27.5 C
Dar es Salaam
Monday, October 2, 2023

Contact us: [email protected]

MIGOGORO MAHALA PA KAZI YAITISHA CMA

shanes-nungu

Na NORA DAMIAN

-DAR ES SALAAM

KUONGEZEKA kwa migogoro mahala pa kazi, kumeitisha Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA) iliyoamua kuviita vyama vya wafanyakazi kujadili namna ya kuipunguza.

Mkoa wa Dar es Salaam ndio unaongoza kuwa na migogoro mingi, ukifuatiwa na Mwanza na Arusha.

Katika mwaka wa fedha wa 2016/17, tume hiyo ilikadiria kusajili migogoro 15,000, lakini katika robo ya kwanza imesajili migogoro 5,163, takwimu ambazo zinaashiria kutakuwa na ongezeko kubwa.

Vyama vilivyoitwa ni Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Fedha, Viwanda, Biashara, Huduma na Ushauri (TUICO), Chama cha Wafanyakazi wa Sekta ya Mawasiliano na Uchukuzi (Cotwu-T), Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (Talgwu), Chama cha Wafanyakazi wa Migodini, Ujenzi na Nishati (Tamico), Chama cha Wafanyakazi wa Reli (Trawu), Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (Raawu) na Chama cha Mabaharia (Tasu).

Akizungumza juzi na makatibu wa vyama vya wafanyakazi Mkoa wa Dar es Salaam, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Shanes Nungu, alisema migogoro mingi inatokana na kuachishwa kazi kinyume cha sheria.

“Migogoro, migomo na malalamiko sehemu za kazi vinazorotesha sana uzalishaji na utoaji huduma bora, hali hii haitasaidia hata kidogo kuimarisha uchumi wa viwanda kwani muda mwingi utatumika kushughulikia migogoro badala ya kufanya kazi,” alisema Nungu.

Alisema sekta ya ujenzi ndiyo inaongoza kwa kuwa na migogoro 253, ulinzi binafsi 229, usafirishaji 191, hoteli 161 na viwanda 122.

Nungu alisema wamejipanga kusuluhisha na kuamua migogoro ya kikazi kwa wakati, na kwamba hatua ya usuluhishi shauri linaweza kumalizika kati ya siku moja hadi 30, wakati hukumu hutolewa ndani ya siku 30 tofauti na ilivyokuwa awali, shauri lilichukua mwaka mmoja hadi 10 kumalizika.

Naye Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Dar es Salaam, Mussa Mwakalinga, aliwataka waajiri wafuate taratibu na kanuni za utendaji bora wa kazi ambazo zinafafanua taratibu za kuachisha kazi kwa usahihi.

Kwa upande wake, Katibu wa Tawi la Tamico katika Kampuni ya Bam International, Juma Hussein, alisema kuna makampuni mengi hayajasajiliwa yanayofanya kazi kiujanjaujanja hatua inayochangia kuwapo kwa migogoro mingi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,770FollowersFollow
575,000SubscribersSubscribe

Latest Articles