MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, ametangaza kutiwa mbaroni kwa watuhumiwa wanaodaiwa kumteka mtoto Pendo Emmanuel (4) ambaye ni mlemavu wa ngozi (albino).
Mulongo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, amesema watu hao wanahusishwa na tukio la kutekwa kwa mtoto Pendo katika Kijiji cha Ndami wilayani Kwimba mkoani hapa.
Akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Mwanza baada ya kumwapisha Mkuu mpya wa Wilaya ya Kwimba, Pili Moshi, ambapo alisema licha ya kutiwa mbaroni kwa watu hao na Jeshi la Polisi, lakini hadi sasa bado haijajulikana alipo mtoto huyo, huku juhudi za kumsaka zikiendelea.
Katika hafla hiyo, Katibu wa Chama cha Albino Mkoa wa Mwanza, Tuju Mashaka, aliwasilisha kilio chake na kuilalamikia Serikali kushindwa kutokomeza mauaji dhidi ya watu wenye ulemavu wa ngozi nchini kwa kipindi cha miaka tisa sasa.
“Mpaka sasa albino 19 wameuawa Kwimba na kwa Tanzania nzima wameuawa 75 ambao ni sawa na asilimia 0.7 ya albino wote 100,000. Wangekuwa wameuawa watu wengine basi wangeuawa 34,200… mauaji yanapuuzwa kutokana na uchache wetu,” alisema Mashaka.
Baada ya kauli hiyo, ilimlazimu Mulongo kueleza namna Jeshi la Polisi lilivyowanasa watu hao ambao hata hivyo hakutaja idadi yao.
Mulongo alisema waliokamatwa ni waliohusika kumteka, kumsafirisha na kumhifadhi hotelini motto huyo, na kwamba bado msako unaendelea dhidi ya watuhumiwa wa mwisho ili waweze kufikishwa katika vyombo vya sheria ikiwamo mahakama.
“Kila aliyehusika kumteka mtoto Pendo amekamatwa, na baada ya kuchukuliwa kutoka kwa wazazi wake alipelekwa hotelini akawa amefichwa hapo, waliohusika na kumfikisha hapo wamekamatwa pamoja na uongozi wa hoteli hiyo, ikiwa ni pamoja na wale wote waliohusika kumhudumia akiwa hapo.
“Hata hivyo, hatuwezi kutaja majina ya watuhumiwa kwani kufanya hivyo kunaweza kuharibu uchunguzi wa tukio zima ambao unaendelea vema,” alisema Mulongo.
Mtoto Pendo Emmanuel alitekwa Desemba 27, mwaka jana baada ya watu wasiofahamika kuvunja nyumba na kutoweka naye kusikojulikana.
Kwa mujibu wa takwimu, inaelezwa kuanzia mwaka 2006 albino 74 wameuawa kikatili, huku 56 wakinusurika kifo na kati yao 11 wamepata ulemavu mwingine wa kudumu.
Chama cha Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Geita (SHIVYAWATA), kimelaani vikali vitendo vya ukatili wanavyofanyiwa walemavu wakiwamo albino, na kuiomba Serikali kuwawezesha ili waondokane na umaskini wa kipato.
Katika hatua nyingine, Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini Mkoa wa Mwanza, imeanza kuhamasisha viongozi wa siasa na wanasiasa kushiriki kukomesha mauaji hayo.
Kutokana na hali hiyo, iliazimiwa kufanyika kongamano la amani la kupiga vita mauaji ya albino na kuliombea taifa Februari 28, katika Uwanja wa Furahisha.