KILA kinachoangaziwa na mwanga duniani lazima kiwe na kivuli ambacho huakisi umbile lake kutokana na mwelekeo unakotoka mwanga unaokimulika.
Kisayansi kuna aina tatu kuu za vivuli, kilichokoza (Umbra) cha pembeni kilichofifia kiasi (Penumbra) na cha pembezoni kabisa kwenye ukingo wa kivuli (Antumbra).
Sitafakari kuhusu muundo wa aina ya vivuli bali kuna muktadha sanjari kwa mada ninayodhamiria kuidadavua, iliyosababisha tafakuri yangu itopee katika fikra ya tukio kubwa la chama tawala (CCM).
 Kabla sijatopea kwenye Kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho iliyoketi hivi karibuni, ni kwamba kwenye elimu adimu ya vivuli miaka iliyopita watengeneza filamu walisumbuka kutumia miale ya taa inayokinzana ili kuua kivuli.
Mtu mmoja aliyekuwa na fikra mbadala alipingana na dhana hiyo na kuua mtindo huo uliosumbua kutokana na kuhitaji vifaa vingi, kwamba hakuna kiumbe au kitu kisichokuwa na kivuli!
Fikra ya pili kuhusu kivuli ingawa haifahamiki sana inahusiana na binadamu, ikitokea siku hukioni kivuli chako unaposimama kwenye mwanga basi anza kuandika wosia maana muda wako wa kufarikiana na dunia umewadia.
Sikutishi, lakini ni elimu adimu mbadala ambayo si wengi mnaifahamu, tuliache jambo hilo kwa sababu si mahala pake, ingekuwa inahusiana na elimu ya ulozi na uganguzi ningekuchambulia.
Kwenye siasa kuna vivuli vyenye mgawanyiko wa aina tatu: ‘Umbra’ ‘Penumbra’ na ‘Antumbra’ na ndicho nilichokiona katika kikao cha CCM, ambacho kilisisimua kutokana na Mwenyekiti wao Rais John Magufuli kuzingatia Katiba ya chama na kunyofoa ‘vilemba vya ukoka’ vilivyokuwa vinautwisha mzigo chama hicho na kusababisha migagasuko kwenye chaguzi za viongozi wa chama.
 Kwamba kwa staili yake ya kubinya matumizi yasiyo ya lazima kwa kupunguza baadhi ya nafasi kwenye NEC, ni sawa kwa muktadha wao kichama kama wamekubaliana pia kuzingatia nafasi za uongozi kwa mujibu wa kanuni za chama zinazobainishwa na Katiba ya chama hilo ni sawa pia.
Mkakati wa kupata wagombea bora wa nafasi za uongozi kwenye uchaguzi ujao wa CCM mwakani kitakapotimiza miaka 40 nalo ni jambo la kheri kabisa.
Mikakati kadhaa ya mabadiliko ndani ya chama ili kiwe imara kwa kuongeza idadi ya wanachama vijana, kuondoa wanachama hewa wanaoibuka wakati wa uchaguzi wa viongozi wa chama, kupiga vita rushwa katika mchakato wa uchaguzi yote hayo ni maazimio mazuri ambayo nadhani yataondoa ‘takrima’.
Pia rasilimali za chama kutumika kwa manufaa ya chama na wanachama badala ya ‘wapigaji’ inapaswa kuungwa mkono na wanachama wote wa chama hicho kikongwe.
Tena baadhi ya vipaumbele vya mkakati wa mabadiliko vimechelewa, kwani kuwepo kwa harufu ya mlungula ingawa haiwezi kuthibitishwa moja kwa moja kila uchaguzi wa chama unapofanyika ni jambo ambalo hata muasisi wa chama hicho Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kulikemea sana katika baadhi ya hotuba zake.
 Kingine kilichonifurahisha ni mabadiliko ya ngazi mbalimbali za uongozi ndani ya chama yaliyofanyika katika kikao hicho, si kwamba waliotoka hawakufaa ukiachilia mbali majukumu mbadala waliyokasimiwa na kulazimika kuachia nafasi hizo, lakini pia nafasi moja kuhodhiwa na mhusika mmoja kwa muda mrefu haiwezeshi kupata fikra mbadala ingawa katika kutimiza majukumu hufuata kanuni za wadhifa huo kwa mujibu wa Katiba.
Kuna mawili ambayo hayakuwa sawa, la kwanza ni CCM kukimbia kivuli chake hususan kwa jinamizi linalokiwewesesha kwa kutaka kuwashughulikia wasaliti tena wakilengwa zaidi wanaohisiwa kuwasaidia vinara waliojiondoa kutoka chama hicho na kujikita kwenye upinzani.
Kwamba wasaliti walioko ndani wanawauzia siri za chama na kusababisha changamoto kubwa wakati wa uchaguzi wa serikali mpya.
Tafakuri yangu ina mtazamo mbadala kwamba kuna wasaliti wa ndani wanaowatumikia walioko ndani ya chama na kuifikisha CCM katika hali ambayo sasa Mwenyekiti wake amepania kupambana na rushwa, wanachama hewa na kofia zaidi ya moja yakiwa machache kati ya mengi ya kurekebishwa.
 CCM ikijelekeza kwenye jinamizi hilo badala ya kung’oa mzizi wa ndani wa fitna maana yake ni kwamba inatazama kivuli cha tatu ‘Antumbra’ badala ya kuangalia kivuli cha kwanza ‘Umbra’ lakini pia ni sawa na mtu asiyetaka kuona kivuli chake, ikimaanisha kuwa anajibashiria kufarikiana na dunia bila kujali itatokea ndani ya muda gani. Kwani, hata vyama vyenye historia tukuka za kisiasa duniani havijawahi kuwa na matukio kama yanayoikuta CCM, kwa wanachama kuhama kutokana na kukwazika au kutokubaliana na mambo yaliyotokea?
Endesheni siasa za kuimarisha chama badala ya kuweweseka kwa waliokihama chama, msije kuwa sawa na bondia anayeweweseka usingizini akilitaja kwa kihoro jina la mpinzani wake atakayepambana naye kwenye masumbwi.
Ikiwa hivyo inamaanisha kuwa anamhofia kabla hajakabiliana naye! La pili ni vyama vingine pia kukaribishwa kufanyia vikao Ikulu kwa kuwa CCM wamefanyia hapo, lakini lazima ajenda zao zifahamike! Inanipa ukakasi, kama vikao vyao tu vya ndani vilivyopaswa kufanyika kwenye hoteli vilizua hamkani na kuzimwa itakuwa kufanyia ikulu!? Sijui, labda inawezekana tafakuri yangu imekosea, lakini sidhani!