32.2 C
Dar es Salaam
Sunday, November 24, 2024

Contact us: [email protected]

KAFULILA AREJEA CHADEMA KUZUIA HARAKATI ZA ZITTO

ALIYEKUWA mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, David Kafulila
ALIYEKUWA mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, David Kafulila

NA EVANS MAGEGE,

ALIYEKUWA mbunge wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya NCCR-Mageuzi, David Kafulila, ameachana na chama hicho na kurejea Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), alichokitumikia siku za nyuma.

Kafulila alitangaza kuchukua uamuzi huo jana na alisema ameamua kurejea Chadema ili kuungana na wahitaji wa mabadiliko.

Taarifa za ndani ambazo MTANZANIA Jumamosi imezipata zinasema Kafulila ameamua kukihama chama hicho kwa sababu kimepoteza mvuto mkoani Kigoma, licha ya kwamba mwaka 2010 alitumwa na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, kwenda kukisaidia kwa miezi michache kukijengea mtandao uliosababisha kipate ushindi katika majimbo manne, likiwamo la kwake la Kigoma Kusini, Buhambwe ambalo Mbunge alikuwa ni Felix Mkosamali, Kasulu Mjini ambalo Mbunge alikuwa ni Moses Machali na Kasulu Vijijini ambalo Mbunge alikuwa ni Agripina Buyogera, lakini katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25, mwaka jana, kimepoteza majimbo hayo.

Taarifa hizo zinasema kuwa, baada ya Kafulila kujiunga atapewa jukumu la kuiimarisha zaidi Chadema mkoani humo, ambako ni ngome ya kisiasa ya Mbunge wa Kigoma Mjini na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT–Wazalendo, Zitto Kabwe, ambaye awali alikuwa ni mshirika wake wa kisiasa, lakini kwa sasa ni hasimu wake wa kisiasa.

Pia taarifa hizo zinasema kuwa, Kafulila atapewa jukumu la kuongoza kanda ya Chadema itakayojumuisha mikoa ya Kigoma, Rukwa na Tabora, ili kupambana na ACT-Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM).

Taarifa hizo zinasema dhumuni la Kafulila kupewa jukumu la kuongoza mikoa hiyo ni kusaidia kuongeza nguvu ya ushindi ya Chadema katika uchaguzi utakaofanyika miaka michache ijayo, ukiwamo wa Serikali za Mitaa.

Wakati taarifa hizo zikiainisha majukumu atakayopewa Kafulila katika mikoa hiyo, pia aliyekuwa mgombea urais wa Chadema katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana ambaye pia ni Waziri Mkuu wa zamani na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa, yuko mkoani Tabora akifanya vikao vya ndani vya chama hicho na kufanya mazungumzo na wanachama na viongozi mbalimbali.

Pia taarifa zaidi zinasema kuwa, Kamati Kuu ya Chadema imekutana juzi kwa siri Tabora, wakati Lowassa akiendelea na ziara yake mkoani humo na hadi sasa vyombo vya habari havijatangaziwa kilichojadiliwa au pengine kama mkakati wa kumpa Kafulila majukumu mapya ndani ya chama hicho nao ulijadaliwa.

Hata hivyo, akizungumza na gazeti hili baada ya kuwasilisha barua ya kujivua uanachama wa NCCR-Mageuzi, Kafulila alisema amefanya hivyo kwa kuamini kwamba anakwenda kukaa na timu kubwa yenye nia ya kufanya mabadiliko ya kweli kwa mustakabali wa Watanzania wote.

Aliongeza kwamba, kujiunga kwake Chadema ni msimamo wake wa kutokata tamaa ya changamoto za kisiasa.

Kafulila, aliyekuwa mbunge wa Kigoma Kusini kuanzia mwaka 2010 hadi mwaka 2015, alisema anaamini ndani ya chama hicho ataongeza ufanisi zaidi wa kupigania mabadiliko ya siasa ya nchi.

