32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

CORD, JUBILEE WAGEUZA BUNGE UKUMBI WA MASUMBWI

kenyan-parliament-getty

NAIROBI, KENYA

WABUNGE wa muungano tawala wa Jubilee na ule wa upinzani wa Cord, wamekabiliana kiasi cha kurushiana makonde bungeni walipopingana kuhusu pendekezo la kuifanyia marekebisho sheria ya uchaguzi.

Dakika chache baada ya kikao maalumu kuanza jana chini ya ulinzi mkali, wabunge wa Cord waliondoka bungeni kwa hasira wakidai kukandamizwa na wenzao wa Jubilee.

Wakiongozwa na Naibu Kiongozi wa Wachache Bungeni, Jakoyo Midiwo, wabunge hao walidai wenzao wa Jubilee walikuwa wamejihami kwa bunduki na silaha butu ambazo walitumia kuwapiga.

“Leo (jana) wabunge wa Jubilee waliruhusiwa kuingia ukumbini wakiwa wamejihami kwa bunduki na silaha nyingine hatari, walizoagizwa wazitumie kutushambulia. Wenzetu Ishrad Sumra, Glady Wanga, James Nyikal ni miongoni mwa waliopigwa na kujeruhiwa na wahuni wa Jubilee,” alisema.

Huku akiwaonyesha wanahabari majeraha usoni, Sumra alidai Mbunge wa Tigania Mashariki, Mpuru Aburi kwa ushirikiano na wenzake walimshambulia kwa ngumi na mateke.

“Niliposogea karibu na Aburu kumuuliza ni kwanini alikuwa akimpiga Wanga na kumtemea mate, alinigeukia na kunitwanga makonde. Wenzake ambao sikuweza kuwatambua pia waliungana naye kunishambulia,” alisema mbunge huyo anayewakilisha Embakasi Kusini kupitia Chama cha ODM.

Gladys Wanga ambaye ni Mbunge Mwakilishi wa Wanawake wa Homa Bay, pia alidai kupigwa kifuani, sehemu ya makalio na Aburi na kutemewa mate.

“Ni aibu kwa mbunge mwanamume kumshambulia mwenzake wa kike. Nawaambia Jubilee kwamba hatutishwi na mbinu hiyo ya kutunyamazisha ili wapitishe sheria mbaya na hatimaye waweze kuiba kura mwaka 2017,” alisema.

Wabunge wa Jubilee pia walidai kushambuliwa na wenzao wa Cord.

Wakiongozwa na Kiongozi wa Wengi, Aden Duale, walidai Midiwo alimshambulia na kumjeruhi Aburi.

“Tungependa kufafanua kuwa japo wabunge wana kinga dhidi ya kushtakiwa kwa kutekeleza maovu ndani ya majengo ya Bunge, kinga hiyo si kamili. Ningependa kutangaza hapa kwamba tutamshtaki Midiwo, ambaye alimshambulia Aburi,” alisema Duale, huku akiwaonyesha wanahabari majeraha kwenye shavu la Aburi.

Wakati huo huo, upinzani umeitisha maandamano makubwa Januari 4 mwakani, kupinga sheria za uchaguzi zilizopitishwa na Muungano wa Jubilee.

Vinara wa Cord, Moses Wetang’ula, Kalonzo Musyoka na Raila Odinga, pia waliituhumu Jubilee kwa kukwamisha haki.

Hatua hiyo inakuja baada ya wabunge wa Jubilee kutumia faida ya wingi wao bungeni kupitisha sheria za uchaguzi, licha ya upinzani mkali kutoka Cord.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles