua, kujimaliza mwenyewe, gari na roho alizobeba garini humo.
Naam, ni barabara ambazo miundombinu yake inasababisha kiwango kikubwa cha ajali duniani, ijapokuwa nyingi hazipo Afrika bali mabara mengine hususani Asia, Amerika na Ulaya.
Picha zifuatazo zinaonesha miongoni mwa barabara hatari zaidi duniani, ambazo pamoja na uhatarishi wake unaosababisha ziwe na kiwango kikubwa cha vifo duniani, wakazi wa maeneo zilipo hawana jinsi ya kuziepuka kwa sababu ndizo wanazozitegemea katika shughuli zao za kila siku kimaisha.