“Leo (jana mchana) muda huu nimewasilisha barua ya kujivua uanachama wa NCCR-Mageuzi na ninajiandaa kujiunga na Chadema. Nimewashukuru kwa kuwa pamoja katika kujenga chama na nafasi ya uenezi waliyonipa mara zote.

“Nimeweka wazi kuwa natarajia kujiunga Chadema na sababu nimesema kuwa ni mahitaji ya wenye nia ya mabadiliko kuwa chama kimoja kufupisha safari hiyo,” alisema Kafulila.

Mwanasiasa huyo machachari alianza kuvuma kisiasa wakati akikitumikia Chadema, lakini aliingia katika mvutano na uongozi wa chama hicho miezi kadhaa kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010.

Kutokana na mgogoro huo, uliofukuta kwa misingi ya tuhuma za usaliti, aliamua kukihama na kujiunga NCCR–Mageuzi.

Akiwa mwanachama mgeni ndani ya NCCR-Mageuzi, Kafulila alichukua fomu ya kugombea ubunge wa Kigoma Kusini, ambapo alishinda kiti hicho.

Ndani ya kipindi cha miaka mitano ya ubunge wake alijijenga zaidi kisiasa na kujikuta akiwa katika kundi la wabunge machachari zaidi wa Bunge la 10.

Katika moja ya mambo ya kukumbukwa aliyoyaibua wakati wa Bunge hilo ni sakata la ukwapuaji wa Sh bilioni 300 zilizokuwa zimehifadhiwa katika Akaunti ya Tegeta Escrow, iliyokuwa chini ya usimamizi wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), wakati majadiliano ya kumaliza mgogoro wa tozo ya malipo kati ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL yakiendelea kufanywa.

Pamoja na kupata sifa kubwa ya kisiasa ndani na nje ya nchi, Kafulila alishindwa kutetea kiti chake cha ubunge katika uchaguzi wa mwaka jana, ambapo alishindwa na Mbunge wa sasa wa Kigoma Kusini, Husna Mwilima (CCM) na mara moja alikwenda mahakamani kupinga matokeo hayo, lakini hakufanikiwa.

Pia Kafulila amewahi kupata misukosuko katika maisha yake ya kisiasa ndani ya NCCR-Mageuzi hadi kufikia hatua ya kutaka kuvuliwa uanachama yeye na wenzake watano waliowahi kutuhumiwa kuchochea usaliti wa kutaka kumpindua Mbatia.

Tuhuma hizo zilimuunganisha yeye na aliyekuwa mgombea urais wa NCCR-Mageuzi katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010, Hasheem Rungwe, Ally Omari, Mbwana Hassan, Josam Rugugila, Lucy Kapya na Jamwe Batifa na ziliwalazimu wajumbe wa Halmashauri Kuu ya chama hicho kuwavua uanachama.

Hata hivyo, alinusurika kuvuliwa uanachama baada ya kumwomba radhi Mbatia, ambaye alimsamehe.

Kuondoka kwa Kafulila ndani ya NCCR-Mageuzi kunaongeza idadi ya wanasiasa vijana ambao hivi karibuni wamevihama vyama vyao.

Wanasiasa hao ni pamoja na Machali, ambaye katika uchaguzi wa mwaka jana aligombea kwa tiketi ya ACT-Wazalendo, akitokea NCCR-Mageuzi, lakini hivi karibuni aliamua kujiunga na CCM.

Mbali na Machali, pia aliyekuwa mgombea ubunge wa ACT-Wazalendo Jimbo la Morogoro Mjini, Selemani Msindi, maarufu kwa jina la Afande Sele, naye alijivua uanachama wa chama hicho.

Uamuzi huo wa Afande Sele umekuja siku chache baada ya Katibu wa Kamati ya Mipango wa ACT-Wazalendo, Habib Mchange, kujivua uanachama na kutangaza kuachana na siasa na kufanya shughuli zake za ujasiriamali.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles