Na Amina Omani, Handeni
WASICHANA 160 wa jamii ya wafugaji wa kabila la Wamasai, wamenusurika kufanyiwa ukeketaji na badala yake wamefanyiwa tohara mbadala.
Wasichana hao wanaoishi Kata ya Kang’ata wilayani Handeni mkoani Tanga, wamenusurika kufanyiwa mila hiyo, baada ya kupata elimu kupitia mradi wa Kijana wa Leo unaotekelezwa na Shirika la Utafiti wa Tiba na Afya barani Afrika (AMREF).
Akizungumza wakati wa sherehe za kuvuka rika kwa jamii hiyo, Meneja Mradi wa Kijana Leo, Dk. Aisha Byanaku, alisema elimu kuhusu madhara ya ukeketaji waliyotoa eneo hilo imesaidia kuwakomboa wasichana hao.
“Lengo la mradi ni kuhakikisha tunawakomboa wasichana wa jamii ya wafugaji, maana tunaamini wengi wao hawana elimu hii kabisa, tumejipanga kuwasaidia kwa nguvu zetu zote,” alisema Dk. Byanaku.
Alisema mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu katika wilaya hiyo, umelenga kuwakomboa wasichana 500.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Handeni, Noeli Abel, alisema mimba za utotoni na ukosefu wa taarifa sahihi za elimu ya ujinsia kwa vijana, ni sehemu ya changamoto kubwa zinazowakabili.
Alisema changamoto hizo zinachangia kwa kiasi kikubwa kusababisha vijana wengi kushindwa kufikia malengo ya maendeleo waliyojiwekea.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi wa AMREF- Tanzania, Dk. Pius Chaya, alisema wamejikita kupunguza na kutokomeza mila hatarithi za ukeketaji, hususani katika jamii za pembezoni.
Alisema elimu ya afya na ujinsia wanayotoa inawasaidia vijana wenyewe kujitambua na kuelewa madhara ya ukeketaji na siku zijazo wawe mabalozi.