28.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

MATUKIO YALIYOBAMBA 2016 KWENYE BURUDANI

diamond

NA FESTO POLEA,

MWAKA huu umeonekana kuwa funzo kubwa kwa wasanii nchini baada ya waliokuwa wakitumia dawa za kulevya kuachana na utumwa huo na kurudi katika kazi zao za sanaa.

Waliojitangaza kuwa walikuwa watumwa wa dawa hizo na wameamua kupata matibabu ya kuachana nazo ni pamoja na Rehema Chalamila ‘Ray C’ ama kiuno bila mfupa kama wengi walivyopenda kumwita.

Wengine ni Rashidi Makwiro (Chid Benz) na Rehema Chalamila ‘Ray C’ ambao wote baada ya kuwa katika hali mbaya ya matumizi ya dawa hizo walipelekwa kituo cha Life and Hope & Rehabilitation Centre (Sober House) kilichopo Bagamoyo kwa ajili ya kusaidiwa kuachana na matumizi ya dawa hizo.

Ray C ni mara ya pili kusaidiwa kuachana na dawa hizo lakini mwaka huu alionekana kupitia video iliyosambaa kwenye mitandao ya jamii ikimuonyesha akisaidiwa na polisi baada ya kudaiwa kutaka kujichoma kisu.

Wasanii wengine walioachana na dawa hizo kwa mwaka huu ni aliyewahi kutamba na wimbo wa ‘Kazi ya dukani’ uliopo katika mahadhi ya mchiriku wimbo ambao ulimpa tuzo ya Muziki Bora wa Asili mwaka 2009, Mfaume Selemani ‘Dogo Mfaume’ na mwaka huo huo kuanza kuwa mtumwa wa dawa hizo lakini sasa anaishi kituo cha kuzuia matumizi ya dawa hizo cha Pillimissana Foundation kilichopo Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Wengine ni Abubakar Katwila (Q Chillah) na David Genzi (Young D), kwao haikuwa rahisi kuachana na dawa hizo kwa kuwa hawakuwa wakiaminiwa kama wameacha, lakini utumwa, dharau na lawama nyingi walizokuwa wakizipata kutoka kwa watu mbalimbali wakiwemo mashabiki wao ziliwaumiza wakaamua kutangaza kuachana na matumizi ya dawa hizo na sasa wanaendelea vizuri na shughuli za muziki huku Young D akiwa na mtoto wa kike aliyemzaa na mpenzi wake Mamisa.

Ushindani

Muziki wa Bongo Fleva umekuwa na ushindani mkubwa kwa mwaka huu huku ukiongezwa hamasa na mafahari wawili katika muziki huo, Ali Kiba na Diamond kiasi kwamba wamekuwa mfano wa kuzungumziwa katika mabaya na mazuri kuhusu muziki huo.

Ushindani wao umekuwa gumzo kwa wadau wa muziki huo na wamekuwa wakizungumzwa sana kwa mwaka huu kwamba ndio wasanii wenye ushindani mkubwa kimuziki.

Tuzo yarudishwa

Lilikuwa tukio la aina yake kwani siku chache baada ya staa wa muziki Nigeria, Wizkid kutangazwa kuwa msanii bora wa kiume ‘Best African Act’ kwenye tuzo ya MTV Europe Music Award 2016, wapiga kura wakapinga tuzo hiyo kwenda kwa mwanamuziki huyo na waandaaji wakakubali kwamba walifanya makosa ya kiufundi hivyo tuzo hiyo ikachukuliwa kwa Wizkid na kupewa aliyeshinda kwa kura, Ali Kiba wa Tanzania.

Singeli

Mapinduzi makubwa ya muziki wa Singeli kutoka kuchezwa Uswahilini hadi redioni yamesaidia kuutangaza vyema muziki huo kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana wengi nchini hadi kujumuishwa katika tuzo za wasanii ambapo kwa mwaka huu Man Fongo ameshinda tuzo ya msanii bora chipukizi kupitia tuzo za EATV.

DC, mbunge watoa wimbo

‘Niache nisome’ ndio wimbo wenye video inayoelezea umuhimu wa elimu kwa Jimbo la Pangani. Wimbo huo umekuwa wa mfano kwa viongozi na watu mbalimbali kuonyesha vipaji vyao kama Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Zainabu Abdallah na mbunge wa jimbo hilo, Jumaa Aweso, kuimba wimbo huo.

Darasa na Muziki

Rapa Sharif Ramadhani ‘Darasa’ licha ya kupata ajali hivi karibuni huko Ntobo, Wilaya ya Kahama, ndiye mwanamuziki anayemaliza mwaka kwa wimbo wake wa ‘Muziki’ aliomshirikisha msanii mwenzake, Bernard Paul ‘Ben Pol’ kuwa na mashabiki wengi huku wengine wakijikuta wakifikishwa mahakamani kutokana na kukiuka sheria za barabarani.

Dereva mmoja mkoani Singida alikamatwa na polisi na kufikishwa mahakamani kwa kuachia usukani huku akicheza wimbo huo akiwa na wenzake wanne kitendo kilichoelezwa kuwa ni hatari kwa usalama wa maisha ya mali na watu wake.

Wimbo huo unachezwa sehemu mbalimbali zikiwemo kwenye sherehe za harusi.

Chura wa Snura afungiwa

Mei mwaka huu ulikuwa mbaya na mzuri kwa msanii, Snura Mushi, kuachia wimbo wake wa ‘Chura’ kwenye You Tube lakini Serikali iliupiga marufuku wimbo huo kuchezwa katika runinga, pia waliagiza utolewe kwenye You Tube kwa kukiuka maadili ya Mtanzania kwa kuchezesha watu wakiwa nusu utupu.

Baada ya kufungiwa wimbo huo ulizidi kujizolea umaarufu kwa wasiouona waliusaka ili wauone jambo ambalo lilimwongezea shoo msanii huyo katika mikoa mbalimbali Bara na Visiwani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles