26.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Mwanafunzi aua mwenzake darasani wakigombea daftari

Na Kadama Malunde, Shinyanga

MWANAFUNZI wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Ilola, Wilaya ya Shinyanga Vijijini, Mkoa wa Shinyanga, Veronica Venance (12), amefariki dunia baada ya kupigwa na mwanafunzi mwenzake wakati wakigombea daftari darasani.
Tukio hilo limetokea juzi mchana wakati wanafunzi hao wakiwa darasani wakiendelea na masomo.
Akizungumza na MTANZANIA jana kuhusu tukio hilo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Ilola, Mahona Joseph, alidai lilitokea wakati Veronoca alipong’ang’ania daftari alilokuwa ameazima kwa mwenzake Sophia Mathew (12) kwa ajili ya kunakili masomo waliyofundishwa.
“Kitendo cha kung’ang’ania daftari hilo wakati si mali yake kilimkera mwenzake na kuzua ugomvi kati yao, hivyo wakati wakinyang’anyana ndipo Sophia alipoanza kumshambulia mwenzake kwa kumpiga makofi na ngumi sehemu za kichwani hali iliyosababishia kifo chake,” alisema Joseph.
Akizungumzia tukio hilo, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Magere Jonas, alisema kifo cha mwanafunzi huyo kilitokea wakati wakigombana darasani ambapo kati ya wanafunzi hao mmoja aliangushwa chini na kugonga eneo la kisogoni.
“Ilikuwa muda wa wanafunzi kupata chakula cha mchana, ambapo wengine wakiwa bado wapo shuleni na hakukuwa na mwalimu hata mmoja, ila mimi na mwalimu mkuu msaidizi tulikuwa chini ya mti tunapunga upepo.
“Tukiwa tunaendelea na mazungumzo ghafla alikuja mwanafunzi mmoja na kutueleza kuna wanafunzi wanagombana darasani, ndipo tukaenda na kumkuta Veronica amelala chali darasani. Baada ya kuona hali hiyo tulimchukua na kumkimbiza zahanati ya Ilola ambako walituambia tumpeleke kituo cha afya Bugisi kwa matibabu zaidi.
“Hata hivyo hali ya mwanafunzi huyo ilizidi kubadilika na kuwa mbaya na tulipofika Bugisi tukaambiwa tayari ameshafariki dunia, tunahisi pengine aliumia kichwani,” alisema Mwalimu Jonas.
Kutokana na tukio hilo, MTANZANIA ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Longinus Tibishubwamu, ambapo alithibitisha kutokea kwa kifo hicho.
“Ni kweli kimetokea kifo cha mwanafunzi Veronica. Baada ya kupata taarifa hizo tulifika katika eno la tukio. Wakati uchunguzi wa suala hili ukiendelea, Jeshi la Polisi tunamshikilia mwanafunzi Sophia Mathew kwa mahojiano zaidi.
“Tukio hilo limetokea Februari 24, mwaka huu saa 7 mchana wakati wanafunzi hao wakiwa darasani kwao wakiendelea na masomo,” alisema Kamanda Tibishubwamu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles